Kigoma kinara usajili mashamba Tanzania bara
- Inaongoza Tanzania bara kuwa na mashamba mengi yaliyopimwa na kusajiliwa.
- Mashamba hayo yamefungua fursa mbalimbali za kilimo na kuufanya mkoa huo kuongoza nchini kwa kilimo cha mihogo.
- Wadau washauri wananchi wa maeneo mengine kuchukua hatua muhimu za kisheria kumiliki mashamba.
Dar es Salaam. Ukitaja mikoa inayosifika kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara Tanzania, basi hautaacha kuutaja mkoa wa Kigoma. Kwa nini Kigoma? Wengi watakuambia ni kitovu cha uzalishaji wa mawese yanayotokana na miti ya michikichi.
Lakini wakazi wa Kigoma hawako nyuma katika uzalishaji wa mihogo. Kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka ya utafiti wa sekta ya kilimo (AASS 2016/17) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa Kigoma inaongoza kwa kilimo cha mihogo ambapo kati ya tani 572,727 za mihogo zinazozalishwa Tanzania bara basi 219,708 zinatoka Kigoma sawa na asilimia 38.4.
Huenda mafaniko hayo yanachangiwa zaidi na hatua iliyopigwa na mkoa huo katika mpango wa kupima mashamba ya wakulima yanayotambulika kisheria.
Ripoti ya AASS 2016/2017 inaeleza pia kuwa Kigoma ndiyo mkoa unaoongoza Tanzania Bara kwa kuwa na mashamba mengi yaliyopimwa na kusajiliwa ambayo yanatumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya mashamba 1. 5 milioni yaliyosajiliwa nchini, basi mashamba 246,327 sawa na asilimia 16.1 yako Kigoma. Hiyo ina maana kuwa mkoa huyo ndiyo unaoongoza Tanzania bara kwa mashamba mengi yaliyopimwa na kusajiliwa kisheria.
Mikoa mingine iliyopiga hatua ya kusajili mashamba ni Tabora, Pwani, Tanga na Shinyanga. Hali hiyo imechochewa zaidi na hamasa na muamko wa wananchi kufahamu haki na wajibu wao wa kutunza na kuendeleza rasimali muhimu kama ardhi.
Lakini mikoa ya Rukwa, Katavi, Dar es Salaam, Njombe na Arusha iko kwenye kundi la mikoa yenye mashamba machache yaliyopimwa licha ya kuwa na eneo kubwa linalotumika katika shughuli za kilimo.
Asilimia ya waliosajili mashamba kwa mikoa yote ya Tanzania Bara
Ripoti ya mwaka ya utafiti wa sekta ya kilimo (AASS 2016/17)
Kwanini mashamba yasajiliwe?
Usajili wa mashamba husaidia katika kuepusha migogoro mbalimbali ya ardhi ambayo inatokea kwa mtu kukosa hatimiliki ya eneo lake au kuingia katika eneo lisilo lake kwasababu ya kukosa mipaka inayotambulika kisheria.
“Inaongeza thamani ya ardhi na hivyo mkulima anaweza hata akapata mkopo kutoka benki kwasababu tu amesajili shamba lake,” anasema Salum Hamidu, Mtaalamu wa masuala ya ardhi kutoka Jijini Dar es Salaam.
Ili kuhakikisha mashamba na viwanja vinapimwa na kusajiliwa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwaka 2015 ilianza kutekeleza programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi Nchini katika halmashauri za wilaya 24, miji 25 na 10 inayokuwa kwa kasi na shughuli hiyo inaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika programu hiyo, vigezo vinavyozingatiwa zaidi ni aina na idadi ya migogoro ya ardhi iliyopo katika eneo husika pamoja na ukubwa wake. Idadi na aina ya mifugo, ukubwa wa ardhi katika matumizi mbalimbali.
Vilevile kiwango cha uwekezaji, shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika eneo husika, idadi ya watu katika eneo husika, mikoa na wilaya mpya pamoja na kasi ya ujenzi.
Kigoma imeonyesha njia kwa maeneo mengine nchini kutumia fursa kusajili na ili kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu.
Shamba lililopimwa linamsaidia mkulima kutumia njia za kisasa za kulima mazao kwa kuzingatia vipimo sahihi vya dawa, mbolea na mbegu zinazotakiwa kutumika ili kuleta matokeo chanya.
Hamidu anawashauri wananchi wakiwemo wakulima wenye mashamba kupima ili kupata umiliki rasmi na kuepuka migogoro mbalimbali inayoweza kujitokeza wakati wa uzalishaji.