Kanda ya Ziwa yatawala biashara ya madini, yavuna Sh4 trilioni 2025/26
- Mauzo ya madini Kanda ya Ziwa yaliongezeka kwa asilimia 5.79 kutoka Sh3.8 trilioni iliyorekodiwa mwaka wa fedha 2024/25.
Dar es Salaam. Kanda ya Ziwa nchini Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kinara wa biashara ya madini nchini baada ya kurekodi mauzo ya Sh4.02 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2025/26, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa ndani ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa ripoti ya utendaji wa uchumi wa kanda inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mauzo hayo ni sawa na asilimia 58.6 ya mauzo yote ya madini nchini.
Mauzo ya madini Kanda ya Ziwa yaliongezeka kwa asilimia 5.79 kutoka Sh3.8 trilioni iliyorekodiwa mwaka wa fedha 2024/25.
Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa maeneo muhimu zaidi katika uchumi wa Tanzania yakiwa kitovu cha sekta ya madini inayochangia asilimia 11.9 ya Pato la Taifa (GDP)

Kanda hiyo inajumuisha mikoa ya Geita, Mwanza, Kagera, Mara na Simiyu ambayo ni maarufu kwa uchimbaji dhahabu pamoja na Mkoa wa Shinyanga ambao unaojulikana zaidi kwa uchimbaji almasi.
Kwa upande wa kanda nyingine, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imeshika nafasi ya pili ikirekodi Sh1.92 trilioni, Kanda ya Kati Sh626.58 bilioni huku Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Kusini Mashariki zikirekodi Sh149.07 bilioni na Sh119.56 bilioni mtawalia.
Dhahabu yaendelea kutawala soko
Mbali na kuwepo kwa shughuli za uchimbaji wa madini aina tofauti, ripoti hiyo inaonyesha kuwa dhahabu iliendelea kuwa kinara wa mauzo ikichangia asilimia 86.3 ya mauzo yote.
Katika kipindi hicho, uzalishaji wa dhahabu ulifikia kilo 54,467.7, ambazo kwa mujibu wa BoT thamani yake ni Dola za Marekani 4.83 bilioni sawa na takriban Sh12.78 trilioni.