Kamati ya bunge ya miundombinu yatoa maagizo mazito Temesa

March 18, 2022 11:43 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Yataka wakala huo ujiendeshe kibiashara.
  • Yaagiza iboreshe mifumo ya ukusanyaji mapato na wafanyakazi.

Mwanza. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imemwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Lazaro Kilahala  kuhakikisha anaibadilisha taasisi hiyo ili iweze kujikwamua kiuchumi kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso ametoa agizo hilo baada ya kamati hiyo kutembelea shughuli zinazofanywa na Temesa jijini Mwanza na kubaini kuwepo kwa mapungufu mengi yanayoikosesha mapato Serikali.

Kakosa amemtaka Kilahala kufanya mabadiliko ya kimfumo ili taasisi hiyo iweze kujiendesha kibiashara sambamba na kutoa huduma ambayo itakuwa kivutio cha wateja wengi wa ndani na nje.

“Ijiendeshe kibiashara maana yake kwanza iwe na mafundi wengi ambao watafanyakazi inayovutia watu ma mazingira bora ya kufanyia kazi,” amesema Kakoso.

Amesema katika karakana zote mbili za utengenezaji wa magari na ile ya vivuko walizopitishwa wamebaini kuwepo uozo mkubwa na hivyo kusababisha karakana za Serikali kutelekezwa au kuchukuliwa na watu binafsi.

“Ndiyo maana utakuta asilimia kubwa ya magari yanayotengenezwa kwenye karakana za Serikali mengi yanaharibika kutokana na kufungiwa na vifaa vibovu pamoja na mifumo ya wafanyakazi kuwa ya ovyo,” amesema.

Ameshauri kwenye karakana hizo wahakikishe viongozi wa Serikali wanakuwepo watakaosimamia ili kupunguza ajali zinazosababishwa na ubovu wa vivuko.

“Kanda ya Ziwa na ndani ya Ziwa Victoria tuna rekodi ya kuwa na ajali nyingi za majini na nchi kavu na hii inasababishwa na usimamizi mbovu kwenye karakana zetu hivyo ni shauri kila karakana awepo msimamizi wa Serikali,” amesema Kakoso.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi  ya Temesa, Mtendaji  Mkuu wa Temesa, Kilahala amesema wamejipanga  kuboresha Mazingira ya utendaji kazi kwenye karakana hiyo ili iweze kuleta matokeo mazuri.

Amesema kufuatia maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo watayafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuandaa taarifa za kina za utekelezaji wa miradi wanayoisimamia na kuiwasilisha kwenye kikao cha kamati hiyo mjini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amekiri kutokuwepo kwa rekodi nzuri kwenye taasisi hiyo licha ya dhamira ya Serikali kuifanyia mabadiliko.

“Ni kweli kuwa Temesa ni kama imeshindwa kujisimamia licha ya Serikali kutoa fedha nyingi lakini bado haijawa na rekodi nzuri na haizingatii kama inabeba hatma za Watanzania,” amesema Mhandisi Kasekenya. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV