Jinsi ya kujifunza lugha za kigeni kwa njia ya mtandao
- Kinachotakiwa ni nia tu kwa sababu teknolojia zipo.
- Unaweza kujifunza kupitia programu tumishi ikiwemo Duolingo.
- Teknolojia hizo zimeonyesha ufanisi mkubwa kwa watumiaji.
Dar es Salaam. Kati ya maarifa ambayo Nukta Habari (nukta.co.tz) imekuwa ikiyataja kuwa muhimu kujifunza hasa kwa vijana ili kuongeza uwanda wao wa ajira ni kujifunza lugha za kigeni.
Wapo wanaozingatia lakini wapo baadhi ambao bado wanajiuliza njia za kujifunza lugha za kigeni na wengine kutokuthubutu hata kufuatilia kwa kuhofia gharama za ada au hawana muda wa kwenda shule tena.
Hata hivyo, kwa karne hii ya 21, unaweza kujifunza lolote lile hasa kwa njia ya mtandao kwani teknolojia imeimarishwa.
Makala haya yanakusogeza na teknolojia za kurahisisha mafunzo ya lugha mpya kwa njia ya mtandao ambayo wataalamu wa lugha wamekiri kushuhudia yakifanya kazi.
Unaweza kutumia simu za video za WhatsApp kujifunza lugha mpya. Picha| Arabiya in Egypt.
Penye nia pana njia
Zipo programu tumishi mbalimbali (app) nyingi mtandaoni ambazo mtu anaweza kuchagua kutumia kujifunza lugha mpya ya kigeni.
App kama Duolingo, Pimsleur, Rosetta Stone, HelloTalk na YouTube ni baadhi ya app zinazotoa elimu kwa njia ya mtandao.
Licha ya kuwa app hizo zinahitaji kulipiwa, wadau wa Nukta Habari wamethibitisha kusaidika nazo.
Mwanafunzi wa shahada ya udhamili katika Chuo Kikuu cha Kiadventista cha Friendensau nchini Ujerumani, Verediana Mwashi amesema baada ya kukubaliwa kujiunga na chuo hicho, ilimlazimu ajifunze lugha ya Kijerumani ili kufanikisha masomo yake.
“Niliingia darasani miezi sita baada ya hapo nimekuwa nikitumia mtandao wa YouTube kujifunza. Inawezekana ukiwa na nia,” amesema Mwashi.
Gharama siyo kikwazo kikubwa
Baadhi ya apps za kujifunza lugha za kigeni kikiwemo Kiengereza unalazimika kulipa kiasi fulani cha fedha ili kupata maarifa ya lugha husika.
Kwa app ya Duolingo, unahitaji takriban Sh16,200 kwa mwezi kutumia app hiyo isiyokuwa na matangazo. Lakini kama ukiwa na uvumilivu, unaweza kutumia bure huku ukikatizwa na matangazo ya hapa na pale.
Kwa upande wa YouTube, unachohitaji ni bando lako tu kujifunza na kuhakikisha kuwa umepata mwalimu mzuri ambaye masomo yake yanafuata mwongozo wa mafunzo ya lugha hiyo.
Programu ya Pimsleur inahitaji Sh48,500 kwa mwezi huku Rosetta Stone ikidai Sh27,800 kwa mwezi au unaweza kuinunua moja kwa moja kwa takriban Sh700,000.
Unachohitaji ni nia ya kujifunza. Picha| The Life Long Learner.
Wanafunzi, watu wazima wanufaika
Njia ya mtandao imeonekana ikifanya kazi siyo kwa watu wazima tu bali hata wanafunzi waliofikiwa na huduma hiyo.
Mratibu Chama cha Waalimu wa Kiingereza Tanzania (Telta), Mwalimu Ayoub Msuya ameiambia Nukta Habari kuwa, mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwa njia ya mtandao yanayoratibiwa na chama hicho yamezaa matunda kwa wanafunzi wengi wa kidato cha pili na cha nne.
Mwalimu Msuya amesema, walichokifanya ni kuwakabidhi simu zenye bando wazazi na kuweka utaratibu wa wanafunzi kutumia simu hizo siku za wikiendi kwa ajili ya kujifunza.
“Jumamosi mwalimu anafundisha kwa njia ya zoom na kutoa maswali ambayo wanafunzi wanawasilisha kwa njia ya zoom au whatsapp kwa video, sauti na maandishi,” amesema Mwalimu Msuya ambaye ni mwalimu wa Kiingereza katika Shule ya Sekondari Jangwani mkoani Dar es Salaam.
Soma zaidi
- Sababu zinazofanya upate ugumu kujifunza lugha ya pili kama Kiingereza
- Zingatia haya wakati ukiwasiliana na mteja wako
- ‘Apps’ zinazoweza kuwasaidia wazazi katika malezi ya watoto
Siyo kwa lugha tu na masomo mengine
Mafunzo ya njia ya mtandao hayawezi kuishia katika lugha pekee bali hata katika masomo mengine.
Mwalimu Msuya amesema kama iliwezekana kwa somo la Kiingereza kufanya vizuri, inawezekana kwa masomo mengine pia endapo itatengenezwa mifumo mizuri.
“Mafunzo kwa njia ya mtandao yanachangamkiwa na waalimu zaidi. Wanafunzi bado mwamko ni mdogo lakini huenda ni kwasababu hamna vifaa kwani sheria ya elimu haimruhusu mtoto kumiliki simu.
“Wanafunzi wote waliokuwa wakijifunza lugha kupitia Telta wamefaulu vizuri somo la Kiingereza hadi katika ngazi ya mkoa,” amesema Mwalimu Msuya.
Hata hivyo, Mwalimu Msuya amesema mafunzo kwa njia ya mtandao yanampatia mawanda mapana zaidi mwanafunzi kujifunza kutoka katika vyanzo vingi.
Hata hivyo, inashauriwa na waalimu pia wajisasishe ili kuendana na kasi ya teknolojia.
Latest
