GST yawatoa hofu wananchi kuanguka kwa ‘kimondo’ mkoani Kagera

November 30, 2018 11:17 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kitu hicho kilichokuwa na mwanga mkali na cheche kikitokea angani kilisababisha ngurumo na mitetemo midogo mnamo majira ya saa tatu usiku wa Novemba 27, 2018.
  • GST imewaomba wakazi wa mkoa huo waendelee kufanya kazi zao za maendeleo kwa sababu kitu hicho kilichoanguka ardhini hakina madhara yoyote kwa maisha yao.
  • Hapa nchini kumewahi kudondoka kimondo katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe kilichogunduliwa mwaka 1930 na kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12.

Dar es Salaam. Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewatoa hofu wananchi wa mkoa wa Kagera na kuwaomba waendelee kufanya kazi zao za maendeleo kufuatia kudondoka kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni “kimondo” katika mkoa huo.

Taarifa iliyotolewa mapema leo na GST imesema kitu hicho kilichokuwa na mwanga mkali na cheche kikitokea angani kilisababisha ngurumo na mitetemo midogo mnamo majira ya saa tatu usiku wa Novemba 27, 2018.

Kwa kawaida vimondo hivi havina athari kwa watu na mali zao kama havijaanguka katika miundo mbinu iliyopo. Aidha, vimondo hivi husababisha mitetemo midogo vinapodondoka katika uso wa dunia. 

GST inaeleza kuwa tukio hilo ni la kawaida na hutokea maeneo mbalimbali duniani na hadi sasa matukio zaidi ya 1,400 yamesharipotiwa.

“Vimondo ni majabali ya miamba ambayo yanapatikana katika mfumo wa Sayari wa ulimwengu (outer space) katika anga za mbali. Majabali hayo ni sehemu ya vipande vya sayari ndogo (asteroids) au vipande vikubwa vya miamba (meteoroids) vilivyovunjika kutokana na sababu ya nguvu za asili,” imeeleza sehemu ya taarifa ya GST.

Kuvunjika kwa sayari ndogo na vipande vikubwa vya miamba husababisha vipande vya miamba kuzunguka bila mpangilio katika mihimili hivyo hugongona na kupoteza uelekeo na kuingia katika anga la Sayari ya dunia. 


Zinazohusiana: Wachimbaji wadogo wa madini Geita kupatiwa mikopo kuendeleza rasimali zao.


Kutokana na uzito mkubwa wa majabali hayo na nguvu ya uvutano ya dunia (gravitational force), majabali hayo hudondoka kwa kasi kubwa kwenye uso wa Dunia ambapo msuguano baina ya majabali hayo na hewa iliyopo katika anga la Dunia husababisha kutokea kwa cheche za moto na mwanga mkali wakati yanadondoka.

Kimondo kilichodondoka katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe. Picha| Youtube.

Hapa nchini kumewahi kudondoka kimondo katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe kilichogunduliwa mwaka 1930 na kinakadiriwa kuwa na uzito wa tani 12 chenye ukubwa wa kimo cha mita 1.22, upana wa mita 1.63 na urefu wa mita 3.3. 

Kimondo hicho ni mojawapo ya vimondo vizito kumi vinavyojulikana ambacho  ni cha nane kwa ukubwa duniani na cha pili kwa ukubwa Afrika. 

“Kimondo hiki ni kati ya vimondo vinavyofahamika duniani kudondoka katika sehemu ya nchi kavu kwenye uso wa dunia, kwa sababu vipo vingi vilivyodondoka katika sehemu za majini kama kwenye bahari na maziwa mbalimbali duniani,” inaeleza taarifa hiyo.

Kutokana na sintofahamu iliyowakumba wakazi wa Kagera, GST inawatoa hofu wananchi wa mkoa huo na kuwaomba waendelee kufanya kazi zao za maendeleo kwasababu kitu hicho hakina madhara yoyote kwa maisha yao.

Hata hivyo, bado haijawa bayana kitu hicho kilidondokea maeneo gani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW