Brenda Msangi kung’atuka CCBRT Machi 2027
- Ni baada ya kuitumikia CCBRT kwa miaka 17, na miaka 8 kama Mkurugenzi Mtendaji.
- Atang’atuka wakati ambao CCBRT ipo kwenye hatua muhimu ya kuimarisha uendelevu wa taasisi na upanuzi wa huduma.
Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya CCBRT imetangaza kumpa mkono wa kwaheri Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Brenda Msangi ifikapo Machi 31, 2027.
Taarifa ya Dk Redempta Mbatia, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CCBRT iliyotolewa Julai 20, 2026 inabainisha kuwa uamuzi huo ni sehemu ya mchakato wa muda mrefu wa hospitali hiyo.
“Mabadiliko haya ya uongozi ni sehemu ya mchakato uliopangwa wa kurithi uongozi ambao bodi imekuwa ikiutayarisha kwa muda wa miezi 18,” amesema Mbatia.
Brenda aliyeitumikia CCBRT kwa zaidi ya miaka 17 alikuwa Mtanzania na mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Desemba 2018 wakati ikiwa katika kipindi cha mageuzi ya huduma zake za afya.
Mwanamama huyo atang’atuka katika nafasi hiyo wakati ambapo CCBRT ipo kwenye hatua muhimu ya kuimarisha uendelevu wa taasisi, kupanua huduma zake na kuongeza uwezo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Mbatia, bodi itaanza mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mtendaji ajaye, huku Brenda akiendelea kuiongoza CCBRT hadi Machi 31, 2027 na kushirikiana na bodi kuhakikisha mabadiliko ya uongozi yanafanyika kwa utaratibu maalum.

Brenda Msangi ni nani?
Brenda Msangi ni mmoja wa viongozi wanawake wanaotajwa katika mageuzi ya sekta ya afya nchini Tanzania, akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika uongozi wa taasisi za afya, dawa na mifumo Afrika na Ulaya.
Alizaliwa na kukulia mkoani Dar es Salaam ambapo alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi Oysterbay kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani kwa ngazi zote mbili za elimu ya sekondari.
Akiwa mwanafunzi wa kidato cha tano na sita alisoma mchepuo wa sayansi (PCB), lakini ndoto yake ilielekezwa zaidi kwenye taaluma ya famasia badala ya udaktari.
Baadaye alijiunga na ngazi za juu za elimu nchini Uingereza ambako alipata Shahada ya Uzamili ya Famasia kutoka Chuo Kikuu cha Brighton na baadaye Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara katika Sekta ya Afya (MBA Healthcare) kutoka Chuo Kikuu cha Plymouth na baadae kupata mafunzo ya uongozi wa bodi kutoka Harvard Business School Executive Education.
Baada ya masomo, Brenda alianza safari yake ya kitaaluma katika sekta ya afya nchini Uingereza, ambako alipata nafasi ya kusimamia timu katika sekta ya famasia.
Mwaka 2009 alirejea Tanzania na kujiunga na CCBRT kama Naibu Mkurugenzi wa Programu za Jamii, nafasi iliyompa uzoefu mkubwa katika usimamizi wa huduma za afya na maendeleo ya jamii.

Baadaye alipanda ngazi na kuwa Afisa Mkuu wa Uendeshaji (Chief Operating Officer) kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT Desemba 2018.
Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brenda ameongoza taasisi hiyo katika kipindi cha mageuzi yaliyolenga kuimarisha uendelevu wa kifedha, kuboresha mifumo ya utoaji huduma na kupanua ushirikiano kati ya Serikali, wafadhili na sekta binafsi.
Chini ya uongozi wake, CCBRT imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi kubwa za afya nchini zinazotoa huduma za matibabu na urekebishaji wa viungo kwa jamii zenye uhitaji.
Mbali na nafasi yake CCBRT, Brenda amekuwa akihudumu katika bodi mbalimbali zikiwemo CEO Roundtable of Tanzania, World Vision Tanzania na taasisi nyingine, akijikita katika masuala ya utawala bora, usimamizi wa hatari, maendeleo ya rasilimali watu na uendelevu wa taasisi.
Pia ni mwanzilishi wa jukwaa la ‘Dear Girl Child BMK’ linalolenga kuwawezesha wasichana na wanawake katika uongozi na kujenga kujiamini.