Bodi iliyowahi ‘kuvunjwa’ na Kigwangalla yapewa kibarua kingine kukuza utalii Tanzania
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla akizindua rasmi Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) jijini Dodoma. Bodi hiyo imeongezewa muda wa miaka mitatu na Rais John Magufuli Aprili 23 mwaka huu. Picha|Wizara ya Maliasili na Utalii.
- Yaagizwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano na mbinu rahisi kutangaza vivutio vya utalii.
- Pia yaagizwa kuwaleta watu mashuhuri duniani walau watano kila mwaka.
- Bodi hiyo ina wajumbe sita na inaongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo.
Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iwekeze zaidi katika matumizi ya njia za kisasa za mawasiliano na mbinu rahisi zenye gharama nafuu kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Dk Kigwangalla ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akizindua rasmi bodi hiyo iliyoongezewa muda wa miaka mitatu na Rais John Magufuli, Aprili 23 mwaka huu.
Bodi hiyo ni ile aliyowahi kuivunja Januari 18 mwaka huu akidai kuwa ilishindwa kutekeleza majukumu yake lakini baadaye Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo aligoma kuachia ngazi kwa madai kuwa Waziri huyo alikuwa hana mamlaka ya kuivunja.
Ameitaka Bodi hiyo iendelee kubuni na kuongeza mbinu mpya za kutangaza utalii zitakazoleta tija na matokeo ya haraka.
“Bodi ya Utalii mnapaswa kuona fursa zilizopo na kutimiza majukumu mliyopewa kwa tija na ufanisi zaidi. Namna pekee ya kufikia malengo hayo ni lazima mtumie teknolojia na mbinu rahisi za mawasiliano zenye gharama nafuu kutimiza majukumu yaleyale ya kutangaza vivutio vya utalii kisasa zaidi,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, wajumbe wa bodi hiyo wametakiwa kushirikiana na taasisi nyingine za Wizara ili kuongezea idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania.
Zinazohusiana:
- Vodacom, Mashercard zaangazia biashara ya mtandaoni kupitia Virtual Card
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni
Aidha, TTB imeshauriwa kuweka mkakati mahususi wa kukamata masoko mapya ya watalii kutoka nchi za Marekani, Hispania, Urusi na nchi za Falme za Kiarabu zikiwemo za Dubai na Oman ambazo watu wake wakiwemo wasomi, wafanyabiashara, wanamichezo na watu maarufu wanapenda kwenda mapumziko ya muda mrefu na kutumia fedha nyingi kwa shughuli za utalii.
“Kama tukiwatumia watu mashuhuri wenye wafuasi wengi wakatembelea vivutio vyetu tuna uhakika watu wengi zaidi watafuatilia ziara zao na kufuata walichokichagua.
“Lazima tuweke mikakati ya kuwaleta watu mashuhuri walau watano kwa mwaka ambao sisi tutawaalika, tutapata mafanikio makubwa sana ndani ya muda mfupi,” amesisitiza Dk Kigwangalla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii amesema kuzinduliwa rasmi kwa bodi hiyo kutaifanya itekeleze majukumu yake kikamilifu akisisitiza kwamba kupitia bodi hiyo sekta ya Utalii Tanzania itasonga mbele kwa kasi kubwa zaidi.
Naye Mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo amemshukuru Rais Magufuli kwa nafasi nyingine aliyompatia kuiongoza bodi hiyo huku akiahidi kuwa bodi yake itafanya kazi kwa kasi na bidii zaidi ili kutimiza malengo ya kuitangaza sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.
Latest