Binti aliyejisomesha kwa biashara za mitumba, viungo vya vyakula

March 7, 2020 9:25 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni binti mwenye miaka 24 ambaye amesema damu yake imejaa biashara.
  • Tangu akiwa kidato cha tano, alianza biashara na kujitegemea kwenye mambo mbalimbali.
  • Kutoka mwanzo wa kuuza kopo 100 la viungo, sasa anauza kopo 700 kwa mwezi.

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokosa mkopo wakilalamika juu ya hali ngumu ya maisha na kubaki kuwa tegemezi kwa wazazi na ndugu zao, wapo ambao wametafuta njia mbadala ya kujisomesha na kujikimu kimaisha.  

Kati ya wachache hao ni Fatuma Mbaga (24) aliyehitimu masomo yake ya shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Morogoro mwaka 2019.

Fatuma ambaye alipata mkopo wa asilimia 80 kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wab Elimu ya Juu (HESLB) aliamua kufanya biashara mbalimbali zikiwemo za kuuza mitumba, kusambaza mchele na kutengeneza viungo vya chakula ili kukidhi asilimia 20 ya malipo ya elimu yake na malazi akiwa chuoni.

Haikuwa rahisi. Unaweza dhani ni bahati ya mtende na “kismati” lakini harakati za binti huyu zinaanzia akiwa Shule ya Sekondari ya Kibasila alipokuwa akisoma kidato cha tano mwaka 2015.

“Mama alikuwa akinipa Sh20,000 kwa ajili ya matumizi ya wiki shuleni. Chakula, sabuni na vitu vyote tulikuwa tunajinunulia wenyewe.

Niliona ninunue nguo makumbusho nikawauzie wanafunzi wenzangu niongeze kipato changu,” amesema binti huyo aliyesema kutokana na kutokuwa na majukumu, alikuwa akiweka akiba.

Akiwa na miaka 19,  Fatuma tayari alifungua mgahawa ambao mtaji wake ulitokana na kuuza mitumba aliyokuwa akiwauzia wanafunzi wenzake.

Kwa siku, binti huyo aliingiza mauzo ya hadi Sh130,000 huku akiajiri wanawake wawili waliomsaidia kazi hiyo wakati akiwa darasani.

Hata hivyo, Safari ya mwanamke mmoja aliyekuwa akisaidia kazi ilifika tamati baada ya hali ya biashara kuwa ngumu na mauzo kushuka.

“Kuna kipindi niliishiwa pesa, nilikuwa na smartphone mbili nikasema Ah! kumbe mtaji natembea nao, nikauza smartphone nikaongeza mtaji,” amesema Fatuma ambaye baada ya kumaliza kidato cha sita alijumuika na msaidizi wake kuendesha mgahawa wake.

Moja ya wafanyakazi katika kiwanda kidogo cha kutengeneza viungo vya vyakula kilichoanzishwa na Fatuma. Picha|Hisani. 

Anguko la kwanza

Kama ilivyo katika kila biashara, kuna kipindi ambacho biashara huwa ngumu na kipindi ambacho mfanyabiashara huneemeka.

Kwa Fatuma, hapa ndipo mlima wa biashara yake ulipoanza.

Akiwa na miaka 20, binti huyo biashara yake ya mama lishe ilianza kusuasua huku mauzo yakishuka siku hadi siku. Hali hiyo ilizua masimango na maswali lukuki kutoka kwa baadhi ya wanafamilia na marafiki yakimbeza kuwa elimu yake haifai kufanya kazi ya mama lishe.

“Nilitafuta oda viwandani. Kote nilipeleka chakula aise!” amesema Fatuma na kubainisha kuwa maneno ya waliomzunguka hayakumkatisha tamaa.

Hata hivyo, nguvu zote zake ziligota mwaka 2016 ambapo alilazimika kuifunga biashara yake baada ya mauzo kuporomoka mara 10 kutoka Sh130,000 hadi Sh13,000 kwa siku.


Bado ana nguvu?

Akiwa chuoni mwaka 2017, Fatuma hakutaka kumsumbua mama yake juu ya matumizi yake ya shuleni na pesa ya kodi. Binti huyo alirudia biashara yake ya mitumba ambapo alisafiri kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam kwenye Soko la Karume kuwachagulia wanafunzi wenzake viwaro.

“Kila ijumaa nilikua naenda soko la Karume, nanunua nguo, narudi getto, naloweka, nafua, naanika, napiga pasi navalisha mdoli napiga picha, naposti na nguo zinaenda,” amesema binti huyo ambaye duka lake linalotembea aliliita “bilionaire boutique”.

Ili kuepuka kama yaliyomtokea awali, Fatuma alifikiria biashara nyingine kwani “udoni” aliokuwa akiwa nao hakutaka upotee kama ilivyokuwa awali.

Fatuma aliamua kuanza biashara ya kusambaza mchele ambapo alipata shule Dodoma na kusambaza mchele ambao alianza na mtaji wa Sh620,000 aliyoipata kwenye kuuza mitumba na kudunduliza.

“Sikutaka kuweka mayai yote kwenye kikapu kimoja,” amesema Fatuma.

Fatuma aliendela kusambaza mchele ambao ulimuingizia faida ya Sh120,000 kila baada ya wiki mbili huku biashara yake ya mitumba ikizidi kumuweka mjini.


Anguko la pili

Wakati Fatuma akifurahia maisha, Shule ambayo alikuwa akisambaza mchele ilikosea kufanya malipo na kulipa fedha zote kwa mfanyabiashara mwenzao ambaye alitokomea na pesa zote.

Hapo ndipo tabu mpya ilipoanza.

“Aliondoka na hela zetu na mimi nilikuwa nimeongeza mtaji. Maisha yakaanza moja na kipindi hicho benki nilikuwa nimebaki na 120,000 tu,” amesema Fatuma.

Hata hivyo, amesema alitafuta kitu kingine cha kufanya kwa kuwa asingeweza kukaa bila cha kufanya.

Fatuma alianza kutengeneza viungo vya vyakula huku akianza na mtaji wa Sh70,000. Kabla ya kuanza kutengeneza viungo kama biashara, awali alikuwa akijihusisha na viungo vya vyakula akiwatengenezea marafiki zake tu kama zawadi lakini hakuona kama ni fursa mahsusi.


Soma zaidi: 


Mwezi wa kwanza kwa binti huyo ulikuwa siyo mbaya sana kwani aliuza kopo siyo chini ya 100.

Kwa kipindi hicho, alikuwa na uhakika wa kupata Sh300,000 kwa mwezi au zaidi kutokana na biashara ya viungo.

“Nilikuwa natengeneza chai masala, mdalasini, pilau masala, tangawizi, iliki, pilipili manga na mchaichai,” amesema Binti Mbaga.

Huenda moyo ya kufanya biashara pia umetokana na ushawishi wa rafiki zake kwa kuwa marafiki wa binti huyo hawakuwa wazembe.

Fatuma amesema marafiki zake wengi ni wafanyabiashara wa nguo na vipodozi na hivyo kukamilisha msemo wa ndege wanaofanana huruka pamoja.

Fatuma akiwa kwenye moja ya maonyesho ya bidhaa mkoani Morogoro. Bidhaa hizo ni moja ya zile zinazolishwa na kampuni yake ya Get Aroma Spices. Picha|Hisani. 

Binti huyo kwa sasa ana kampuni ya “Get Aroma Spices” ambayo inatengeneza viungo mbalimbali vya kupikia na “Get Fahari Packages” ambayo inatengeneza vifungashio vya bidhaa nyingi za wajasiriamali zikiwemo sabuni, losheni, maziwa mchele na unga.

Kutokana na wengi kupenda viungo vyake, Fatuma ameanza kuona mauzo yake ya kipaa kutoka kopo 100 za viungo kwa mwezi mwaka 2018 hadi kufikia wastan wa kopo 700 kwa mwezi hivi karibuni.

Licha ya kuwa na majukumu ya kufanya biashara, mrembo huyo siyo kichwa maji baada ya kufaulu masomo yake aliyokuwa akibobea kwenye masuala ya usimamizi wa biashara na ujasiriamali.

Umejifunza nini kutoka kwa Binti Mbaga? Toa maoni yako kupitia mitandao yetu ya kijamii.

Enable Notifications OK No thanks