Luca: Filamu maalum kwa marafiki wanaotengenishwa na usaliti

July 2, 2021 6:36 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inamhusu kijana anayekataa kufungamana na maisha yake ya kawaida na kutafuta ndoto yake.
  • Katika safari yake, anakutana na mtu ambaye daima, atabaki na deni lake.
  • Luca anakutana na Alberto aliyetoa kafara ya ndoto  yake kuona ndoto ya rafiki yake inatimia.

Unaweza kusikiliza simulizi ya filamu hiyo hapa

                                               


Dar es Salaam. Kati ya binadamu wote, yupo mmoja ambaye yupo huru kusema siri zake, kuvua uhusika wake wa maigizo na kubaki na uhalisia wake akiwa mbele yako. Ni rafiki yako.

Umewahi kujiuliza umbali unaweza kwenda kutetea mapenzi yako kwake hasa pale inapobidi kutoa kafara ya furaha yako? 

Inaanza na kiumbe samaki mdogo ambaye anaishi na wazazi wake baharini. Muda wa mchana, Luca huchunga mifugo ya familia na jua linapozama, anarudisha mifugo zizini. 

Hayo ni maisha yake ya kila siku na kwa muonekano wa baba na mama yake, hayana dalili za kubadilika.

Sijui simulizi ambazo Luca amekua akiambiwa juu ya binadamu lakini anaogopa kila kitu kinachohusiana na binadamu siyo kuwaona tu, hata vitu wanavyomiliki. 

Hofu yake ipo mbali zaidi kiasi cha kuogopa kusogea ufukweni ambako binadamu huendesha shughuli zao za kila siku ikiwemo uvuvi.

Yote hayo yanafikia kikomo siku ambayo Luca anakutana na Alberto wakati akiendelea na shughuli zake za uchungaji. 

Tofauti la Luca, Alberto makazi yake ni nchi kavu ambapo huchukua mfumo wa binadamu na ana uwezo wa kuwa samaki kama alivyo Luca.

Siku moja, Alberto anamwalika rafiki yake mpya nchi kavu. Siku hiyo inabaki siku ya kukumbukwa daima kwa Samaki Luca.

Ni siku ambayo inabadilisha kila kitu kuhusu Luca.

Akiwa duniani, Alberto anabaki tegemeo pekee la Luca. Picha| wdwmagic.

Siku ambayo Luca anatembelea nchi kavu, anagundua kuwa naye ana uwezo kama alionao Alberto. Anagundua kuwa pale anapokuwa nje ya maji na yeye anabadilika kuwa binadamu.

Anagundua kuwa na yeye ana nywele za singasinga, vidole, miguu na ngozi nyororo. 

Magamba, matezi na hata mkia wake haupo tena. Kwa Luca, ni siku ambayo kipofu ameona mwezi.

Alberto anamfunza rafiki yake kutembea, jinsi ya kuwasiliana kama binadamu na kumweleza ndoto yake ya kumiliki pikipiki ambayo ndani ya sekunde inageuka kuwa ndoto ya Luca pia.

Licha ya kuwa Alberto anamlisha Luca matango pori kuhusu baadhi ya vitu kama mwezi ni samaki mkubwa anayelinda samaki wengine wadogo ambao ni nyota, uwezo wa pikipiki kupaa kiasi cha kukutana na samaki hao wa angani na matango pori mengine, bado wawili hao ni marafiki kama alivyo pwagu na pwaguzi.

Kumbuka, Luca siyo kwamba anayafanya hayo akiwa na ruhusa ya wazazi wake na pale wanapogundua kuwa amekuwa akitoroka na kwenda nchi kavu, wanakasirika na kuamuru Luca akaishi na mjomba wake ambaye huishi katika kina kirefu cha bahari. 

Huko, hakuna mwanga, jua wala binadamu wa kumdhuru.

Hata hivyo, inamlazimu mjomba aondoke mikono mitupu kwani Luca anatoroka na kwenda kwa rafiki yake Alberto.

Wawili hao wanashauriana kuchangamana na binadamu wengine ambako wanakutana na Julia ambaye anawatambulisha kwa baba yake.

                     

Baba Julia sio mtu wa mchezo mchezo, ni mvuvi ambaye anategemea samaki kujipatia kipato lakini haumwambii lolote la kumhusu mwanae Julia. 

Binti Julia anamshawishi baba yake kumruhusu ashiriki mashindano makubwa kisiwani hapo ili rafiki zake wapate fedha ya kuwatimizia ndoto zao. Kununua pikipiki.

Mashindano hayo yanahusisha kuogelea, kula na mbio za baiskeli. Julia na rafiki zake wanajifua vilivyo ili washinde mashindano hayo lakini haichukui muda watatu hao wanasambaratika.

Julia anaugundua ukweli ambao unasambaratisha urafiki wao baada ya Alberto kuamua kufunguka juu ya hali yao. Siri ya kua wawili hao ni samaki inafichuka na haiachi urafiki wa watatu hao katika mikono salama kwani Luca, anamsaliti Alberto kwa kumbeza kuwa yeye ni samaki na mnyama kana kwamba yeye ni binadamu halisi.

Alberto ambaye usaliti huo unamwacha mdomo wazi, anarudi kule alikokuwa akiishi zamani kabla ya Luca kuingia maishani mwake.

Luca ambaye sasa hataki pikipiki tena, anataka kusoma kama Julia. Luca ambaye sasa hata matango pori ya Alberto hayamwingii tena, ana kiu ya kuelimika.

Nini kitatokea? Marafiki hao watatatua changamoto zao na kuendelea kuzikimbizia ndoto zao?

Hali ya Julia na baba yake baada ya kuujua ukweli itakuwaje?

Jibu maswali yako kwa kuitazama filamu hii ya katuni ambayo itamwacha mtoto wako na mafunzo makubwa na hata mtu mzima itamfundisha jinsi ya kutatua changamoto zinazomkabili.

Enable Notifications OK No thanks