Rasmi wageni kuanza kulipa USD44, bima ya safari Tanzania
- Bima inahusisha dharura za kitabibu, kupotea kwa mizigo, uokoaji wa dharura na pamoja na mgeni kurejeshwa nchini kwake.
- Raia wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameondolewa kwenye hitaji hilo.
Dar es Salaam. Rasmi leo, Oktoba 1, 2026, Serikali imeanza kutekeleza mfumo wa bima ya lazima ya safari unaowataka wageni kutoka nje ya nchi wanaoingia Tanzania Bara kulipia Dola za Marekani 44, sawa na takriban Sh116,000.
Hatua hiyo inatekelezwa chini ya kanuni za bima ya safari kwa wasafiri wa kimataifa wanaoingia Tanzania, 2026, zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 256 la Septemba 4, 2026, chini ya kifungu cha 134A cha Sheria ya Bima, Sura ya 394.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha, bima hiyo inawalenga wageni wote wanaoingia Tanzania Bara kupitia mipaka ya nchi kavu, bandari na viwanja vya ndege na itadumu kwa muda wa hadi siku 92.
Inamlinda mgeni dhidi ya nini?
Shirika la Taifa la Bima (NIC), limesema bima hiyo inatoa ulinzi dhidi ya matukio mbalimbali yanayoweza kumpata mgeni akiwa nchini, ikiwamo dharura za kitabibu, kupotea kwa mizigo, uokoaji wa dharura wa kitabibu na kurejeshwa nchini kwake, kwa kuzingatia masharti ya sera.Â
NIC inaeleza kuwa bima hiyo ambayo hudumu wa siku zisizozidi 92 huanza kutumika mara tu baada ya malipo na mgeni hupewa cheti cha kidijitali au cha karatasi ambayo inaweza kuhitajika wakati wa kuwasili kwa ajili ya uthibitisho.
Mgeni anayehitaji bima anaweza kununua kupitia mfumo maalumu wa NIC kwa Tanzania Bara, na Shirika la Bima Zanzibar huku taarifa za utaratibu wa ununuzi, malipo na uthibitishaji zikitolewa na watoa huduma husika.
Kwa mujibu wa Serikali, mgeni ambaye sehemu yake ya kwanza ya kuingia ni Tanzania Bara na kupata bima kupitia NIC anaweza baadaye kwenda Zanzibar bila kununua bima nyingine ya lazima.
Hata hivyo, endapo dharura itatokea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huduma itatolewa na mtoa bima ambaye mgeni alinunua kwake, kwa kuzingatia masharti ya sera.
EAC, SADC waondolewaÂ
Licha ya bima hiyo kuwa ni ya lazima kwa wageni wote wanaoingia nchini, Serikali imesema wageni ambao ni wakazi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameondolewa kwenye hitaji hilo.
Hii inamaanisha kuwa wageni raia wa Burundi, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda, Angola, Botswana, Comoros, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe hawatahitajika kukata bima hiyo wanapoingia Tanzania.Â
Wizara ya Fedha imewataka wasafiri wa kimataifa kufanya maandalizi ya bima kabla ya kusafiri ili kurahisisha taratibu za kuingia nchini na kuepuka usumbufu au ucheleweshaji wanapowasili.Â
Hata hivyo, NIC inaeleza kuwa malipo yanaweza pia kufanyika wanapowasili katika vituo vya kuingilia nchini.
Tanzania si nchi ya kwanza kuweka utaratibu wa bima ya lazima kwa wasafiri wanaoingia nchini, hata nchi jirani kama vile Kenya pia imeweka bima ya afya ya safari ya lazima kwa wageni wasio raia ikilenga kuwakinga dhidi ya gharama za matibabu na dharura wakati wa safari.Â