Zaidi ya mawasiliano: Vodacom inavyochochea mustakabali wa kidijitali Tanzania
- Vodacom Tanzania iliibuka mshindi wa kwanza katika sekta ya mawasiliano na kushinda tuzo kadhaa za ubora katika maonesho ya Sabasaba 2026.
- Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Rais wa Msumbiji walitembelea banda la Vodacom kujionea ubunifu wa kidijitali.
- Vodacom yasisitiza mageuzi ya kidijitali na uwezeshaji jamii kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi ya Watanzania.
Dar es Salaam. Mabadiliko ya kidijitali nchini Tanzania yanaendelea kushika kasi, yakichochewa zaidi na maendeleo ya teknolojia yanayowaunganisha watu, biashara na huduma za umma.
Kadiri matumizi ya teknolojia yanavyoendelea kubadili uchumi wa nchi, nafasi ya kampuni za mawasiliano pia inazidi kupanuka kutoka katika kutoa huduma za mawasiliano pekee hadi kuwezesha ubunifu, ujumuishaji wa kifedha na maendeleo endelevu.
Vodacom Tanzania PLC ilidhihirisha mabadiliko hayo kupitia huduma na suluhisho mbalimbali za kiteknolojia zinazolenga kuboresha maisha ya kila siku ya Watanzania katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) mwaka huu.
Kuanzia simu janja za gharama nafuu, huduma bora za mawasiliano, huduma za kifedha za M-Pesa hadi suluhisho za biashara, ushiriki wa kampuni hiyo ulidhihirisha dhamira yake ya kuendelea kuiwezesha Tanzania kuelekea kwenye jamii iliyounganishwa zaidi kidijitali na inayojumuisha kila mwananchi.
Mchango wa Vodacom katika maonesho ya Sabasaba mwaka 2026 ulitambuliwa kupitia tuzo mbalimbali zilizothibitisha nafasi yake kama kinara katika sekta ya mawasiliano pamoja na mchango wake katika maendeleo ya kidijitali na kiuchumi nchini. Vodacom Tanzania PLC iliibuka mshindi wa kwanza katika Sekta ya Mawasiliano, huku pia ikishika nafasi ya tatu katika kipengele cha banda bora miongoni mwa waoneshaji wote.
Aidha, kampuni hiyo ilitunukiwa tuzo Maalum ya Jubilei ya Dhahabu kwa kushika nafasi ya tatu miongoni mwa washiriki waliodumu kwa muda mrefu katika maonesho hayo, ikiwa ni sehemu ya kutambua taasisi zilizochangia safari ya miaka 50 ya Sabasaba.
Vodacom pia ilitunukiwa tuzo ya nafasi ya pili ya udhamini kutokana na mchango wake kupitia huduma za tiketi za kidijitali (e-ticketing) pamoja na mchango wa nafasi za maonesho.

Mbali na tuzo hizo, Vodacom pia ilitambuliwa kama mshindi wa nafasi ya tatu katika kundi la washindi wa jumla wa maonesho hayo pamoja na kushika nafasi ya pili katika kipengele cha udhamini, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa Vodacom Tanzania kama mshirika muhimu wa Maonesho hayo.
Katika maadhimisho hayo, banda la Vodacom lilipata heshima ya kutembelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo, waliopata fursa ya kujionea huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania PLC, Brigita Shirima, aliyekuwa akizungumza wakati wa maonesho hayo alisema uwekezaji endelevu wa kampuni katika ubunifu unaongozwa na lengo moja kuu la kufanya teknolojia ipatikane kwa urahisi zaidi na kuwa na manufaa kwa kila Mtanzania.
“Wateja wa leo wanahitaji zaidi ya huduma za mawasiliano. Wanahitaji suluhisho zinazorahisisha maisha yao ya kila siku, zinazosaidia biashara zao kukua na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika dunia inayozidi kuunganishwa huduma za kidijitali.
Vodacom tunaendelea kuwekeza katika simu janja za gharama nafuu, huduma bora za mtandao na suluhisho bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji hayo yanayoendelea kubadilika huku tukiwajumuisha Watanzania wengi zaidi katika uchumi wa kidijitali,” alisema.
Maono haya yanazidi kudhihirika kupitia mifumo mipana ya huduma za Vodacom zinazoendelea kukua. Kupitia M-Pesa, kampuni inawezesha miamala salama ya kifedha, upatikanaji wa simu janja, kuboresha huduma za mawasiliano katika biashara na kuchochea ushiriki wa wananchi katika maisha ya kidijitali, hivyo kuendelea kudhihirisha nafasi yake ya kuwa mshirika muhimu katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini.
Mbali na teknolojia, Vodacom inaamini kuwa maendeleo yenye tija yanategemea kuwawezesha watu kupata maarifa na ujuzi wa kutumia fursa zinazoletwa na teknolojia mpya.
Dhamira hiyo inaendelezwa kupitia ‘Vodacom Foundation’, ambayo inaendelea kuwekeza katika programu zinazokuza ujasiriamali, elimu ya fedha na ushiriki jumuishi katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation Sandra Oswald, alisema teknolojia huleta matokeo ya kudumu pale ambapo watu wanakuwa na uwezo na ujasiri wa kuitumia katika kuboresha maisha yao.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma wakati Tanzania inaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia mpya. Kupitia programu zetu za uwezeshaji, tunawasaidia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata ujuzi wa ujasiriamali, uongozi na usimamizi wa fedha ili waweze kujenga biashara imara na kuboresha maisha yao,” alisema.
Miongoni mwa programu zilizooneshwa katika maadhimisho ya Sabasaba ni Think Equal, Lead Smart(TELS), inayotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi ya CEO Roundtable pamoja na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC). Programu hiyo tayari imewafikia zaidi ya washiriki 800 wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, uongozi na matumizi ya huduma za kifedha ikiwemo M-Pesa na M-Koba.
Vodacom Foundation pia iliwatunuku washiriki wawili waliofanya vizuri zaidi kwa kuwapatia vocha zenye thamani ya shilingi 500,000 kila mmoja kama mtaji wa biashara.
Mpango huo unaongeza nguvu katika ajenda pana ya Vodacom Tanzania Foundation ya uwezeshaji wa jamii, ambayo tayari imewafikia zaidi ya wanawake 500,000 nchini kupitia programu mbalimbali zinazopanua ujumuishaji wa kifedha, kuimarisha ujasiriamali na kuunda fursa za maendeleo endelevu ya kiuchumi.
Wakati Tanzania ikiendelea na safari ya mageuzi ya Uchumi unaotegemea zaidi teknolojia na mifumo ya kidijitali, Vodacom inaendelea kubaki na dira na dhamira yake kupanua upatikanaji wa huduma, kuchochea ubunifu na kuunda fursa zinazoboresha maisha ya wananchi. Ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho ya Sabasaba haukuwa maonesho pekee, bali ulikuwa uthibitisho wa dhamira yake ya muda mrefu ya kuijenga Tanzania ya kidijitali kupitia teknolojia, ujumuishaji na maendeleo endelevu.