Tanzania yaanika afua 10 kudhibiti Ebola
- Ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege.
- Wizara ya Afya yathibitisha hakuna mgonjwa wa Ebola Tanzania.
Arusha. Serikali ya Tanzania imetahadharisha umma juu ya uwepo wa ugonjwa wa Ebola ikitangaza afua 10 muhimu zitakazotumika kudhibiti ugonjwa huo ulioripotiwa katika nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Tanzania inatangaza afua hizo ikiwa ni takribani siku nne tangu nchi hizo zinazopakana na Tanzania ziripoti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na kutangazwa rasmi kuwa dharula ya kiafya ya kimataifa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kufuatia darura hiyo, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imesema
imetangaza afua hizo kutokana na ukaribu uliopo kati ya Tanzania na nchi zilizoripoti ugonjwa huo huku kukiwa hakuna kisa cha ugonjwa huo kilichoripotiwa hadi sasa.
“Kutokana na ukaribu na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi na kijamii uliopo kati yetu na nchi zenye mlipuko huo, Serikali imeendela kuimarisha utayari no kuzuia ugonjwa huu kupitia afua mbalimbali,” imesema Taarifa ya Mganga Mkuu wa Serikali Grace Maghembe,iliyotolewa jana Mei 18, 2026.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya afua hizo ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege ili kubaini mapema viashiria vya ugonjwa.
Nyingine ni uimarisha utayari wa vituo vya huduma na kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na tiba muhimu ili kutoa huduma kwa wagonjwa endapo ugonjwa utaingia nchini pamoja na kupeleka timu za wataalam wa kitaifa katika mikoa yenye hatari kubwa ili kuimarisha hatua za kinga, ufuatiliaji na utayari wa kukabiliana ugonjwa huo.
Mbali na hizo Seikalli pia itaendelea kutoa elimu ya afya kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo TV, radio na mitandao ya kijamii, kuimarisha ushirikiano na nchi jirani kupitia uratibu wa afya mipakani na ubadilishanaji wa taarifa za tahadhari na kutuma timu ya ngazi ya taifa katika mikoa iliyo katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo.
Aidha, woizara hiyo imesema itatoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na kuamsha timu za wataalam pamoja na kubainisha vituo maalum vya kuhudumia wagonjwa endapo kutatokea maambukizi
Kuendelea na vikao vya uratibu wa kitaifa kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na wadau mbalimbali ili kuimarisha hatua za kuzuia Ebola na kusambaza miongozo na vitendea kazi kwa mikoa na kuwakumbusha kuviweka katika hali ya kutumika endapo vitahitajika.
“Kuhuisha mwongozo wa wasafiri Travel Advisory) ili kutumika kuanzia tarehe 19 Mei 2026, kutekeleza afua za kinga kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa,” imeongeza taarifa hiyo ikirejea hatua ya 10 ya kudhibiti Ebola.
Pamoja na hayo, wizara hiyo imewataka watanzania kuchukua tahadhari zote za kiafya zinazohitajika ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka kugusa majimaji ya mtu Mwenye dalili za Ebola.
Ikiwa jamii itamshuku yoyote kuwa na dalili za ugonjwa huo Wizara ya Afya imewataka kutoa taarifa kupitia simu bila malipo kwa namba 199.
Latest