Sekta ya fedha inavyoimarika Tanzania

January 23, 2026 3:01 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ukuaji huo umejidhihirisha kupitia ongezeko la idadi ya benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, mawakala wa benki pamoja na rasilimali za kibenki.

Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni, sekta ya fedha nchini Tanzania imeendelea kuonesha mwelekeo chanya wa ukuaji, ikichochewa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, upanuzi wa taasisi za kifedha na kuimarika kwa imani ya wananchi katika mifumo rasmi ya fedha. 

Ukuaji huo umejidhihirisha kupitia ongezeko la idadi ya benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, mawakala wa benki pamoja na rasilimali za kibenki, hali inayoashiria kuimarika kwa mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula aliyekuwa akizungumza Januari 21, 2025 katika uzinduzi maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya huduma ya fedha, amesema hadi kufikia Septemba 2025, Tanzania ilikuwa na jumla ya benki za kibiashara 35, benki za kijamii mbili, benki za maendeleo mbili pamoja na benki tatu za huduma ndogo za fedha. 

Aidha, taasisi 2,811 za huduma ndogo za fedha pamoja na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha 70,913 zilisajiliwa, huku taasisi mbili za ubadilishanaji wa fedha zikiongeza idadi ya watoa huduma rasmi nchini.

Aidha, Luswetula ameeleza kuwa upanuzi huo umeenda sambamba na ongezeko kubwa la mawakala wa benki nchini. Ambapo Idadi ya mawakala wa benki imeongezeka kutoka 106,176 hadi kufikia 145,430, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hadi ngazi ya jamii.

Mbali na ongezeko la taasisi, rasilimali za kibenki nazo zimeendelea kuimarika na kufikia Sh71.8 trilioni Septemba 2025, ikilinganishwa na Sh62.2 trilioni zilizorekodiwa Septemba 2024.

Aidha, katika kipindi kama hicho, amana za benki zimeongezeka hadi Sh50.2 trilioni kutoka Sh42.7 trilioni mwaka uliotangulia, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya kuongezeka kwa imani ya wananchi katika sekta ya fedha.

Katika maelezo yake, Luswetula pia amebainisha kuwa mikopo kwa sekta binafsi imekua kwa kasi kubwa. Ikiongezeka na kufikia Sh42 trilioni mwaka 2025 kutoka Sh35 trilioni mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 24.

Hata hivyo, pamoja na ongezeko la mikopo, amebainisha kiwango cha mikopo chechefu bado kiko katika hali inayodhibitiwa. 

“Mikopo chechefu imeongezeka kwa asilimia 2.78, kiwango ambacho bado kipo ndani ya ukomo wa kisheria wa asilimia tano,” ameeleza Luswetula.

Soko la hisa laongezeka 

Kwa upande wa sekta ndogo ya mitaji na dhamana, Luswetula amesema Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kukua ambapo kuonesha ukuaji idadi ya kampuni zilizosajiliwa katika soko hilo imefikia 28 huku mifuko ya uwezeshaji ikifikia 21.

Aidha, ameainisha kuwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji ilifikia Sh63.7 trilioni katika kipindi kilichoishia Desemba 2025.

“Jumla ya mauzo ya hisa na hati fungani katika soko la hisa la Dar es Salaam yamefikia Sh6.87 trilioni vilevile thamani ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja ilifikia Sh4.35 trilioni katika kipindi hicho,” ameongeza Luswetula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks