Mambo ya kuzingatia kabla ya kuwekeza soko la hisa 

January 22, 2026 4:35 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kuwa na elimu ya uwekezaji ikiwemo kuelewa faida na hasara za uwekezaji.
  • Kuna wakati utaingiza zaidi na kuna wakati utapoteza.

Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa, inayoshuhudia kuongezeka kwa gharama za maisha na kuzorota kwa uhakika wa ajira, uwekezaji umekuwa ni sehemu ya suluhu kwa watu wanaotaka kupata uhuru wa kifedha. 

Miongoni mwa maeneo ya uwekezaji ni soko la hisa ambalo huwapa fursa watu kuwekeza fedha zao kwa kununua hisa na kuwa sehemu ya umiliki wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko husika. 

Kwa mujibu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hisa ni uwakilishi wa umiliki wa kampuni pamoja na haki ya kudai mali na mapato ya kampuni husika.

Aidha, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) inaeleza kuwa hisa na dhamana nyingine ni mali halali sawa na mali nyingine kama nyumba au magari. 

Hii ina maana kuwa mwekezaji ana haki ya kumiliki, kuuza au kunufaika na mali hiyo kulingana na mabadiliko ya soko. Kampuni inapopata faida mwekezaji wa hisa huwa na fursa ya kupata gawio ikiwa ni matunda ya uwekezaji wake na iwapo itapata hasara naye atakuwa amepata hasara. 

Thamani ya hisa zilizoorodheshwa katika soko la hisa hupanda na kushuka kutokana na mwenendo wa soko. Iwapo mwekezaji atauza hisa zake zikiwa na thamani ya juu kuliko bei aliyonunulia basi ataingiza faida nyingi kibindoni na vivyo hivyo iwapo zitapoteza thamani atakuwa ameangukia pua. 

Kwa umuhimu huo Nukta Habari tunakuletea mambo ya kuzingatia kabla ya kuwekeza soko la hisa.

Jengo la Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) lililopo jijini Dar es Salaam eneo la Morocco. Hivi karibuni kumekuwa na hamasa kubwa ya watu kuwekeza katika soko la hisa kupanua wigo wa uwekezaji. Picha|Goodluck Gustavo/Nukta Habari.

Wekeza kwenye elimu ya uwekezaji

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya fedha na uwekezaji jijini Dar es Salaam Miriamu Bukuku ni lazima mwekezaji awe na elimu ya uwekezaji kwa kuwa ni msingi wa safari yake kiuwekezaji. 

“Huwezi kuwekeza kwa usalama kama hujaelewa mantiki ya hisa, faida zake na hatari zake,” anasema Bukuku.

Bukuku anaeleza kuwa ni muhimu kwa mwekezaji kufanya uchambuzi wa kina wa kampuni kabla ya kununua hisa akizingatia taarifa za kifedha, mwenendo wa biashara na hali ya uchumi wa taifa. Uelewa huu humsaidia mwekezaji kubaini kama kampuni husika inafaa kuwekeza au la.

Kuwa na mkakati wa uwekezaji 

Kuwekeza bila mkakati ni sawa na kuendesha gari bila ramani, anasema Bukuku huku akibainisha kuwa uwekezaji wa kiholela au wakufuata maoni ya wengine bila kufahamu malengo ni hatari. 

Anabainisha kuwa mkakati mzuri wa uwekezaji unapaswa kujumuisha malengo yaliyo wazi kama kuandaa fedha za kununua gari baada ya muda fulani au kujenga mtaji wa biashara.

Aidha, mwekezaji anatakiwa kupanga ratiba ya uwekezaji kulingana na kipato chake, iwe kwa siku, wiki au mwezi na kuwe na mfumo wa kufuatilia taarifa za soko na utendaji wa kampuni mara kwa mara.

Kuwa na mfuko wa dharura kabla ya uwekezaji

Kabla ya kuanza kuwekeza ni muhimu kuwa na mfuko wa dharura unaoweza kugharamia matumizi ya miezi mitatu hadi sita.

 Mfuko huu humlinda mwekezaji dhidi ya kulazimika kuuza hisa kwa hasara au kukopa fedha pale anapokumbwa na dharura.

CMSA inaeleza kuwa bei za hisa hubadilika mara kwa mara zinaweza kupanda au kushuka hali inayomlazimu mwekezaji kuwa tayari kisaikolojia na kifedha.

Wataalamu wa masuala ya fedha wanashauri kabla ya kununua hisa ni muhimu kuwa na elimu ya kutosha kuhusu soko la hisa. Picha|Goodluck Gustavo/Nukta Habari.

Anza kuwekeza kwa kipato kidogo

Mara baada ya maandalizi yote, Bukuku anasema mwekezaji anaweza kuanza kuwekeza kidogo kidogo na si lazima awe na kipato kikubwa. 

“Mtu unaweza kuanza kuwekeza kwa kutenga asilimia 10 (moja ya 10) ya kipato chake,” anaeleza. 

Pamoja na kasi hiyo ya kuanza kuwekeza anasisitiza kuwa ni busara kwa mwekezaji kutafuta ushauri wa wataalamu wa masuala ya fedha ili kusaidia kuchagua kampuni zenye mwelekeo mzuri wa kibiashara kabla ya kuwekeza.

Fuatilia gawio la faida (Dividend)

Kwa mujibu wa tovuti ya Investopedia, wawekezaji wasiotaka kufuatilia soko kila siku wanaweza kuzingatia hisa zinazotoa gawio baada ya kupata faida. Gawio hili, kwa mujibu wa tovuti hiyo ya elimu ya fedha na uwekezaji ya Marekani, hufanya kazi kama riba ya akaunti ya akiba.

Gawio hutolewa iwapo kampuni imeamua sehemu ya faida husika itolewe kwa wawekezaji kama rejesho la uwekezaji wao na kiasi kingine hubakizwa ajili ya kuimarisha mtaji na uendelezaji wa kampuni. 

Pia, kabla ya kuwekeza, mwekezaji anaweza kutumia uchambuzi wa kimsingi au wa kiufundi au zote kwa pamoja ili kupata picha halisi ya utendaji wa kampuni na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji.

Kuwa tayari kupata, kupoteza

Kama ulivyo uwekezaji mwingine wa biashara, mwekezaji wa hisa anatakiwa moyo wake uwe tayari kupata na kupotea. Kuna nyakati uwekezaji wake utakuwa hata zaidi ya mara tatu ndani ya muda mfupi na kuna wakati thamani ya uwekezaji wake unaweza kuporomoka hata mara sita.

Wenye roho nyepesi na waoga kuwekeza kwenye biashara zenye vihatarishi wanapaswa kupata ushauri juu ya kampuni zenye mwenendo chanya wa uwekezaji au watafute fursa nyingine za kuwekeza. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks