Sh1.2 trilioni kusambaza umeme vitongoji 9,009 Tanzania

January 17, 2026 2:37 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Upatikanaji wa umeme katika vitongoji hivyo utachochea zaidi maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Dar es Salaam. Serikali imetia saini mikataba 30 yenye thamani ya Sh1.2 trilioni kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchini, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi hususan katika maeneo ya vijijini.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi aliyekuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo leo Januari 17, 2026 amesema kuunganishwa kwa umeme katika vitongoji hivyo kutachochea maendeleo nchini.

“Miradi hii itaweza kusimamia maendeleo kwa kasi katika vijiji vyetu kwenye Taifa letu,” amesema Ndejembi.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutafanya jumla ya vitongoji 50,447 kati ya 64,359 vilivyopo nchini kufikiwa na huduma ya umeme suala litakalochochea zaidi maendeleo ya shughuli za kijamii na kiuchumi.

Ndejembi ameeleza kuwa mradi huo utafikisha umeme kwa Watanzania 260,000 katika mikoa 19 ukitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu, akisisitiza kuwa utekelezaji wake utapiga hatua kubwa katika kuongeza upatikanaji wa umeme.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutafanya jumla ya vitongoji 50,447 kati ya 64,359 vilivyopo nchini kufikiwa na huduma ya umeme. Picha | Majira Times.

“Mkoa wa Katavi, mkoa wa Kilimanjaro, na Kigoma ipo katika mikoa ambayo baada ya kukamilika kwa mradi huu umeme utakuwa umefika kwa asilimia 100” amesisitiza Ndejembi.

Mikoa mingine itakayotekelezwa miradi hiyo ni pamoja na Tanga, Tabora, Singida, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa, Pwani, Njombe, Mwanza, Mtwara, Morogoro, Mbeya, Mara, Manyara na Lindi.

Kwa mujibu wa Ndejembi, hadi sasa upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini umefikia asilimia 70, huku vijiji 12,318 vikiwa tayari vimeunganishwa na huduma hiyo, na kiwango cha uunganishaji kwa wateja kikiwa asilimia 37.

Wakandarasi waonywa

Ndejembi amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kufanya kazi kwa weredi ili kufikisha umeme kwa haraka kwa Watanzania.

“Watanzania wanataka kuona umeme unawaka, na nyinyi mmeaminika kupewa kazi hizi twendeni tukazifanye ili tuongeze thamani lakini na nyinyi tuweze kuona uwezo wenu ili muweze kupata kazi nyingine,” amesisitiza Ndejembi.

Aidha, Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuweka jitihada za kimkakati kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa wote unafikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks