Sababu Kagera kununua mafuta kwa bei ya juu

January 9, 2026 11:48 am · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na umbali kutoka Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

Arusha na Dar es Salaam. Kila mwanzoni mwa mwezi wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) inapotangaza bei mpya za mafuta ama kwa kupandisha au kushusha wakazi wa mkoa wa Kagera wao mara nyingi hujikuta wakitoboa zaidi mifuko yao kununua bidhaa hiyo.

Hali hiyo hutokana na ukweli kwamba wakazi wa mkoa huo hususan maeneo ya Kyerwa, Muleba, Ngara na Katoro ndio wanaonunua mafuta kwa bei ya juu zaidi ukilinganisha na maeneo mengine nchini na kuwaongezea maumivu ya kiuchumi.

Uchambuzi wa takwimu za bei ya mafuta uliofanywa na Nukta Habari kwa miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2023 umebaini kuwa wakazi hao hawajawahi kununua petroli chini ya Sh2,900 na dizeli chini ya Sh2,782. Wakazi hao katika kipindi hicho cha miaka mitatu wamekuwa wakinunua petroli kwa wastani wa bei ya Sh3,124 kwa lita na Sh3,094 kwa dizeli.

Bei wanayonunua wakazi hao wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ni ya juu zaidi kwa wastani wa asilimia nane ya bei ya petroli iliyotumika jijini Dar es Salaam katika kipindi hicho cha miaka mitatu.

Hata katika mwaka mpya 2026 bado wakazi hao wameendelea kununua mafuta kwa bei ya juu ikipeleka maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto na huduma nyingine zinazotegemea mafuta hayo yakiwemo malori na bodaboda.

Mathalan, katika taarifa ya bei kikomo iliyotangazwa Januari 7, 2026 na Ewura wakazi wa Kyerwa (Buberwa) wananunua petroli kwa Sh3,050 na dizeli kwa Sh2,998, Biharamulo (Petroli – Sh3,003, dizeli – Sh2,950) na Karagwe wao wananunua Petroli kwa Sh3,045 na dizeli ni Sh2,993.

Pamoja na kupaa kwa bei katika mikoa hiyo wakazi wa Dar es Salaam wananunua mafuta hayo kwa bei ya chini zaidi ambapo kupitia Bandari ya Dar es Salaam lita moja ya petroli imeuzwa Sh2,778, na dizeli kwa Sh2,726

Kupitia Bandari ya Tanga petroli inauzwa kwa Sh2,839 na dizeli Sh2,787 huku mafuta yanayopitia Bandari ya Mtwara yakiuzwa Sh2,870 kwa petroli na Sh2,818 dizeli.

Tofauti na mikoa mingine yenye ahueni ya bei, mikoa ya kanda ya ziwa hasa Kagera ipo mbali na bandari ambazo hupokea shehena ya mafuta kutoka ng’ambo hivyo bei zake za rejareja huathiriwa na gharama za usafiri. Wafanyabiashara wa mafuta wa fursa ya kuchukua nishati hiyo ama kupitia Dar es Saaam au Tanga.

Adhabu ya kijiografia
Ripoti ya Utendaji wa Kiuchumi wa Kanda inayotolewa na Benki Kuu Tanzania (BoT) inabainisha kuwa Kagera na mikoa mingine ya kanda ya ziwa huathirika na bei ya juu ya mafuta kutokana na sababu za kijografia.


“Hali hii imejitokeza kwa karibu kila mwaka, jambo linaloifanya kanda hiyo kuwa mfano halisi wa athari za kijiografia na miundombinu katika upangaji wa bei za mafuta nchini Tanzania,” imesema BoT katika ripoti hiyo ya robo ya mwaka iliyoishia Juni 2025.

Ramani inayoonyesha umbali kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Kyerwa mkoani Kagera.Picha/Google Map.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi na fedha Paulo Chengula ameiambia Nukta Habari kuwa ongezeko la bei kwenye bidhaa za mafuta huathiri moja kwa moja gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida na watumiaji wa vitu vinavyotumia mafuta kama magari na usafiri binafsi.

“Mafuta yanapopanda, gharama za usafiri nazo zinaongezeka, mtu aliyekuwa analipa Sh500 anaweza kujikuta analipa Sh700,” anasema Chengula. 

Kwa mujibu wa Chengula, mzigo mkubwa wa ongezeko la bei hubebwa na mlaji wa mwisho na sio mfanyabiashara ambaye yeye haiwezi kumuathiri kwa sababu huhamisha bei kwa mtumiaji wa mwisho.


Uchambuzi huu umefanywa na Lucy Samson na Fatuma Hussein

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks