Ulinzi mkali Dar es Salaam wadhibiti maandamano Desemba 9

December 9, 2025 8:26 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Jeshi la polisi laeleza kuwa hadi jioni ya Desemba 9, 2025 hali amani ni shwari.
  • Baadhi watembea kwa miguu jijini Dar es Salaam kwa kukosa usafiri.

Dar es Salaam. Hali ya usalama nchini imeendelea kuwa shwari baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti maandamano ya vijana yaliyokuwa yamepangwa kufanyika bila kikomo kuanzia Desemba 9, siku ya maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara.

Kwa zaidi ya wiki tatu kumekuwa na uhamasishaji mtandaoni wa maandamano ya amani kupinga mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kushinikiza uwajibikaji baada ya vurugu zilizoibuka wakati wa maandamano yaliyofanyika Oktoba 29 na siku zilizofuatia.

Vurugu hizo ziligharimu maisha ya watu na kuharibu mali za umma na watu binafsi vikiwemo vituo vya mafuta, magari, vituo vya mabasi ya mwendokasi, maduka na ofisi za Serikali. Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume ya kuchunguza madhila hayo makubwa kuikumba Tanzania ndani ya miongo ya hivi karibuni.

Serikali ilipiga marufuku maandamano ya Desemba 9 likieleza kuwa ni kinyume na sheria kwa kuwa “wanayoitisha hawafahamiki, ujumbe wao haufahamiki na hawajaomba kibali kutoka Jeshi la Polisi.

Leo tangu asubuhi ulinzi iliimarishwa katika maeneo mengi nchini ikiwemo jijini Dar es Salaam ambapo polisi na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wametanda barabarani kudhibiti maandamano hayo.

Jijini Dar es Salaam, barabara kuu, maeneo ya jiji kati yalikuwa kimya na tulivu huku kukiwa na watu wachache sana wanaotembea. Maduka yote maeneo ya Kariakoo, Mnazi Mmoja na Posta yamefungwa huku polisi na wanajeshi wakidhibiti njia zote za kuingia na kutoka maeneo hayo.

Maumivu usafiri wa umma ukiadimika

Usafiri wa umma umeadimika huku bodaboda chache zikionekana zaidi maeneo ya mitaani kuliko mjini. Watu waliokuwa wameenda kazini leo wamejikuta wakitembea sehemu kubwa kutokana na kukosa usafiri.

Mkazi wa Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameiambia Nukta Habari kuwa amelazimika kutembea kutoka Upanga anapofanya kazi ya usafi hadi nyumbani kwake kwa kuwa hakuna daladala, bajaji wala bodaboda zinazofanya kazi.

“Hata bodaboda unayemjua ukimpigia simu aje akufuate, hataki anaogopa kukamatwa na polisi,” amesema.

Watoa huduma wa daladala wanaeleza kuwa sehemu kubwa wamepaki magari kutokana na tahadhari za kiusalama.

Hemed Juma, Dereva wa daladala jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa alitamani kuwasha gari kwa ajili ya kutoa huduma ila akikumbuka kilichotokea wakati wa maandamano baada ya uchaguzi aliona bora wapaki kujinusuru uhai na mali.

“Nilijiwekea vijisenti (fedha) kidogo kwa ajili ya kula siku mbili au tatu lakini hali ikiendelea hivi watoto watalala na njaa,” amesema.

Ukaguzi wa kutosha

Wanaotumia magari binafsi ndani ya jiji wanalazimika kusimama mara kwa mara katika vizuizi vya polisi na jeshi na kutakiwa kuonyesha vitambulisho vyao na sababu za safari zao.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) watu wameonekana wakiingia na kutoka na magari binafsi au taxi huku baadhi ya mashirika ya ndege ya ndani na ya kimataifa yakiendelea na safari.

Baadhi ya ndege zimeonekana zikipaa na kushuka ikiwemo ya Shirika la ndege la Qatar Airways inayofanya safari za kimataifa. Hata hivyo, usafiri wa umma ambao mara nyingi huwa mitaa ya uwanja huo wa ndege umeadimika.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema hali ya usalama wa nchi unazidi kuimarika siku hadi siku na kwamba mpaka jioni wa Desemba 9 hali ilikuwa shwari nchi nzima na polisi wanaendelea kulinda usalama wa watu na mali zao.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinazidi kuimarisha ulinzi jioni ya leo ili kuhakikisha kuwa hakuna vitendo vitakavyovunja amani.

Misime amewataka Watanzania kupuuza picha na video zinazosambaa mtandaoni zikionyesha kuwa kuna maandamano ni uzushi kwa kuwa wanatumia picha na video hizo wakati wa maandamano yaliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks