Kihongosi: Viongozi wazembe Serikalini kukiona
- Utendaji wa viongozi kupimwa kwa viwango vipya vya uwajibikaji.
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetoa onyo kali kwa viongozi wa Serikali kikiahidi kumchukulia hatua yeyote atakayeshindwa kutimiza majukumu yake au atakayebainika kufanya kazi kwa maslahi binafsi.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 19, 2025 mkoani Dodoma, amesema viongozi hao wanaounda awamu ya pili ya Serikali ya awamu ya sita wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu wakiweka mbali maslahi binafsi na uzembe.
“Chama hakitasita kumchukulia hatua kiongozi yoyote wa Serikali awe mteuliwa awe mchaguliwa ambaye atakwenda kufanya kazi kwa maslahi yake binafsi,’’ ameeleza Kihongosi.
Kihogosi ametoa maagizo hayo kwa mara ya kwanza baada ya kukamilika kwa uchaguzi na uteuzi wa viongozi wa juu wa Serikali ikiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Spika wa Bunge, Naibu Spika wa Bunge, Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri.
Kihongosi amesisitiza kuwa rungu la kuwawajibisha wazembe litawagusa viongozi wote waliopo madarakani kwa tiketi ya chama hicho kuanzia mawaziri hadi watendaji wa vijiji.
CCM imesema kuwa vigezo maalumu vitatumika kupima utendaji wa kila kiongozi, na yeyote atakayeshindwa kufikia viwango hivyo atachukuliwa hatua mara moja.
Hatua hizo zinaweza kujumuisha mashauriano na Mwenyekiti wa Chama kwa ajili ya hatua za kiutawala, pamoja na hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani, kufilisiwa au hata kifungo.
Ahadi za CCM zaanza kutekelezwa ndani ya siku 16
Kihongosi ameeleza kuwa ndani ya siku 16 tu tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani baada ya kuapishwa Novemba 3, 2025, baashi ya ahadi zilizotolewa na chama hicho zimeanza kutekelezwa
Miongoni mwa ahadi hizo ni pamoja na utoaji wa ajira mpya 12,000 ambazo zinajumuisha walimu 7,000 na wahudumu wa afya 5,000, pamoja na kutolewa kwa marufuku ya hospitali kuzuia miili ya marehemu kutokana na maagizo ambayo kwa sasa yanatekelezwa nchi nzima.
“Kila Mtanzania tunamuomba aweze kulinda amani ya nchi yetu taifa hili ni la kwetu. Tanzania hii ni ya kwetu, nchi hii ikiharibika hatuna nchi nyingine wajibu wa kulinda ni wa kwetu sote kwa hiyo tudumishe umoja upendo na mshikamano wa taifa,” amehitimisha Kihongosi .
Latest