Rais Samia Suluhu Hassan atangaza baraza jipya la mawaziri
- Amemteua Noel Nanauka kuwa Waziri Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana na Paul Makonda kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Dar es Salaam Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza baraza jipya la mawaziri, likiwa na jumla ya wizara 27 ikiwemo ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.
Rais Samia aliyekuwa akitangaza baraza hilo leo, Novemba 17, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma amesema kuwa marekebisho yaliyofanyika yamelenga kuimarisha utendaji wa Serikali pamoja na kuboresha mahusiano kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii.
“Tumefanya marekebisho kidogo kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana sasa tumeona kuna haja ya kuwa na Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano,” ameeleza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambayo awali ilikuwa chini ya Ofisi ya Rais, imerejeshwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kurahisisha usimamizi wa shughuli za Serikali.
Walioteuliwa katika baraza jipya ndani ya Wizara 27
Kwa mujibu wa Rais Samia katika baraza hili jipya kutakuwa na jumla ya na mawaziri 27 na manaibu mawaziri 29.
Katika Ofisi ya Rais, Ridhiwani Kikwete ameteuliwa kuwa Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Prof Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, huku Joel Nanauka akiongoza wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana.
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Waziri ni Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, akisaidiwai Dk Festo John Dugange.
Kwa upande wa Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi ataongoza Sera, Bunge na Wenye Ulemavu; Deus Sangu ataongoza Kazi, Ajira na Mahusiano na Prof Riziki Shemdoe ataongoza Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akisaidiwa na manaibu wawili.
Wizara ya Fedha inaongozwa na Balozi Khamis Omar, huku diplomasia ikiendelea chini ya Balozi Mahmoud Kombo.
Katika sekta za uchumi, kilimo na miundombinu, Daniel Chongolo ataongoza Kilimo, Jumaa Aweso Wizara ya Maji, Abdallah Ulega Wizara ya Ujenzi, na Prof Makame Mbarawa Wizara ya Uchukuzi.
Usalama wa ndani unaendelea chini ya Boniface Simbachawene, na ulinzi chini ya Dk Rhimo Nyansaho.
Katika huduma za jamii, Mohamed Mchengerwa ataongoza Wizara ya Afya, Prof Adolf Mkenda Wizara ya Elimu, Dk Dorothy Gwajima Maendeleo ya Jamii, na Dk Ashatu Kijaji Maliasili na Utalii.
Aidha, Dk Leonard Akwilapo ataongoza Wizara ya Ardhi, huku Angellah Kairuki akiendelea kuongoza Mawasiliano na Tehama.
Katika sekta za uzalishaji, Anthony Mavunde ataongoza Madini, Deogratius Ndejembi Nishati, na Balozi Dk Bashiru Ally Kakurwa Mifugo na Uvuvi.
Kwa upande wa Prof Palamagamba Kabudi amepewa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akisaidiwa na manaibu wawili ambao ni Hamisi Mwinjuma na Paul Christian Makonda.

Aidha, uapisho wa mawaziri na naibu mawaziri wateule utafanyika Ikulu Chamwino Dodoma Novemba, 18 2025 kuanzia saa 05.00 asubuhi.
Latest