INEC yamteua upya Luhaga Mpina kugombea urais uchaguzi mkuu 2025

September 13, 2025 1:24 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Chama chake chakataa kupokea gari kwa ajili ya usaidizi wa kampeni.
  • Idadi ya wagombea wa urais waliopitishwa na INEC mpaka sasa imefikia vyama 18.

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemteua rasmi Luhaga Mpina kuwa mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Hatua hii imekuja baada ya mgombea huyo kushinda kesi aliyofungua kupinga uamuzi wa kuenguliwa kwenye mchakato wa uteuzi.

Akizungumza wakati wa kupokea fomu za uteuzi leo Septemba 13, 2025, Mwenyekiti wa INEC Jaji Jacobs Mwambegele,amebainisha kuwa uteuzi wa Mpina na mgombea mwenza wake Fatma Fereji, umetokana na kutimiza masharti ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

“Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Mheshimiwa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji kuwa mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo. Waheshimiwa wagombea,” amesema jaji Mwambegele.

Awali, Agosti 27, 2025, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na INEC ilitengua uteuzi wa Mpina wa ACT Wazalendo na Wilson Elias wa ADC, ikidai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama hivyo. 

Hata hivyo, Mahakama Kuu, Masijala Kuu Dodoma, ilitengua uamuzi wa INEC wa kumzuia Mpina kurejesha fomu zake za uteuzi na kubainisha kuwa uamuzi huo uliwaathiri waleta maombi hivyo wanapaswa kupewa fursa ya kurejesha fomu.

Kwa mujibu wa taratibu, Mpina amekabidhiwa fomu za uthibitisho pamoja na nakala ya tamko la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025.

Aidha, kama ilivyo kwa wagombea wote, tume hukabidhi gari na dereva kwa ajili ya matumizi ya kampeni, ingawa ACT Wazalendo kupitia mwanasheria wake Omar Shaaban imesema haitachukua gari hilo.

Kwa uteuzi huu, idadi ya wagombea wa urais waliopitishwa na INEC mpaka sasa imefikia vyama 18, ambao wote wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks