Shangwe ACT Wazalendo Mahakama ikiruhusu Mpina kurejesha fomu ya Urais
- Yasema INEC kutopokea fomu ya Mpina ilimnyima haki ya kikatiba pamoja na haki ya kusikilizwa.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masijala Kuu Dodoma, imetengua uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wa kumzuia Luhaga Mpina, mgombea wa urais kupitia ACT-Wazalendo, kurejesha fomu zake za uteuzi.
Kwa mujibu Mahakama, uamuzi wa INEC uliofanyika Agosti 27, 2025 uliwaathiri waleta maombi, hivyo wanapaswa kupewa fursa ya kurejesha fomu.
Uamuzi huo ni matokeo ya shauri Na. 21692/2025 lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT Wazalendo pamoja na Luhaga Mpina dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza umesema INEC ni taasisi huru na haikupaswa kusikiliza maelekezo ya mtu au taasisi yoyote, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Hivyo tunasema kutokana na tamko hilo, waleta maombi wapewe fursa immediately kwa maana ya haraka iwezekanavyo, ya kuwasilisha fomu za mleta maombi wa pili (Luhaga Mpina) na mchakato wa kuzipokea uendelee pale ulipoishia tarehe 27/08/2025,” amesema Jaji Kagomba aliyekuwa akisoma uamuzi huo.
Aidha, Jaji Kagomba ameainisha kuwa kutopokea fomu ya Mpina, INEC ilinyima haki ya kikatiba na pamoja na haki ya kusikilizwa ambapo pamoja na mahakama kutoa uamuzi wa urejeshwaji wa fomu kuendelea, ombi la waleta maombi la kutaka kulipwa fidia ya Sh100 milioni limekataliwa.
Uamuzi wa mahakama umepokelewa kwa shangwe na baadhi ya wanachama wa ACT wakipongeza mahakama kwa uamuzi huo huku wakiwa na matumaini ya kurudi ulingoni kwa kishindo licha ya kuwa wapinzani wao wameshapiga hatu katika kukimbizana na ratiba za kampeni.
“Najua wametuacha lakini najua kwamba kampeni yetu itakuwa na nguvu sana,” amesema Khadija Yusuph moja ya wanachama waliokuwa wakifuatilia kesi kwa njia ya mtandao katika Ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Nukta Habari.
Itakumbukwa kuwa Mpina alikubaliwa kuwa mgombea urais kupitia ACT Wazalendo mara baada ya kujiunga katika chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako alikosa nafasi ya kugombea ubunge.
Baadaye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitengua uteuzi wake, ikidai kwamba usajili wake kama mgombea uliendeshwa kinyume na taratibu za chama, na kisha INEC kuzuia kuwasilisha fomu za uteuzi, licha ya chama chake kujaribu kuzirudisha.
Hata hivyo, uamuzi wa Mahakama haufanyi Mpina kuwa mgombea wa Urais moja kwa moja, kurudi kwa Mpina kunategemea na uamuzi utakaotolewa na INEC baada ya kupitia fomu ya urais itakaporudishwa.
Latest



