Mahakama yaipa Serikali siku tano kujibu kesi ya ACT Wazalendo
- Ni baada ya Mahakama kukataa ombi la Serikali kuongezewa siku 14.
- Yatoa wito kwa wananchi kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo kupitia kiunganishi maalumu kitakachotolewa.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu Dodoma, imetoa siku tano kwa Serikali kujibu kesi iliyofunguliwa na Chama cha ACT Wazalendo na mwanasiasa Luhaga Mpina dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
ACT Wazalendo walifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa INEC wa kumzuia mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho Luhaga Mpina kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kwenye nafasi hiyo jana Agosti 27.
INEC ilifikia uamuzi huo mara baada ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kutengua uteuzi wa Mpina kuwa mgombea urais kupitia ACT baada ya kile kinachodaiwa kuwa ukiukwaji wa sheria na taratibu za chama hicho.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 28, 2025 na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa ACT, Mahakama imeitaka Serikali kutoa majibu ya pingamizi ndani ya siku tano badala ya 14.

Taarifa ya Mwanasheria wa ACT imebainisha kuwa, mahakama imesema endapo itabaini INEC ilikiuka masharti ya Katiba na Sheria, itatoa amri ya kumpa Mpina fursa ya kurejesha fomu zake na hatimaye kuteuliwa kugombea urais.
Aidha, Mahakama imeagiza kuwa kesi hiyo itatajwa na kuanza kusikilizwa kwa njia ya mtandao Septemba 3, 2025 saa tatu asubuhi ambapo imetoa wito kwa wananchi kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo kupitia kiunganishi cha mtandaoni ambacho kitawasilishwa rasmi na Mahakama.
Latest



