ACT Wazalendo watofautiana na INEC Mpina kutogombea urais wa Tanzania
- Walaani hatua ya INEC na kudai inakiuka na kuvunja moja kwa moja Katiba, Sheria na Kanuni za nchi.
- Wawataka Watanzania kote nchini kusimama imara kudai haki.
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakikubaliani na uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wa kumzuia mgombea wake wa urais Luhaga Mpina, kurejesha fomu za uteuzi kikidai kuwa kitendo hicho ni kinyume na Katiba, Sheria na Kanuni za Uchaguzi.
Taarifa ya Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo ya leo Agosti 27, 2025, inaeleza kuwa chama hicho kinapinga uamuzi uliofanywa dhidi ya mgombea wao.
Hiyo ni kwa sababu alifuata taratibu zote za kisheria, ikiwemo kuteuliwa rasmi na chama, kutambulishwa kwa INEC na kukabidhiwa fomu za uteuzi kwa mujibu wa sheria.
“ Tume ya Uchaguzi ilituandikia barua Agosti 23, 2025 ikitupatia utaratibu wa urejeshaji fomu kwa mgombea wetu, kwamba turejeshe fomu Agosti 27, 2025 saa 7:00 mchana…
…Hata hivyo, leo tulipofika ofisi za Tume ya Uchaguzi tulikuta ‘deployment’ kubwa ya askari wakituzuia kuingia ofisi za Tume wakitueleza kuwa wana maelekezo kwamba Mpina hatakiwi kurejesha fomu,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, ACT wamesema kuwa, watafungua shauri mahakamani kupinga kile walichokiita ni ukandamizaji wa haki za kisiasa na kutaka mchakato wa uchaguzi usimame mara moja hadi suala la kuzuiwa kurejesha fomu lipatiwe ufumbuzi wa kisheria.
Itakumbukwa kuwa usiku wa kuamkia leo Jumatano, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ilitoa taarifa ya kutengua uteuzi wa Luhaga Mpina baada ya kubaini ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Katiba na Kanuni za chama hiko.
Uamuzi huo, unakuja baada ya ofisi hiyo kuwakutanisha viongozi wa chama hicho na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala aliyelalamikia kupitishwa kwa Mpina, akidai kulivunja kanuni.
Mpina amekutana na kigingi hicho siku moja kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya uteuzi wa wagombea udiwani, ubunge na urais watakaoshiri Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
Baada ya hatua hiyo, inafuata hatua ya kuweka mapingamizi dhidi ya mgombea urais, hatua inayoweza kuwekwa na mgombea mwingine yeyote, msajili wa vyama au Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwisho wa kuweka pingamizi kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, ni hadi kesho Agosti 28, saa 10:00 jioni, isipokuwa kama aliyeliweka ni Msajili wa Vyama vya Siasa, ukomo wake ni ndani ya siku 14 baada ya siku ya uteuzi.
Hata hivyo, sio Mpina pekee aliyekutana na kigingi hiko, hata mgombea wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Wilson Elias utezi wake umetenguliwa , kwa madai ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria katika mchakato wa uteuzi ndani ya chama chake.
Latest



