Si Kweli: Serikali imepunguza vipimo vya VVU kwa wajawazito
- Wizara ya Afya imesema vipimo vya VVU kwa wajawazito na wanaonyonyesha hufanyika mara tatu kuanzia kipindi cha ujauzito hadi baada ya kujifungua, na si mara mbili kama inavyodaiwa.
Dar es Salaam. Huenda ukawa umekutana na taarifa zinazodai kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imepunguza idadi ya vipimo vya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa wajawazito kutoka mara tano hadi mara mbili. Wizara ya Afya imesema taarifa hizo si za kweli.
Taarifa hizo potofu zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kupunguzwa kwa idadi ya vipimo kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, zikidai mabadiliko hayo yameanza kutekelezwa mwaka huu.
Ukweli ni Huu
Kwa mujibu wa tamko la Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, vipimo vya VVU kwa wajawazito na wanaonyonyesha hufanyika mara tatu (3) kuanzia kipindi cha ujauzito hadi baada ya kujifungua, na si mara mbili kama inavyodaiwa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya kipimo cha kwanza hutolewa wakati wa hudhurio la kwanza la kliniki ya wajawazito, pamoja na uchunguzi wa kaswende na homa ya ini. Kipimo cha pili hutolewa kati ya wiki ya 32 na 36 za ujauzito na Kipimo cha tatu hutolewa ndani ya miezi mitatu baada ya kujifungua.
Kwa walio kwenye makundi hatarishi, vipimo hufanyika kila baada ya miezi mitatu na hutolewa dawa kinga (PrEP).
Wizara ya Afya imesema kuwa upimaji huu unatosha kubaini maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya ngono kwa lengo la kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Aidha, Wizara ya Afya imesisitiza kuwa mwongozo wa Tanzania unafuata mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na matokeo ya tafiti mbalimbali, na kwamba huduma za upimaji wa VVU zinaendelea kutolewa bila malipo katika vituo vyote vya afya nchini.
Latest



