Nyama, nguo vyapunguza mfumuko wa bei Tanzania
- Kasi ya mfumuko wa bei wapungua hadi asilimia 3.2 kutoka 3.3.
- Nchi za Kenya na Uganda zashuhudia ongezeko la mfumuko wa bei
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Aprili 2025 imepungua kidogo nchini ikichangiwa zaidi na kushuka kwa bei ya bidhaa zisizo za vyakula na sizizo za vyakula ikiwemo nyama, samaki, nguo.
Katika mwaka ulioishia Aprili 2025, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 3.2 kutoka kasi ya asilimia 3.3 iliyorekodiwa katika mwaka unaoishia Machi 2025.
Mfumuko wa bei ni kasi ya ongezeko la bei ya bidhaa na huduma nchini na kwa mujibu wa NBS kupungua kwa mfumuko huo wa bei maana yake kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma imepungua kuliko ilivyokuwa Machi mwaka huu.
“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na kuku wa kienyeji na wa kisasa kutoka asilimia 12.9 hadi asilimia 5.6; nyama ya ngombe (kutoka asilimia 22.1 hadi asilimia 18.9); na nyama ya mbuzi kutoka asilimia 15.4 hadi asilimia 14.8,” imeeleza NBS katika taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei iliyotolewa leo Mei 8, 2025.

Aidha, bidhaa zisizo za chakula zilizosaidia kupunguza mfumuko wa bei ni pamoja na nguo za wanaume kutoka asilimia 1.9 hadi asilimia 1.5, nguo za watoto (kutoka asilimia 1.5 hadi asilimia 1.4) na mkaa kutoka asilimia 13.1 hadi asilimia 8.5.
Kasi hiyo ya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Aprili 2025 imeendelea kuwa ndani ya malengo ya Serikali ya wigo wa asilimia 5 licha ya kuwepo kwa presha kutoka katika soko la dunia ikiwemo hatua ya Marekani kuongeza ushuru wa bidhaa zinazoingizwa nchini humo.
Mfumuko huo wa bei umeshuka ikiwa ni mwezi mmoja tangu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itangaze kubakiza Riba ya Benki ya Kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 6 ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kudhibiti mfumuko wa bei.
NBS imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2025 umepungua hadi asilimia 5.3 kutoka asilimia 5.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2025.
Mfumuko wa bei usiojumuisha bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Aprili, 2025 umesalia asilimia 2.3 kama ilivyokuwa mwaka ulioishia Machi, 2025.
Maumivu kwa majirani Kenya na Uganda
Wakati mfumuko wa bei ukipungua Tanzania,NBS imeeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa nchi za jirani ikiwemo Kenya na Uganda kwa mwaka unaoishia mwezi Aprili 2025 umeongezeka.
Nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2025 umeongezeka hadi asilimia 3.5 kutoka asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Machi, 2025 huku nchini Kenya, ukiongezeka hadi asilimia 4.1 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Machi 2025.
Latest


