Bajeti ya Wizara ya Maji yapaa kwa asilimia 61 mwaka 2025/26
- Zaidi ya asilimia 90 ya bajeti kutekeleza miradi ya maendeleo.
- Miradi 1,544 ya maji kutekelezwa nchi nzima ikijumuisha miradi mikubwa ya kimkakati.
Dar es Salaam. Wizara ya Maji imeliomba Bunge liidhinishe Sh1.017 kama bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambayo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 kutoka Sh627.78 bilioni mwaka 2024/25.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni, leo Mei 8, 2025 Waziri wa Maji Juma Aweso amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya bajeti hiyo itatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwa ajili ya ikiwemo kuongeza usambazaji wa huduma ya maji kwa Watanzania.
Aweso ameongeza kuwa kati ya bajeti hiyo zaidi ya Sh73.78 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Sh55.70 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa wizara, Ruwasa, Mfuko wa Maji na Chuo cha Maji na Sh18.08 bilioni zitaelekezwa kwenye matumizi mengineyo ya uendeshaji.
“Ninaomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya Sh1trilioni kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2025/26. Hii ni ongezeko dogo kutoka matumizi ya kawaida ya mwaka uliopita yaliyokuwa Sh 69.66 bilioni,” amesema Waziri Aweso.
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, ambayo inachukua sehemu kubwa ya bajeti, Serikali imepanga kutumia Sh943.12 bilioni mwaka 2025/26, ikilinganishwa na Sh558.12 bilioni mwaka uliopita.

Kati ya fedha hizo, Sh340.46 bilioni sawa na asilimia 36.1 ni fedha za ndani na Sh602.65 bilioni sawa na asilimia 63.9 ni fedha za nje.
Ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo fedha za nje zilikuwa Sh217.65 bilioni mwaka huu kumekuwa na ongezeko la Sh385 bilioni, sawa na asilimia 176, linalotokana na ushirikiano na wahisani wa maendeleo wa kimataifa.
Waziri Aweso ameeleza kuwa bajeti hiyo imelenga kutekeleza miradi mikubwa ya maji vijijini na mijini, kuboresha vyanzo vya maji, kupanua huduma katika maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji na kuimarisha taasisi za sekta hiyo kwa ajili ya kudumisha huduma endelevu.

Vipaumbele vya Wizara ya Maji mwaka 2025/26
Waziri Aweso ameongeza kuwa katika mwaka 2025/26 Wizara ya Maji imeainisha vipaumbele maalum vya sekta ya maji ikiwemo utekelezaji wa jumla ya miradi 1,544 ya maji nchini kote, ambapo miradi 1,318 itatekelezwa vijijini na miradi 226 mijini.
Vipaumbele vingine ni “kukamilisha mpango kabambe wa Taifa wa maji (National Water Master Plan), pamoja na kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji na uendelezaji wake kupitia uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua.” imeeleza hotuba ya Waziri Aweso.
Wizara pia imelenga kuimarisha usimamizi na udhibiti wa ubora wa maji ili kuhakikisha yanakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, sambamba na juhudi za kudhibiti upotevu wa maji na kuimarisha utoaji wa huduma endelevu.
Juhudi nyingine zitakazopewa kipaumbele ni utekelezaji wa miradi ya gridi ya Taifa ya maji, ikiwemo mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Dodoma na Singida, kutoka Ziwa Tanganyika kwenda Kigoma, Katavi na Rukwa, kutoka Mto Ruvuma kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi, pamoja na kutoka mto Rufiji kwenda Dar es Salaam na Pwani.
Vilevile, maji kutoka maziwa ya Victoria na Nyasa yatapelekwa kwenye maeneo jirani, hasa vijiji vilivyo karibu na maziwa hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Jackson Kiswaga amesema kamati hiyo ya Bunge kwa kauli moja inampongeza kwa kazi nzuri Waziri wa Maji na kuitaka Serikali kuhakikisha inatoa fedha kwa wakati na uaminifu ili kuiwezesha wizara hiyo kutimiza majukumu yake.
Latest


