Ratiba ya mazishi ya Papa Francis
- Mwili wa Papa Fransisko utawekwa hadharani kwa ajili ya ibada na heshima za mwisho Jumatano, Aprili 23.
- Papa Fransisko atazikwa rasmi Aprili 26 saa 4:00 asubuhi (saa za Vatican).
Dar es salaam. Ulimwengu unaendelea kuomboleza kifo cha Baba Mtakatifu Papa Francis, aliyefariki dunia Jumapili, Aprili 20, 2025, baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.
Papa Francis, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 88, alikuwa akikabiliwa na changamoto za kiafya kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku akilazwa mara kadhaa hospitalini kabla ya hali yake kudhoofika siku chache kabla ya kifo chake.
Ofisi ya Habari ya Vatican imetangaza rasmi ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, ambapo shughuli zitafanyika kwa heshima ya juu kwa kuzingatia utaratibu wa kipapa.
Mwili wake kuwekwa hadharani
Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican siku ya Jumatano, Aprili 23, mwili wa Papa Fransisko utahamishiwa kutoka Casa Santa Marta, alikokuwa akiishi, hadi katika Kanisa Kuu, Basilika ya Mtakatifu Petro saa 3:00 asubuhi.
Safari ya jeneza lake imepangwa kupita katika uwanja wa Santa Marta na uwanja wa mashahidi wa kwanza wa Kirumi, kisha kuingia katika uwanja wa Mtakatifu Petro kupitia ‘Arch of the Bells’ na hatimaye kupitia mlango wa kati wa kanisa.
Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Kirumi, ataongoza ibada ya uhamishaji (rite of translation) kwa sala fupi kabla ya mwili kuwekwa hadharani kwa waamini kutoa heshima zao. Kisha Kardinali Camerlengo ataongoza Liturujia ya Neno katika Madhabahu ya ‘Confession’ ndani ya Kanisa Kuu, kabla ya watu kuanza matembezi ya kuaga mwili wa Baba Mtakatifu.
Ibada ya mazishi Jumamosi
Mazishi ya Papa Francis yatafanyika siku ya Jumamosi, Aprili 26, saa 4:00 asubuhi (saa za Vatican), katika Uwanja wa Mtakatifu Petro.
Misa takatifu ya mazishi itaongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Mkuu wa Baraza la Makardinali, na kushirikishwa na Maaskofu Wakuu wa Kiyunani (Patriarchs), Makardinali, Maaskofu, Maaskofu Wakuu na mapadre kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ibada hiyo ya Ekaristi itahitimishwa kwa ibada ya Sala ya kumkabidhi marehemu kwa Mungu ‘Ultima commendatio’ na salamu ya mwisho ‘Valedictio’, ishara ya mwisho ya Kanisa kwa Papa, kabla ya kuanza rasmi kwa siku tisa za maombolezo ‘Novemdiales’ na Misa kwa ajili ya kuombea roho ya Baba Mtakatifu.
Mahali pa mazishi
Baada ya ibada ya mazishi, mwili wa Papa Fransisko utaingizwa rasmi ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, na baadaye kupelekwa katika Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu kwa ajili ya kuzikwa, ikiwa ni utekelezaji wa mapenzi yake mwenyewe ya kuzikwa katika unyenyekevu, tofauti na mapapa waliomtangulia.
Papa Fransisko aliwahi kueleza kuwa hatamani maziko ya kifahari, akitaka jeneza rahisi la mbao moja tu, bila matumizi ya majeneza matatu kama ilivyo desturi. Uamuzi huu unaakisi maisha yake ya unyenyekevu, ya kujitolea kwa maskini, na ya kuishi kama “mtumishi wa watumishi wa Mungu”.
Kwa sasa, Kanisa Katoliki linaingia katika kipindi cha ‘Sede Vacante’, ambapo kiti cha Papa hubaki wazi hadi Papa mpya atakapochaguliwa kupitia ‘Conclave’ ya Makardinali katika siku zijazo.
Latest



