Dk Mpango abainisha changamoto zinazoikabili sekta ya nishati EAC

March 5, 2025 6:57 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Uhaba wa rasilimali za kifedha na utegemezi wa gesi asilia vimetajwa kukwamisha maendeleo ya kiuchumi.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Isdor Mpango, ameainisha changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta ya nishati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akizitaja kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi wanachama.

Dk Mipango aliyekuwa akizungumza leo Machi 5, 2024 katika kongamano la 11 na maonesho ya petroli Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam amesema ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi huku vyanzo vya nishati na athari za mabadiliko ya tabianchi yakizingatiwa.

“Kwa upande mmoja, ni lazima tushughulikie changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinahitaji mabadiliko katika maisha yetu ya kila siku, ikiwemo vyanzo vya nishati tunavyotegemea. Kwa upande mwingine, tunayo mahitaji ya kijamii na kiuchumi ya watu wetu ambayo yanahitaji nishati na rasilimali za kifedha ili kuyakabili,” ameeleza Dk Mpango.

Wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano wa 11 wa petroli wa Afrika Mashariki.

Afrika Mashariki ina utajiri mkubwa wa rasilimali za nishati, ikiwa ni pamoja na gesi asilia inayopatikana nchini Tanzania, mafuta nchini Uganda, Kenya, na Sudan, pamoja na nishati ya maji na ‘geothermal’ inayopatikana katika mataifa kama Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Kenya.

\Licha ya utajiri huo wa rasilimali za nishati, Dk Mpango amebainisha kuwa uhaba wa kifedha na utegemezi wa gesi asilia umekuwa ukikwamisha maendeleo ya kiuchumi katika nchi za jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wake, endapo nchi za jumuiya hiyo zikikabiliana na changamoto hizo zitaweza kukuza uchumi wake kwa kutumia nishati hiyo katika kuendesha viwanda na kuiuza katika nchi wahitaji.

“Zaidi ya hayo, vyanzo hivi vya nishati vinaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa Serikali zetu, ambayo yanaweza kuwekeza tena katika miundombinu na maendeleo ya rasilimali watu, na hivyo kusaidia ajenda pana ya maendeleo,” amesema Dk Mpango.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma muhimu za kijamii, hasa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na huduma za umeme kwa gharama nafuu.

Naye, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, amesema kuwa kadri uchumi unavyokua, mahitaji ya nishati yanaongezeka, hasa gesi asilia ambayo ni mhimili mkubwa wa maendeleo ya nchi.

Biteko ameongeza kuwa Tanzania imefanikiwa kuimarisha uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu vya Songosongo na Mnazi Bay, ambavyo ni msingi wa maendeleo ya sekta hiyo. 

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango, akiwa anatembela mabanda ya maonesho wakati wa mkutano wa 11 wa petroli wa Afrika Mashariki.

Pia, amebainisha kuwa gesi asilia iliyogunduliwa katika eneo la Ntoria, kitalu cha Ruvuma, inaendelea kuendelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya L Petroleum, huku ushiriki wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kituo cha Mnazi Bay ukiongezeka kutoka asilimia 20 hadi asilimia 40.

 Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Uganda, Ruth Nankabirwa, amebainisha  kuwa nchi yake inaendelea kuboresha miundombinu ya nishati huku ikiimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta.

Nankabirwa amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya nchi zote mbili na kanda kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks