Rais Samia: Elimu, uongozi visiwasahaulishe wanawake wajibu wa malezi
- Asema kutimizwa kwa wajibu huo kutasaidia kujenga jamii bora.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake wenye elimu na nafasi za uongozi katika taasisi na mashirika ya umma kutothamini tu taaluma zao bali kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto wao ili kujenga jamii bora.
Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya maadhimisho ya miaka 10 ya programu ya mwanamke kiongozi iliyofanyika leo Februari 21, 2025 jijini Dar es Salaam amesisitiza kuwa nafasi za uongozi kwa wanawake hazipaswi kuwa sababu ya kuyumba kwa maisha ya kifamilia.
“ Elimu mnazopata na stadi za uongozi mnazopewa zikainufaishe jamii, familia na Taifa kwa ujumla, haitegemewi kuwa usomi au nafasi za uongozi unayoipata mwanamke iwe sababu ya kuvuruga familia au kuharibu watoto wake,’’ ameeleza Rais Samia.
Rais Samia pia ameeleza kuwa jitihada za kuendelea kuielimisha jamii kufahamu kuwa usawa wa kijinsia sio mapambano ya wanawake kutaka kuwa juu ya wanaume bali ni hitajio la ibara ya 12 ya Katiba ya Tanzania isemayo binadamu wote wamezaliwa huru na binadamu wote ni sawa.

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa kusahau wajibu wa malezi kunaweza kusababisha athari mbaya kama vile watoto kujiingiza katika mienendo isiyofaa, kuwa tegemezi na hatimaye kuwa mzigo kwa Taifa, jambo linaloweza kuleta huzuni na aibu kwa wazazi wao.
Rais Samia amebainisha kuwa wanawake kusahau wajibu wao kutarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuelimisha mtoto wa kike na kuhalalisha hoja za wahafidhina na waumini wa mfumo dume.

“Wakati ule hakukua na imani kabisa kwamba yule mwanamke anaweza kufika hapa hakukua, kuna waliothubutu kusema tuna Rais wa kuambiwa fanya tu anatafanya, kuna waliothubutu kusema hatuna Rais tuna ‘house girl’ (msaidizi wa kazi za nyumbani) kuna waliothubutu kusema maamuzi ya ‘kitchen party’ (sherehe inayofanywa kabla ya ndoa) yale ambayo nilokuwa nikifanya,” amesema Rais Samia.
Akiwahimiza wanawake waliopata nafasi za uongozi, Rais Samia amewataka kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na imani na elimu kwa mtoto wa kike, sambamba na kuwainua wanawake wenzao ili kuwasaidia kifikra.
“Nyie mna dhima kubwa ya kuwasaidia wanawake wenzenu hapa simanishi kuwa mkawapendelee bali mkawaongoze na muwasidie na wenyewe wanyanyuke. Mnakila sababu ya kufanya hivyo kwa sababu nyinyi mnajua majungu na hila zilizopo kule mlipotoka kwa wanawake,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, Rais Samia amewahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akibainisha kuwa taasisi zinazoongozwa na wanawake zimekuwa zikifanya vizuri katika utendaji wake.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzanne Ndomba ameeleza kuwa kwa miaka 10 iliyopita, programu hiyo imewawezesha wanawake 643 kupata mafunzo ya uongozi.
Kwa wastani, kila mwaka kumekuwa na washiriki 45, huku awamu ya tatu ya programu ikiwa na idadi ndogo ya washiriki 21 kutokana na athari za janga la Uviko 19 ingawa awamu ya 10 imekuwa na idadi kubwa zaidi ya washiriki 110.
Maadhimisho haya ya miaka 10 ya programu ya Mwanamke Kiongozi yameambatana na mahafali ya wahitimu wa awamu ya 10 ya mafunzo hayo, huku lengo kuu likiwa ni kuwawezesha wanawake kupata ujuzi wa uongozi na kuwa na mchango mkubwa katika jamii.
Latest



