Ifahamu Deep seek AI, mshindani wa Chat GPT
- Deep Seek AI imepata umaarufu hivi karibuni baada ya kuzindua modeli yake DeepSeek R1.
Arusha. Wakati matumizi ya akili mnemba yakiendelea kushika kasi katika shughuli mbalimbali duniani, hivi karibuni kuna ugunduzi mpya wa teknolojia ya akili mnemba unayotajwa kuwa mpinzani wa Chat GPT.
Kwa wasiofahamu ChatGPT ni programu ya mawasiliano ya akili mnemba inayotumia teknolojia ya hali ya juu ya lugha asilia (Natural Language Processing – NLP) kuwezesha mawasiliano yanayoiga mazungumzo halisi ya binadamu.
Kupitia teknolojia hii yenye matoleo manne tangu kuanzishwa kwake na kampuni ya Open AI mwaka 2018 watumiaji wanaweza kuuliza maswali yanayohitaji ufafanuzi wa kina, kupata usaidizi wa kuandika ripoti, makala na maudhui mengine pamoja na kutafsiri lugha.
Kwa mujibu wa Tovuti ya Open AI ambayo ni wamiliki wa teknolojia hiyo, Chat GPT hutumiwa na wastani wa watu milioni 250 duniani kote ikitarajiwa kufikia watu bilioni 1 kwa wiki kufikia mwisho wa mwaka huu.
Hata hivyo, huenda lengo hilo lisifikiwe baada ya kampuni ya Deep seek kutengeneza teknolojia mpya ya akili mnemba ambayo inahusika zaidi na mawasiliano yenye uwezo sawa na ChatGPT.
Deep Seek AI imepata umaarufu hivi karibuni baada ya kuzindua modeli yake DeepSeek R1 ambayo inadaiwa kuwa na uwezo mkubwa mfano wa Open AI lakini kwa gharama nafuu zaidi.
Hadi kufikia Januari, 2024 ikiwa ni mwezi mmoja tangu kuzinduliwa kwa model mpya Deep Seek AI imepakuliwa na watumiaji zaidi ya milioni 10 katika App store.
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/b4f477a86dfb19bb780df49bd45fe1a4.jpg?resize=1024%2C576&ssl=1)
Deep Seek AI inafananishwa na toleo la juu zaidi la ChatGPT (version 40) ambalo ili uipate unalazimika kuilipia.PichaYahoo.
Tofauti kati ya Chat GPT na Deep seek AI
Tovuti ya Data Camp inabainisha kuwa japo teknolojia hizo zina muundao unaofanana ila zinatofautiana kwenye masuala kadhaa ikiwemo upatikaaji na gharama ya kupata huduma hiyo.
Toleo jipya la akili bandia ya Deep Seek kwa sasa hupatikana bure ikiwawezesha watumiaji wapya kuipakua kwa urahisi na kuanza matumizi yake bila gharama zozote wakati ChatGPT inatumia modeli ya ‘freemium’, ikimaanisha kuwa inatoa huduma za msingi bila malipo lakini ikihitaji malipo kwa huduma za hali ya juu.
Victor Matiku miongoni mwa watumiaji wa akili mnemba anasema kuwa Deep seek Ai ni rafiki kwa matumizi kwani haihitaji malipo huku ikitumia feature za hali ya juu ambazo alilazimika kulipia.
“Chat GPT 4.0 (toleo la juu zaidi ya Chat GPT) inaaminika kuwa ‘smart and faster’ lakini lazima aulipie kuipata, ‘Now Deep Seek AI’ ni mara kumi zaidi ya ChatGPT 4.0 na ni bure,” amesema Matiku.
Tofauti nyingine kati ya teknolojia hizo ipo katika udhibiti wa maudhui na vizuizi ambapo DeepSeek imeonekana kuwa na msimamo wa wastani zaidi kuhusu mada tata, ikiruhusu majadiliano ya kina zaidi.
Kwa mfano, inaweza kushughulikia mada changamano au nyeti kwa kutoa majibu yenye muktadha unaoenda na hitaji lako wakati ChatGPT huzuia mazungumzo yanayohusu mada zisizofaa au zenye utata.
Kwa wanafunzi na watengeneza maudhui teknolojia zote mbili zinaweza kusaidia katika kuandaa nyaraka au kuunda maudhui, lakini kila moja ina namna yake ya utendaji kazi.
ChatGPT ni bora zaidi kwa kuandaa maudhui yanayovutia na yenye mazungumzo (dialogue) yanayoendana na muktadha huku kueleza dhana ngumu ikiwemo zinazohusu takwimu kwa urahisi zaidi
Kwa upande mwingine, DeepSeek AI ni hueleza mada kwa kutumia maneno machache yanayoeleweka zaidi huku ikikuruhusu kutoa majibu ya papo kwa hapo (real time conversation) kulinganisha na Chat GPT ambayo mara nyingi haina taarifa za matukio ya karibuni.
Licha ya faida lukuki za matumizi ya AI, wataalamu wa teknolojia wanashauri watumiaji wa AI kuwa makini wakati wa matumizi huku wakidhibiti na kuhakiki taarifa zinazotolewa na teknolojia hizo.
Latest
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/crypto-decoded-img.width-2000.jpg?fit=300%2C169&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/619263.png?fit=300%2C150&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/pound-coins-and-bank-notes-909209056-5af38dc11d64040036b164f8.jpg?fit=300%2C217&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/GjQX7wZXMAAnWUD.jpg?fit=300%2C222&ssl=1)