Hofu ya kukosa vizimba soko kuu yawaibua wafanyabiashara Mwanza
- Ni wale waliopisha ujenzi wa soko mwaka 2019 kwa kuahidiwa kupewa kipaumbele litakapokamilika.
- Baadhi wasema waliendelea kulipia vizimba licha ya kuwa ujenzi ulikuwa unaendelea.
Mwanza. Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mbugani jijini Mwanza walio ondolewa kupisha ujenzi wa soko kuu mkoani humo wameonyesha wasiwasi wa kutopata nafasi ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi baada ya kukosa vyumba na vizimba vya biashara kwenye soko hilo.
Wafanyabiashara rasmi katika masoko hutakiwa audha kuwa na chumba (fremu) au kizimba (meza) ya kufanyia biashara yake ambayo huilipia kodi iliyowekwa na mamlaka husika, hivyo wafanyabiashara hao huenda wakatakiwa kutafuta sehemu nyingine jambo wanalohofia litawarudisha nyuma kiuchumi.
Hofu hiyo imetanda kwa wafanyabiashara hao mara baada ya Jiji la Mwanza kutangaza tenda ya watu kuomba nafasi katika soko hilo katika kipindi hiki ambacho soko lipo mbioni kukamilika huku kukiwa hakuna kipaumbele kwa wafanyabiashara walioondolewa hapo awali.
Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mbungaji Jijini Mwanza wakiwa kwenye kikao cha pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuzungumzia hatima ya vizimba na vyumba vya biashara katika soko jipya la Mwanza. Picha na Mariam John/Nukta
Wafanyabiashara hao waliokiuwa wakizungumza mara baada ya kukutana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba wamesema waliahidiwa kupewa kipaumbele soko litakapokamilika tangu walipoondolewa mwaka 2019 kupisha ujenzi wa soko hilo.
Hata hivyo, wafanyabiashara wameeleza kuwa licha ya kuwa walipisha ujenzi wa soko katika kipindi chote cha ujenzi waliendelea kulipia gharama za meza zao wakati hawazitumii.
“Soko limekaribia kukamilika tunataka kurudi tunaambiwa hawakuweka soko la Samaki, wakati toka tulivyoondolewa mwaka 2019 tulikuwa tunalipia meza mpaka dakika hii na baada ya tenda kutoka tumeambiwa tutume baada ya hapo tunakuja kuambiwa sisi hatuna meza wakati sisi wauza samaki ni zaidi ya watu 100,” amesema Ester Nanai Mfanyabiashara wa samaki soko kuu Mbugani.
Kwa upande wake mfanyabiashara wa vitenge na nguo soko kuu Mbugani, Fidelis Mwita amesema wasiwasi wao ulikuwa ni kutaka kujua hatima yao iwapo watapata nafasi katika soko kuu baada ya ujenzi kukamilika.
“Kitu ambacho kinatupa wasiwasi mkubwa kuna wale ambao tulipisha mradi wa ujenzi huo na tukapewa ilani tunahofia kuwa hatutapata nafasi ya kurudi tena kule wataingia wengine lakini baada ya kukutana na Mkurugenzi kidogo imani inarudi kwamba tunaweza kurudi tena,” amesema Mwita
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati amesema mbali na kutokuwa na imani ya kupata vyumba lakini pia hata ikitokea wakikosa hawatasita kufika katika mamlaka za juu kupambania haki yao.
“Wasiwasi wetu ni huo kwa sababu moja ya sifa ambayo unatakiwa kutimiza wakati unaomba fomu ni kutaja namba ya chumba unacho kihitaji ina maana wakikuingiza kwenye mchakato wa kupata chumba hicho kama mmeomba watu 100 ina maana atapata mmoja na hao wengine 99 watakosa na watakuwa wamepoteza sifa ya kupata chumba au nafasi katika soko hilo,” amesema Masagati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomon Kibamba amesema wafanyabiashara waliondolewa katika soko hilo wenye sifa tu ndio watapewa kipaumbele sio watahakikishiwa kupata vizimba.
“Tuliweka sifa kwamba wale wafanyabiashara wa zamani watapewa kipaumbele sio watapata ila watapewa kupaumbele wakikidhi vigezo na wale wengine waliomba baada ya hawa wa kipaumbele kuisha nao watapata nafasi kupitia mfumo wa Tausi, kwa sasa hivi ambao watakuwa wamekosa ndo tutakuwa tumeishia hapo kwa sababu kila soko litakuwa na mchakato wake kama huu,” amesema Kibamba.