Fahamu faida za wanandoa kujua makundi yao ya damu

January 11, 2025 1:23 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni hatua muhimu kwa wanandoa kuboresha afya ya familia.

Dar es Salaam. Kufahamu makundi ya damu kabla na baada ya ndoa ni hatua muhimu inayowasaidia wanandoa kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya yao na ya familia watakayounda. 

Makundi ya damu si tu yanahusiana na urithi wa jeni (genetics) bali pia yanaweza kuwa na athari kubwa kwa masuala kama usalama wa ujauzito, kinga ya mwili, na hata ufanisi wa matibabu katika familia. 

Makundi ya damu ni nini?

Makundi ya damu ni njia ya kugawanya damu ya binadamu kulingana na aina za protini maalum zinazopatikana kwenye uso wa seli nyekundu za damu. 

Protini hizi hujulikana kama antijeni, na zipo katika aina mbili kuu yaani  ABO na Rh (Rhesus) ambapo mfumo wa ABO una makundi manne ya damu ambayo ni A, B, AB pamoja na O.

Kwa upande mwingine, mfumo wa Rh hugawanya damu kwa Rh chanya (+) au Rh hasi (-), kulingana na uwepo au ukosefu wa protini ya Rhesus kwenye seli za damu.

Makala hii inachambua kwa kina kwa nini wanandoa wanapaswa kuelewa makundi yao ya damu na jinsi maarifa haya yanavyoweza kuchangia afya bora ya kizai chao.

Mathalani wanandoa kutojua makundi yao ya damu kunaweza kusababisha tatizo la Rhesus (Rh incompatibility) linaloweza kuathiri usalama wa mtoto aliyepo tumboni, ambapo mtoto anaweza kuzaliwa na anemia au matatizo mengine yanayohusiana na mfumo wa damu. 

Rh incompatibility ni hali inayotokea wakati mama mjamzito ana kundi la damu la Rh hasi (-), lakini mtoto anayembeba ana kundi la damu la Rh chanya (+) alilorithi kutoka kwa baba. 

Hali hii husababisha mfumo wa kinga wa mama kutambua protini ya Rh kwenye damu ya mtoto kama “mgeni” na kuanzisha mchakato wa kutengeneza kingamwili (antibodies) dhidi ya damu ya mtoto.

Kujua makundi ya damu si tu suala la afya ya mwili, bali lina manufaa mengi ikiwemo kupunguza hatari ya matatizo ya kiafya kwa mama na mtoto, kusaidia kupanga matibabu mapema ya Anti D na kuwapatia wanandoa uelewa wa afya zao. 

Kwa mujibu wa Dk Deogratias Soka, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Siko Seli Tanzania, makundi ya damu yenyewe hayana tatizo, isipokuwa ni suala la ‘Rhesus factor’ linalopaswa kupewa umuhimu.

Dk. Soka ameileza Nukta Habari kuwa, “Rhesus si kundi la damu, lakini iwapo mwanandoa mmoja ana Rhesus chanya (Rh+) na mwingine ana Rhesus hasi (Rh-), inaweza kuleta athari kubwa.”.

Kwa mujibu wa Dk. Soka, kuwa na Rhesus chanya au hasi si tatizo moja kwa moja, bali matatizo hujitokeza pale ambapo mwanandoa mwenye Rh- anaoana na mwenye Rh+. 

Katika hali hii, mama mwenye Rh- (Rhesus hasi) anapooana na baba mwenye Rh+ (Rhesus chanya), kuna hatari ya mtoto wao kuathirika. 

Hii ni kwa sababu mama mwenye Rh- anaweza kuanza kutengeneza kingamwili (antibodies) dhidi ya damu ya mtoto mwenye Rh+ akiwa tumboni. Hizi kingamwili zinaweza kumdhuru mtoto katika mimba.

Aidha, Dk Soka amefafanua kuwa madhara kwa mama mwenye Rh- yanaweza kuwa makubwa, ikiwemo kuzaa mtoto kabla ya wakati au hata mtoto kufia tumboni. 

Hali hii hutokea kwa sababu mwili wa mama unakiona kiumbe kilichobebwa kama mvamizi, hivyo kingamwili zake huanza kukishambulia. 

Hata hivyo, Dk Soka amesema kuwa asilimia kubwa ya watu duniani wana Rhesus chanya, huku waliokuwa na Rhesus hasi wakiwa wachache.

Hivyo, ili kukabiliana na changamoto hii, wanawake wenye Rh- wanaweza kupatiwa sindano ya ‘Anti-D’ mara tu baada ya kujifungua mtoto wa kwanza. 

Sindano hii ni kinga maalum inayozuia kingamwili zinazotengenezwa mwilini mwa mama kushambulia ujauzito unaofuata. 

Sanjari na hayo kinga hii hufanya kazi mara moja tu, na hivyo ni muhimu kwa wanandoa kupima makundi ya damu na kupata ushauri wa kitabibu mapema.

Kwa kumalizia, kujua makundi ya damu si jambo la hiari kwa wanandoa, bali ni hatua ya msingi ya kujikinga dhidi ya madhara makubwa ya kiafya na kudumisha furaha katika familia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks