Jeshi la Polisi laimarisha ulinzi kuelekea sikuu za mwisho wa mwaka

December 24, 2024 5:01 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Lasema litawachukulia hatua watakaokiuka Sheria.

Arusha. Jeshi la Polisi limesema limejipanga vizuri kuimarisha usalama katika sikukuu za mwisho wa mwaka ambazo ni Christmas na Mwaka mpya.

Taarifa ya David Misime, Msemaji wa Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Disemba 24,2024 inafafanua kuwa Jeshi hilo litashirikiana na wananchi, viongozi wa nyumba za Ibada, kamati za usalama za nyumba za Ibada ambako Ibada mbalimbali zitafanyika na viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kila mmoja anasheherekea kwa amani na utulivu.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kusheherekea sikukuu hizo kwa kuzingatia amani, utulivu na usalama.

“Katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka, tukumbuke usalama unaanza na wewe mwenyewe kwa kujiepusha na vitendo vitakavyohatarisha usalama wako, mali zako na familia yako,”imesema taarifa ya Misime.

Jeshi hilo limevitaja vitendo hatarishi kuwa ni pamoja na kuacha nyumba bila uangalizi, kutumia vilevi kupindukia, kuacha watoto wakizurura hovyo bila uangalizi wa mtu mzima na mwenye akili timamu na kuepuka kuweka mali au fedha katika hali hatarishi.

Katika hatua nyingine Misime amebainisha kuwa wataendelea na zoezi la ukamataji kwa madereva  wanaovunja sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali pamoja na  kuutoa elimu ili kuzuia vitendo hivyo. 

“Tunatoa wito kwa kila mmoja wetu kukemeana papo kwa papo pamoja na kutoa taarifa pale tunapoona mwenzetu anafanya vitendo vya kizembe na vile vinavyohatarisha usalama wa maisha yetu barabarani…

..Baadhi ya ajali zilizotokea ukisikiliza mashuhuda inaonyesha wazi tungekuwa na utamaduni na uthubutu wa kukemeana zingeepukika hata kwa yale magari yaliyokuwa yanatumiwa na familia na mengineyo, imebainisha taarifa ya Misime.

Waziri wa Mambo ya Ndani Innocent Bashungwa akizungumza na waandishi wa habari Desemba 18, 2024 alitoa angalizo hilo pia kwa madereva, wasafiri pamoja na wazazi na walezi kuzingatia usalama tunapoelekea sikukuu za mwisho wa mwaka Krismas na Mwaka Mpya. 

Bashungwa aliwataka wasafiri na wasafirishaji kuzingatia na kuheshimu sheria za usalama barabarani kupunguza ajali zinazoepukika ili kuepusha vifo, majeraha au ulemavu utokanaona ajali za barabani.

“Yapo matukio ya ajali ambazo zinatokana na uzembe wa madereva, ama wamiliki wa magari kutofanyia matengenezo mara kwa mara vyombo vyao vya usafiri,” alisema Bashungwa.

Enable Notifications OK No thanks