Jinsi ya kuhakikisha usalama wa mali/samani wakati wa kuhama nyumba au ofisi
- Ni pamoja na kutenganisha vitu vya thamani pamoja na vile vinavyoweza kuharibika haraka (flagile).
- Mbinu hizi zinaweza kuokoa gharama ya kununua samani mpya kila mara unapohamia ofisi au nyumba mpya.
Dar es Salaam. Kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni moja ya sehemu ya maisha ya binadamu inayochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo za kijamii, kimazingira pamoja na zile za kiuchumi.
Wapo wanaohama kutoka maeneo waliyopanga iwe ni makazi au ofisi na kuhamia katika majengo yao huku wengine wakihamia katika maeneo mengine ambayo wameyapangisha.
Mchakato huu huwatoa jasho watu wengi, huku wengine wakijikuta wakiharibu samani zao pamoja na kupoteza vitu vya thamani katika maisha yao bila kutarajia.
Ikiwa wewe ni miongoni mwa wanaoharibu na kupoteza sehemu ya vitu vyako wakati ukihama kutoka eneo moja kwenye nyingine Nukta Habari imekuandalia mbinu saba zitakazopunguza tatizo hilo
Safisha mahali unapohamia
Kwa mujibu wa tovuti ya Assure Shift, wataalamu wa uhamishaji na usafirishaji wanashauri kabla ya kuanza kufunga mizigo yako unatakiwa kuhakikisha kuwa umeandaa mahali ambapo unatarajia kuhamia kwa kufanya usafi na kukarabati pale inapobidi.
Hii inasaidia usalama wa vitu vyako na kukuwezesha kuvipanga kwa urahisi pale tu unapowasili katika makazi mapya.
Usafi wa nyumba mpya unaweza kufanya na wataalamu au mtu binafsi. Picha| Weekend Maids
Punguza visivyo hitajika
Hakuna anayependa kuhama na lundo la mizigo ambayo huenda asiitumie siku za mbeleni, hivyo katika hatua hii unaweza kuchagua vifaa au samani za muhimu pekee zitakazokusaidia katika kazi au maisha yako.
“Kuondoa vitu visivyo muhimu kutarahisisha mchakato wa kuhama na pia kupunguza gharama. Unaweza kuuza vitu vyenye thamani sokoni, kuwapa wanafamilia/marafiki, au kuchangia mashirika ya hisani” isema tovuti ya Assure Shift.
Tenga vitu vyenye thamani na vile vinavyohitaji umakini kuhamisha (flagile)
Louise Oliphant, mtaalamu wa maswala ya uhamishaji kutoka Home Gardens ameshauri, kutenganisha vitu vyenye thamani ambavyo utalazimika kuwa karibu navyo ili visipotee au kuharibiwa wakati wa kuhama
Vifaa vingine vinavyohitaji umakini kubeba kama kompyuta mpakato pamoja na vifaa vyake, friji na makabati ya vioo ambayo ni vyema yakasafirshwa kivyake au kuwekwa sehemu moja kurahisisha ubebaji na usalama.
Orodhesha na ufungashe samani zako
Oliphant ameshauri kuandaa samani zako zote kwa kuzifunga mahali pamoja kama ikihitajika huku ukizioroshesha ili usisahau chochote wakati wa kubeba lakini hata wakati wa kushusha mizigo vifaa na mali zote ziwe salama.
Hatua hii itakusaidia kutopoteza wala kusahau vifaa vidogo vidogo kama remote za Tv, simu zisizotumika, funguo za makabati pamoja na flash au kamera ndogo.
Unaweza kupanga vifaa na samani zako kupitia maboksi maalum ambayo yatarahisisha ubebaji. Picha| Brisbane Conveyancing.
Andika orodha ya mizigo yako
Kwa upande wake tovuti ya Home Basic Loan wanashauri kuwa ni vizuri kuunda orodha ya kina ya vitu vya kuhamisha ili mwishoni mwa mchakato, uweze kukagua vitu vilivyofikishwa kwa usahihi na kudai bima kwa vitu vilivyoharibika au kupotea.
“Unaweza kupiga picha za mizigo kabla ya kufungashwa ili kuwa na ushahidi wa hali ya awali ya mali zako na nyumba. Picha hizi pia zitakuwa njia nzuri ya kukumbuka nyumba yako ya zamani na kumbukumbu ulizotengeneza huko” imesema tovuti ya Home Basic Loan inayojishughulisha na masuala ya utoaji wa mikopo mbalimbali ikiwemo nyumba.
Zingatia ya upakiaji wa mizigo yako
Baada ya kuorodhesha na kufunga mizigo hatua inayofuata ni kupakia mizigo katika magari maalum ya usafirishaji, kama unatumia wataalamu wa usafirishaji hauna haja ya kuwaza juu ya usalama wa vifaa vyako lakini kama unatumia wasafirishaji wa kawaida ni lazima kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uangalifu.
Katika zoezi hili hakikisha kuwa ,mizigo yako inakaa vizuri kwa kuzingatia matirio ya vitu husika. Hakikisha vitu vinavyovunjika au vile ambavyo ni rahisi kuharibika havigandamizwi na vitu vingine.
“Kama una watoto, hakikisha wanakaa mbali na wahamishaji kwani wanaweza kufanya kazi yao iwe ngumu zaidi au kujiumiza,” imeshauri tovuti ya Assure Shift.
Hakiki mizigo yako, fungua na anza kupanga
Baada ya mizigo kufika, wafanyakazi wataanza kufungua na kuunganisha tena samani zilizofungashwa. Hakikisha mchakato huu unafanywa kwa uangalifu ili kuepusha uharibifu.
Baada ya kufungua kila kitu, kagua mizigo kupitia orodha uliyoandaa awali kuhakikisha hakuna kitu kilichopotea au kuharibika. Ikiwa kuna uharibifu au upotevu unaweza kudai fidia kutoka kwa wasafirishaji.
Mara bada ya kuhakikisha kila kitu kiko salama unaweza kuipangilia ofisi yako au nyumba yako mpya kadiri ya mahitaji na matakwa yako na kuendelea kufurahia makao mapya.