Tishio: Ukatili dhidi ya watoto wa kiume ukiongezeka Tanzania
- Matukio 1,038 yaliripotiwa mwaka 2023 katika mikoa 11 kati ya 20 ukilinganisha na matukio 460 yaliyoripotiwa mwaka 2022.
- Mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Kagera, Tabora, yaongoza kwa ukatili wa watoto wa kiume.
Dar es Salaam. Huenda Serikali, wanajamii, viongozi wa dini wakatakiwa kuongeza nguvu kumlinda mtoto wa kiume dhidi ya ukatili mara baada ya ripoti mpya ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kubaini kuongezeka kwa matukio hayo nchini.
Ripoti hiyo ya haki za binadamu kwa mwaka 2023 iliyotolewa hivi karibuni na LHRC inabainisha kuwa matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kiume yaliyoripotiwa ni pamoja na ulawiti, unyanyasaji wa kihisia na kisaikolojia, mauaji, adhabu kali mashuleni kutoka kwa walimu, kuunguzwa viungo vya mwili,ukatili wa kiuchumi, biashara ya uuzwaji wa watoto pamoja na kufanyishwa kazi ngumu.
Katika kipindi hicho matukio 1,038 yalirikodiwa katika mikoa 11 kati ya 20 ukilinganisha na matukio 460 yaliyoripotiwa katika maeneo hayo mwaka 2022.
Hiyo ni sawa na kusema matukio hayo yameongezeka zaidi ya mara mbili kwa asilimia 125 hali inayoweza kuwa tishio kwa watoto wa kiume nchini.
Hali ni mbaya zaidi kwa matukio ya ulawiti yalioongezeka kwa asilimia nane kutoka asilimia 79 iliyorekodiwa mwaka 2022 hadi matukio 87 mwaka 2023 huku wahusika wakuu wakiwa ni watu wa karibu kama baba, walezi, walimu, madereva bodaboda na majirani.
Matukio haya yameripotiwa zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Kagera, Tabora, na mikoa mingine kama Rukwa, ambapo baadhi ya wanawake wamebainika kuwashawishi watoto wa kiume kwa mahusiano ya kingono.
Ana Henga Mkurugenzi wa LHRC aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo amesema kuwa jamii imejisahau katika suala la malezi kwa mtoto wa kiume badala yake imewekeza nguvu zaidi kwa mtoto wa kike bila kujua watoto wa kiume kwa sasa ndio wenye uhitaji zaidi.
“Tunavyofanya kampeni za watoto tuingie kwa watoto wa kiume kwa sababu watoto wa kiume ndio wameonekana ni wahanga na tumewaacha sasa hivi tumekimbilia sana kwa mtoto wa kike tumesahau watoto wa kiume…lakini pia mifumo ukizaa mtoto wa kiume unaambiwa umezaa jembe,” ameelezea Henga.
Miongoni mwa sababu zinazopelekea ukatili huo kwa mujibu LHRC ni pamoja na wazazi kuruhusu watoto kulala pamoja na ndugu au wageni wanaowatembelea, ufisadi, watoto kushuhudia matendo ya kijinsia ya wanayofanya wazazi, makosa ya kitaalamu katika uchunguzi wa kesi na ukaribu wa shule.
“Tulipokea kesi ya wavulana wakinyanyasiana na tukagundua kuwa wazazi wanaolala katika chumba kimoja na wavulana ilikuwa sababu muhimu,” imesema ripoti hiyo.
Aidha, LHRC imetoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa ili kulinda haki za watoto wa kiume, na kuelimisha jamii juu ya madhara ya unyanyasaji wa kijinsia, huku ikihimiza Serikali na taasisi husika kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo hivi vya kikatili.