Rais Samia ataka udhibiti zaidi madini ya Tanzanite
- Aitaka wizara ya madini kukaa na wawekezaji kujadiliana njia nzuri ya kutengeneza mfumo huo wa kiudhibiti.
Mwanza. Rais Samia Suluhu ameigiza wizara ya madini nchini Tanzania kuanzisha mchakato wa kuboresha nembo (rebranding) madini ya Tanzanite na kuimarisha mfumo wa kudhibiti uuzaji wa madini hayo ulimwenguni ili kutunza thamani na kulifaidisha zaidi taifa.
Katika hotuba yake wakati akizindua mtambo wa kusafisha dhahabu jijini Mwanza, June 13, Rais Samia amesema miongoni mwa maeneo ya kuyaboresha kwa sasa ni katika madini hayo yanayochimbwa Mirerani mkoani Manyara kwa kuwa ndiyo rasilimali pekee ambayo inapatikana Tanzania tu ulimwenguni.
Kiwanda hicho cha kusafisha dhahabu kina uwezo wa kuzalisha kilo 480 kwa siku na iwapo kitaongezwa uwezo kinaweza kufikia hadi kilo 960 kwa siku.
“Kama tunavyojua kwamba Tanzanite, Mungu aliipendelea Tanzania…lakini tunavyokwenda sasa ni kama madini yanayochimbwa dunia nzima. Ukienda kwa majirani zetu kuna Tanzanite nyingi, bara la Asia kuna Tanzanite nyingi, kotekote kuna Tanzanite nyingi tu…imesambaa duniani,” amesema Rais Samia.
Rais Samia Suluhu Hassan akizindua kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metal Refinery chenye thamani ya Sh12.2 bilioni. Picha|Mariam John.
Amesema madini yote siku zijazo yatamalizika ikiwemo Tanzanite hivyo yapaswa kuwa na mfumo bora wa kuyadhibiti na kunufaisha Tanzania.
Hii ni moja ya maagizo ya mwanzo ya kiongozi huyo katika udhibiti wa madini nchini tangu aingie madarakani Machi 19 mwaka huu baada ya kifo cha mtangulizi wake Dk John Magufuli aliyefariki kwa maradhi ya moyo Machi 17 jijini Dar es Salaam.
“Tanzanite yetu itakwenda kumalizika. Inavyotumiwa na kuuzwa sasa haiendi vizuri. Kuna haja ya kukaa ‘kuirebrand’ (kuiboresha nembo) Tanzanite yetu, kuipa jina litakalotoa umuhimu, litaloipa utukufu, jina litakaloipa upekee Tanzanite yetu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kuna haja ya kuwa na mfumo wa kudhibiti madini hayo ili Tanzanite yote inayochimbwa nchini inunuliwe chini ya mwamvuli mmoja wa mashirika yanayonunua Tanzanite.
“Tanzanite yote iliyopo mikononi imilikiwe na mwamvuli huu. Mwamvuli huu ujipange jinsi ya kuuza Tanzanite yetu kwa uchache kwa bei kubwa kwa jina zuri la Tanzanite yetu na Tanzania yenyewe ipate jina na ifaidike na Tanzanite yetu,” amesema.
Kufanikisha mapendekezo hayo, kiongozi huyo wa juu wa nchi amememwagiza Waziri wa Madini Dotto Biteko kukaa na wawekezaji katika eneo hio ili wapendekeze mfumo mzuri utakaoweza kuyalinda madini hayo ya vito.
Ndani ya miaka minne iliyopita, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite ikiwemo kujenga ukuta katika migodi ya madini ya Mirerani iliyopo mkoani Manyara, Kaskazini mwa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Wizara ya madini kuweka nguvu kwa wachimbaji wadogo kwa kuwapatia vifaa ili wasaidiwa katika kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta hiyo.
Nyongeza na Nuzulack Dausen (Dar es Salaam).
Latest
