Mipango miji: Silaha kutokomeza migogoro ya ardhi, umaskini
- Serikali yaagiza mipango hiyo itekelezwe katika halmashauri zote.
- Italeta tija kwa watu na kupunguza ujenzi wa makazi holela.
Mwanza. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameziagiza halmashauri zote nchini kuwa na mipango ya kuendeleza miji na majiji itakayosaidia kupunguza migogoro ya ardhi na kukuza uchumi kwenye maeneo yao.
Mipango hiyo kabambe italeta tija kwa watu na kupunguza ujenzi wa makazi holela.
Waziri Lukuvi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango kabambe wa makazi jijini Mwanza Desemba 22, 2021 amesema halmashauri zinapaswa kufikiria namna ya kutekeleza malengo ya kupanga miji ili iwe kivutio cha utalii na kuongeza fursa za ajira.
Kuhusu uzinduzi wa mpango kabambe wa makazi jijini Mwanza, Waziri Lukuvi ameziagiza halmashauri za jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kuhakikisha zinatekeleza mpango huo na usibakie kwenye makaratasi.
“Mpango huu umeanza toka mwaka 2014 na utasaidia katika kuboresha makazi na sekta mbalimbali za kiuchumi, rai yangu kwenu ni kuhakikisha unaanza kutekelezwa mara moja na kukamilika ifikapo mwaka 2025,” amesema Waziri Lukuvi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezindua wa mpango kabambe wa makazi jijini Mwanza Desemba 22, 2021. Picha| Mariam John.
Kuanza kutekelezwa kwa mpango huo kutachochea fursa mbalimbali za kiuchumi kwa maendeleo endelevu na utasaidia kuondokana na migogoro ya ardhi na ujenzi wa makazi holela katika mkoa huo.
Pia kila mtu anayetaka kujenga jijini Mwanza ametakiwa kufuata sheria ya mpango kabambe ili kuepuka migogoro hapo baadaye.
Mwanza ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi na ni kitovu cha shughuli za biashara katika ukanda wa maziwa makuu ambalo lina fursa nyingi za uwekezaji kulingana na jiografia yake ilivyo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratias Kalimenze amesema kwa jiji la Mwanza mpango huo ni watatu wa uendelezaji wa mji ambapo mpango wa kwanza ulikuwa mwaka 1974, wa pili 1992 na watatu 2015 hadi 2035 ambapo zoezi hilo mchakato wake ulianza 2014 kwa Serikali kutoa maelekezo ya mpango kabambe uandaliwe katika Jiji la Mwanza na Arusha
Soma zaidi:
- Mgogoro wa ardhi unavyosababisha wanafunzi 200 wabanane darasa moja Mbeya
- Kigoma kinara usajili mashamba Tanzania bara
Lengo mahususi la kuandaliwa mpango huo ni kuhakikisha wanakuwa na maendeleo endelevu kwa lengo la kuweka utaratibu na kuwezesha mpangilio mzuri wa mji na afya za wakazi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel amesema jiji hilo limebahatika kuwa na fursa nyingi na kuwa kituo cha biashara kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.
Pia jiji hilo limekaa kimkakati hivyo kuvutia kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika shughuli za usafiri viwanda na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na utalii.
Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mosses Seleki, amesema malengo ya mpango kabambe huo ifikapo mwaka 2035 kuwe na jiji lililochngamka lenye kufikika ambapo asilimia 70 za safari ziweze kufanywa na usafiri wa umma.
Kuwa na jiji lenye ufanisi stahimilivu na ufanisi ambapo hata mvua ikiwa inanyesha watu waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kuwe na ajira milioni 1.5 kutoka kwenye kilimo, biashara na viwanda.
Latest
