Sababu za wazazi kuwaongoza watoto kusoma vitabu

November 28, 2018 7:39 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Usomaji wa vitabu unamfanya mtoto kuwa mbunifu na kupata maarifa mengi yatakayomsaidia kuweza kufika mbali kimaendeleo.
  • Anzisha mfumo wa kusimuliana na mtoto stori kupitia kitabu alichosoma, hii itamjengea uwezo wa kusimulia jambo na kuweka kumbukumbu.

Dar es Salaam. Katika zama hizi za sayansi na teknolojia usomaji wa vitabu hasa kwa nchi zinazoendelea bado umekuwa mdogo ukilinganisha na zile zilizoendelea. 

Lakini kupitia kusoma vitabu ndipo  kizazi chenye uwezo mzuri wa kupambanua mambo na kuyaelezea kwa undani kinapopatikana.

Swali la kujiuliza ni kwa kiasi gani wazazi au walezi wanatoa kipaumbele cha kusoma vitabu kwa watoto na hapa hatuzungumzii vitabu vya darasani au vya kiada, tunazungumzia vitabu vya ziada ukiondoa vile vya kujifunzia katika masomo ya kawaida.

Wazazi wanajukumu la kuwajenga watoto wao tangu wakiwa wadogo utamaduni wa kusoma vitabu ili  kuelewa mambo yaliyojificha na kukuza uwezo wao wa kufikiri na kuelimika zaidi kwenye masuala mbalimbali ya kijamii,kisiasa na kiuchumi.

Mzazi anatakiwa achague vitabu vinavyoendana na umri wa mtoto wake katika duka la vitabu lililo karibu nae, na baadhi ya wauzaji vitabu huwa wanatembeza mkononi na kupitisha kwenye foleni za magari na hata katika migahawa au baa.

Mzazi anaweza akaletewa kitabu hakiangalii na utasikia tu anamwambia muuzaji ‘asante’, labda angekisoma kabla hajakataa angeweza kumnunulia mtoto kitabu kizuri, hii inaonyesha dhahiri kuwa bado wazazi wengi pia hawana utamaduni wa kusoma.

kama mzazi hauna utamaduni wa kusoma usimfanye na mtoto wako apitie ulipopita wewe msaidie aweze kupenda kusoma vitabu.

Unaweza kuanza kwa kumsomea kitabu kimoja cha hadithi kila jioni kabla hajaenda kulala,ukifululiza kwa miezi mitatu, mtoto ataanza kuzoea hali hiyo  na atajenga tabia ya kusoma mwenyewe bila ya kusurutishwa na mtu yeyote.

Pia anzisha utaratibu wa kusimuliana na mtoto stori kupitia kitabu alichosoma, hii itamjengea mwanao uwezo wa kusimulia jambo na kuweka kumbukumbu ambayo inaweza pia kumsaidia katika masomo yake ya darasani.

Utamaduni wa kusoma vitabu unamfanya mtoto awe na uwezo wa kujiamini na kuwa mdadisi katika jamii. Picha| Blavity.com 

Kusoma vitabu kutamsaidia mtoto kusafiri sehemu mbalimbali akiwa sehemu moja. Hii ni kwasababu anaposoma kitabu anakuwa yupo katika hali ya kuumba matukio yaliyopo kwenye kitabu, kutembea na mhusika katika kitabu, kuweza kufikiria anapoenda na kujifunza vingi kupitia wahusika.

Kwa mujibu wa mtandao wa Rusevec wa nchini Slovenia wanasayansi wameweka wazi kuwa mtoto anayesoma vitabu katika mazingira mazuri na akawa anajisikia utulivu wa kihisia basi kuna uwezekano mkubwa wa kupenda kusoma vitabu zaidi.

Mtoto apata misamiati mbalimbali ya lugha na hapa unashauriwa kumpa vitabu vya kiswahili na kiingereza aweze kujifunza zaidi na hata kujua maneno mapya kwa kutumia vitabu.

Jarida la ScienceDaily la nchini Marekani linaeleza kuwa kusoma na mtoto wako tangu akiwa mchanga, kuna mjengea uwezo wa kuchangia aweze kufahamu misamiati vizuri na kuongea lugha iliyonyooka kabla hata ya kuanza shule.

Usomaji wa vitabu unamfanya mtoto kuwa mbunifu na kupata maarifa mengi yatakayomsaidia kuweza kufika mbali kimaendeleo.  


Zinazohusiana: Twaweza: Wazazi wengi hawajui matokeo halisi ya shule za watoto wao

                            Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufaulu vizuri


Ni wajibu wa mzazi kumuandaa mtoto wake na kumuwekea utamaduni wa kupenda vitabu ili unufaike katika maisha yake yote. 

Hapa Tanzania wadau mbalimbali kama Soma Book Cafe, Read International, Children Book Project (CBP), Room 2 Read wameanzisha vituo kwa ajili ya watoto kusoma na kujifunza, na hata kuanzisha miradi ya kutengeneza maktaba katika shule za msingi na sekondari pamoja.

Pia mashindano mbalimbali ya uandishi na usomaji wa vitabu ikiwa ni mchango wao wa kuinua muamko kwa watu kuandika na kusoma vitabu.

Hata Rais John Magufuli wakati akizindua maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Novemba 27 mwaka huu aliwasisitiza wazazi kuwasaidia watoto wanapenda vitabu kwa kuwajengea miundombinu rafiki kujifunzia.

“Tuhakikishe tunawajengea watoto wetu kuwa na utamaduni wa kusoma,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Enable Notifications OK No thanks