Magufuli atoa maagizo mazito uvunaji mamba, viboko
- Asema wanatakiwa kuvunwa kisayansi ili wasimalizwe wote.
- Awataka wananchi wasiwafuate kwenye maziwa na mito.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia namna nzuri ya kuvuna mamba na viboko kwa njia ya kisayansi na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya mito na maziwa ili kupunguza vifo, uharibifu wa mazao na makazi.
Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Oktoba 7, 2019) mkoani Rukwa, amesema wizara ihusike katika kupanga mikakati ni kwa namna gani wanaweza kuanza mipango ya kuwavuna mamba na viboko na kuwatumia kama vitoweo ili kuwapunguza katika vyanzo vya maji.
“Hawa wanyama tuliopewa na Mungu ni lazima watusaidie katika kujenga uchumi wetu lakini pia wasimalizwe ni lazima uvunaji (wa mamba na viboko) uwe wa kisayansi kwa manufaa ya wote,” amesema Magufuli.
Pamoja na hayo, Rais ameutaka uongozi wa Mkoa wa Rukwa na wizara inayohusika na wanyama pori waelemishwe na wajue madhara ya kusogea kwenye mito na maziwa hasa ziwa Rukwa.
“Kwa hiyo ni lazima wote tujipange katika kushare (kutumia pamoja) ardhi tuliyopewa na Mungu. Wananchi wasisogee sana kujenga makazi yao na kulima mazao kando kando ya Ziwa Rukwa, ambavyo kwa vyovyote viboko watakuja kuyala,” amesema Rais.
Soma zaidi:
- Tanzania yaangalia uwezekano wa kuwavuna mambo kuokoa maisha ya raia
- Tanzania kupiga mnada asilimia 10 ya mamba kuokoa maisha ya raia.
- Hifadhi ya Katavi; mahali unapoweza kushuhudia mapigano ya viboko na mamba.
Agosti 17, 2019, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alisema Serikali itauza asilimia 10 ya mamba wote nchini ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ongezeko la wanyama wakali na wanaovamia maeneo ya watu na kufanya uharibifu ikiwemo kusababisha vifo.
Aidha, Kigwangalla alisema watauza viboko wote waliopo kwenye maeneo yenye maji kama maziwa, mabwawa na mito iliyopo mjini ukiwemo mji wa Mpanda mkoani Katavi, Mafia (Pwani) na Babati (Manyara).
Latest
