Haya ndiyo makosa yanayowamaliza vijana wengi wakati wa kuomba kazi

January 29, 2020 5:29 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya makosa hayo ni matumizi yasiyo sahihi ya barua pepe na kukosa umakini wakati kutuma maombi ya kazi.
  • Makosa mengine ni kukosa kujua vizuri kampuni na nafasi anayoombea kazi.
  • Waajiri wasema vijana wanatakiwa kujielimisha zaidi ili kuwa na ujuzi wa kuomba kazi.

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa vijana ambao wamekuwa wakisaka fursa za ajira kwa muda mrefu bila mafanikio, bado una kila sababu ya kutabasamu tumaini bado lipo la kupata kazi ya ndoto yako. 

Unahitaji kufahamu baadhi ya mambo unayopaswa kuzingatia wakati wa kutuma maombi ya kazi ili ufanikiwe kuitwa kwenye mahojiano (Interview) na kisha kuipata kazi ya ndoto yako. 

Miongoni mwa mambo hayo ni kuepuka kuafanya baadhi ya makosa ikiwemo kutokufuata maelekezo uliyopewa,  ambayo yamekuwa yakijirudia kwa waombaji wengi na kuwakosesha fursa ya kazi. 

Nukta (www.nukta.co.tz) inakuletea makosa yanayojitokeza mara kwa mara na  katika uombaji wa kazi ambayo ukiyaepuka unaweza kupata kazi unayotarajia:


Matumizi yasiyo sahihi ya barua pepe

Kutokana na ukuaji wa teknolojia, waajiri wengi hutumia njia ya mtandao kutangaza nafasi za kazi na kuwataka waombaji kutuma maombi yao kwa njia ya barua pepe. 

Hata hivyo, baadhi ya waombaji wanashindwa kuzingatia mambo ya msingi wakati wa kutuma maombi kwa njia hii, jambo ambalo linawafanya waonekane hawako makini. 

Baadhi yao wanashindwa kupanga taarifa zinazohitajika kwa usahihi kama kuweka viambatanishi vinavyohitajika, utangulizi wa barua, makosa ya kiuandishi na herufi na kutumia lugha isiyo rasmi.

Afisa Rasilimali Watu wa kampuni ya Buzwagi Gold Mine, Emmanuel Venus anasema kabla mtu hajatuma maombi ya kazi, anatakiwa kujua matumizi sahihi ya barua pepe ili kujiwekea nafasi kubwa ya kupenya katika kinyang’nyiro cha kupata kazi.

“Moja ya vitu tunavyoangalia ni uwezo wa kutumia vizuri barua pepe. Kama mtu hawezi kutumia barua pepe atawezaje kuendesha shughuli za kiofisi atakapopewa kazi,” anasema Venus.

Waombaji wanashindwa kuzingatia mambo ya msingi wakati wa kutuma maombi kwa njia hii, jambo ambalo linawafanya waonekane hawako makini. Picha | Mtandao.

Kutokuifahamu vizuri kampuni na nafasi unayoombea kazi

Hili ni kosa la kwanza linalowasumbua  waombaji wengi kwa sababu  katika uombaji wa kazi mtu anawasilisha taarifa bila kujua undani wa kazi na kampuni anayoombea kazi au nafasi anayoitaka katika kampuni husika. 

Mara nyingi tatizo hili husababisha watu kutuma taarifa zisizoendana na nafasi zilizotangazwa na waajiri.

Mfano kampuni ya masuala ya mawasiliano inaweza kutuma nafasi za kazi zinazohitaji wanasheria au maafisa masoko. Mwombaji mwenye taaluma ya mawasiliano anatuma maombi wakati hana ujuzi wa kazi zilizotangazwa. 

Huyu lazima maombi yake yatawekwa pembeni, labda awe na ujuzi wa ziada utakamuwezesha kutimiza majukumu atakayopewa. Hakikisha kazi unayoomba inalingana na ujuzi ulionao ili kuepuka usumbufu wa maombi yako kuwekwa kapuni. 


Zinazohusiana:


Kukosa umakini 

Moja ya vitu muhimu vinavyotakiwa kuzingatiwa wakati wa kuomba na kutuma maombi ya kazi katika kampuni husika ni umakini katika kutuma taarifa zako kwa usahihi. 

Hii ina maana kwamba pindi mtu anapotuma maombi yenye makosa mengi inamwonesha mwajiri kuwa kiwango cha umakini wa mwombaji ni kidogo hivyo inaweza kuwa sababu ya kukukosesha nafasi unayoomba.

Umakini unahusisha kufanya makosa madogo yanayoweza kupoteza umahiri wako kwa mwajiri. Makosa haya yanahusisha matumizi yasiyo sahihi ya  herufi kubwa na ndogo, kutokuandika kwa usahihi maneno kama inavyohitajika na upangaji wa taarifa kwa usahihi unaohitajika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Angle Informatics Limited, Mkono Shadrack,  amesema makosa mengi yanayosababisha mtu kushindwa kuitwa kwa ajili ya mahojiano (Interveiw) ni madogo madogo, hivyo wahusika wanataki  wa kujitahidi kuzingatia ufasaha katika utumaji maombi.

“Mara nyingi kinachosababisha mtu asiitwe kwenye interview ni makosa madogo sana. Waombaji wakiwa makini kupita kwenye mchujo ni rahisi sana,” anasema Shadrack.


Kutokufuata maelekezo yaliyotolewa

Maelekezo ni moja ya vitu muhimu vinavyoweza kukupa sifa za kupenya kwenye mchuano katika uombaji kazi. 

Waombaji wengi hukosa sifa ya kuchaguliwa kuitwa kwenye mahojiano kwa sababu ya kushindwa kufuata maelekezo yaliyotolewa ya namna ya kuwasilisha au mtindo unaokubalika kuwasilisha maombi ya kazi kwa kampuni husika.

“Waombaji wanapaswa kuwa makini wakati wanatuma maombi. Tukiona umekosa umakini kwenye kitu kidogo hatuwezi kuendelea kushughulika na maombi yako huku tuna maombi mengi ya kupitia,” anasema Venus. 

Moja ya vitu muhimu vinavyotakiwa kuzingatiwa wakati wa kuomba na kutuma maombi ya kazi katika kampuni husika ni umakini katika kutuma taarifa zako kwa usahihi. Picha|Headway/Unsplash.

Kuweka taarifa nyingi kwenye barua ya maombi na wasifu (CV)

Kwa mujibu wa tovuti ya The balance carriers, mkusanyiko wa taarifa nyingi zisizo na maana kwenye barua ya maombi ya kazi na wasifu kunaweza kukosesha kupata kazi. 

Siyo wingi wa maneno au maelezo ndiyo kunamvutia mwajiri bali uwezo wako wa kujieleza kwa ufupi na kuweka mambo ya msingi yanayohitajika, ndiyo turufu yako ya kupenya kwenye kazi. 

Mwajiri anategemea kusikia zaidi kile mwombaji anachoweza kuifanyia kampuni ili ikue na kutimiza malengo yaliyowekwa. Pia inatarajia kuona taarifa ulizowasilisha zinashabiana na ujuzi ulionao na siyo taarifa binafsi za mwombaji wa kazi.

Hata hivyo, vijana bado wana nafasi nzuri ya kurekebisha makosa hayo kwa kujifunza na kupata maarifa zaidi kutoka mtandaoni au kwa watu wenye uzoefu namna ya kuepuka makosa magodo madogo wakati wanaomba kazi. 

Pia wanakumbushwa kuhakiki taarifa za maombi ya kazi kabla ya kutuma, ikibidi kuwapa marafiki au ndugu kupitia ili kuona kama ziko sahihi. Umakini na jinsi unavyopangilia maombi yako ya kazi kulingana na maelekezo uliyopewa ni hatua muhimu ya kukufanya ufanikiwe katika hatua zinazofuata za kupata kazi. 

Katika makala ya kesho tutaangazia kwa undani vitu vinavyowakwamisha waombaji wa kazi hasa vijana wanapokuwa katika mahojiano (interview) na mbinu zitakazowasaidia kutoboa katika ajira. 

Enable Notifications OK No thanks