5G ya Huawei yagonga mwamba Uingereza

July 16, 2020 8:36 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kupiga marufuku ya kampuni za mawasiliano nchini humo kutumia mitambo ya mtandao wa 5G iliyotengenezwa na Huawei.
  • Kampuni za mawasiliano zimepewa hadi mwaka 2027 kuhakikisha haimiliki mtambo wowote wa 5G uliotengenezwa na kampuni hiyo.
  • Hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa nchi ya Uingereza pamoja na uchumi wake.

Dar es Salaam. Kampuni zinazotoa huduma ya mawasiliano nchini Uingereza zimetakiwa kuondoa mitambo na mashine zote za 5G zilizotengenezwa na kampuni ya Huawei ya China ili kuimarisha usalama na kukuza uchumi wa nchi hiyo. 

Pia kampuni hizo zimepewa muda hadi mwaka 2027 kuhakikisha zimeondoa kila mashine za Huawei kwenye mitandao yake ya 5G nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kenyan Wallstreet, Uingereza imepiga marufuku  kampuni yoyote ya mawasiliano kununua mashine za kampuni ya Huawei baada ya Desemba 31, 2020. 

Waziri wa Uingereza mwenye dhamana ya masuala ya kidijitali, utamaduni, vyombo vya habari na michezo, Oliver Dowden hivi karibuni alisema kufanya maamuzi hayo haikuwa rahisi lakini ni maamuzi sahihi kwa ajili ya mitandao na uchumi wa nchi hiyo.

“Njia sahihi zaidi kulinda mitandao yetu ni kwa waendeshaji kuachana na matumizi ya vitu vipya vya Huawei visivyofaa kujenga mitandao ya Uingereza ya baadaye. Ili kuwa sawa, kuanzia mwisho wa mwaka huu, waendeshaji wa mitandao ya simu wasinunue mashine yeyote ya 5G kutoka Huawei,” Ameeleza Waziri Dowden.

Uingereza pia itapitisha muswada utakaokataza kampuni yoyote ya mawasilianno kununua kifaa cha 5G kutoka Huawei mwishoni mwa mwaka huu.


Zinazohusiana:


Hata hivyo, Huawei imeonya kuwa hatua iliyochukuliwa na nchi hiyo itapunguza kasi ya safari ya teknolojia ya 5G nchini humo na kuwa maamuzi hayo ni ya kisiasa na siyo ya kibiashara.

Baada ya Huawei kuondolewa Uingereza, baadhi ya kampuni za teknolojia ikiwemo Nokia na Ericsson zimeonyesha nia kufanya kazi na nchi hiyo ili kusimika mitambo ya 5G. 

Baadhi ya wachambuzi wamesema uamuzi wa Uingereza bado una mashaka kwa sababu kampuni hizo zinatumia vifaa vinavyotoka China. 

Nchi nyingine zilizoachana na teknolojia ya 5G ya Huawei ni pamoja na Marekani, Australia, New Zealand, Japan, Italia na Denmark.

Huenda idadi hiyo ikaongezeka hivi karibuni kwani Ujerumani, Canada, Ufaransa na India wapo njiani kufanya hivyo ili kuhakikisha usalama wa nchi zao. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW