Aina mbalimbali za mzio na madhara yake

September 11, 2021 8:36 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mzio ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote kisichokuwa na madhara kwenye mwili.
  • Vitu hivyo ni vumbi, poleni, vyakula na hata harufu kali.
  • Unaweza kuleta shida kwenye machoni, ngozi na mfumo wa hewa.

Dar es Salaam. Unaweza kushangazwa na vitu ambavyo watu wana mzio (allegy) navyo pale wakikuelezea. 

Wapo wenye mzio na vumbi, harufu kali na wengine mzio wao umeenda mbali na kuwakataza kuvalia madini ya thamani ikiwemo dhahabu.

Endapo wakivunja masharti, wanaovimba mwili, wanapata mafua makali na wapo wanaowashwa na kuvimba macho.

Matokeo ya mzio yanaweza kuathiri kwa muda mfupi sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo ngozi, macho, mfumo wa hewa na wengine kuharisha, tumbo kuuma na kichefuchefu.

Dk Fabian Mghanga kupitia tovuti ya masuala ya afya ya TanzMed ameelezea kuwa mzio ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote kisichokuwa na madhara kwenye mwili. 

Hali hiyo hutokea pale kitu hicho kimeingia ndani ya mwili au kugusa sehemu ya mwili.

“Haishangazi basi kuona kuna baadhi ya watu wanakuwa na mafua karibu kila siku au wengine wanashindwa kuvaa baadhi ya vitu kama saa au cheni za dhahabu kwa vile tu huvimba mwili au kuwashwa pindi wanapofanya hivyo,” ameandika Dk Mghanga.

Hata hivyo, siyo watu wote wanajua kuwa wana mzio na kitu fulani licha ya kuwatokea mara kwa mara. Mtaalamu huyo amesema zipo dalili za kuonyesha kuwa unaweza kuwa na mzio na kitu fulani bila kujua.

Baadhi ya watu, vumbi kidogo tu linaweza kumpatia mafua makali. Picha| Lightfield Studios.

Aina maarufu za mzio na sababu zake

Mzio unaotokea kwenye mfumo wa hewa

Mzio huu hutokana na mfumo wa hewa kufikiwa na kitu ambacho mtu anatakiwa kuchangamana nacho licha ya kuwa hakina madhara. Mfano, pale anapovuta hewa yenye harufu kali, mzio wake unaweza kuchochea matatizo kwenye upumuaji, mafua makali pamoja na muwasho kwenye pua na koo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Healthline, mzio huu unaweza kusababishwa na chembechembe zinazotokana na kujikuna kwa wanyama (mba), chakula ikiwemo siagi ya karanga na poleni kutoka kwenye maua na miti.


Mzio wa kwenye ngozi

Huu hutokea pale kinga ya mwili inapokutana na kitu inachopingana nacho na matokeo yake yakaonekana kwa njia ya ngozi. 

Zipo baadhi ngozi ambazo zikikutana tu na vumbi zinapata matokeo hasi ikiwemo mafua, kuvimba, kupata vipele na vijipu.

Tovuti ya Medical News Today imeandika kuwa mzio huo unaweza kusababishwa na kushika wanyama, kuvalia baadhi ya nguo zenye malighafi yasiyopatana na mwili wako, kushika kemikali na baadhi ya sabuni na vipodozi.

“Mizio ya chakula pia inaweza sababisha ngozi kuwasha,” imeandika Medial News Today.

zio wa macho unaweza kusababishwa na poleni au mba. Picha| Healthline.

Mzio wa machoni

Hali hii hutokea pale macho yanapovimba au kuwa na rangi nyekundu  baada ya mwili wako kuelekeza matokeo ya mzio kwenye macho.

Mtu mwenye hali hii anaweza kuhisi macho kuwaka ya moto, kutokwa na machozi bila sababu, kushindwa kuona vizuri na kuumia pale anapopitiwa na mwanga mkali.

Tovuti ya WebMd imeandika kuwa, hali hiyo inaweza kusababishwa na macho kuchangamana na poleni au mba kutoka kwa wanyama na hata watu. 

Ni muhimu kufahamu kuwa siyo sahihi kujiamulia tu kuwa una mzio fulani bila kauli hiyo kutoka kwa mtaalamu.

Inashuriwa, pale unapohisi kuna changamoto fulani inayokupata kutokana na kitu fuani, ni muhimu kuonana na mtaalamu wa afya ili athibitishe.

Makala zinazofuata zitaangazia kila aina ya mzio kwa undani ili uweze kuelewa zaidi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW