Athari za kiafya rangi zenye madini ya risasi
- Ni kwa kudhibiti matumizi ya rangi zenye madini zisizoruhusiwa.
- Elimu ya utambuzi wa rangi hizo nayo itasaidia.
- Rangi hizo huathiri ubongo, upungufu wa uwezo wa mtoto kuelewa, na mabadiliko ya tabia.
Dar es Salaam. Ili kupunguza athari za rangi zenye madini ya risasi kwa watu na mazingira, Serikali imeshauriwa kuongeza udhibiti wa uagizaji na matumizi ya rangi za majengo zisizo na viwango.
Risasi ni metali (madini) yenye sumu ambayo kiasili yanapatikana katika mazingira. Madini hayo hupatikana katika baadhi ya rangi za mafuta na katika vifaa vingine kama vile betri na vifaa ikiwemo midoli na samani.
Madini hayo huongezwa kwenye rangi za mafuta wakati wa uzalishaji. Zinakuwa ni sehemu ya viambata (vikaushaji (driers) na vikolezo (pigments)). Vikaushaji husaidia rangi kukauka haraka na kuonekana nzuri baada ya kupakwa kwenye jengo au sehemu yoyote ile. Pia vikolezo hivyo husaidia kuzuia kutu au kulika kwa vifaa vya chuma na bati.
Hata hivyo, watalaam wa masuala ya afya na mazingira, wanaeleza kuwa madini hayo yanayopatikana kwenye rangi za mafuta yana madhara kiafya hasa kwa watoto wadogo.
Afisa Programu Mkuu wa taasisi inayojihusisha na masuala ya mazingira ya AGENDA, Silvani Mng’anya amesema madhara ya madini ya risasi yanaweza kuwa makubwa na ya kudumu (yasiyoweza kutibika) hasa kwa watoto wadogo chini ya miaka sita.
“Kwa watoto, madini ya risasi yanaweza kuathiri ukuaji wa ubongo na kusababisha upungufu wa uwezo wa mtoto kuelewa, mabadiliko ya tabia kama vile mapungufu ya kuzingatia jambo, na ugumu wa kufikia malengo ya masomo,” amesema Mng’anya wakati akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).
Pia madini ya risasi yanasababisha upungufu wa damu, shinikizo la juu la damu, matatizo ya figo, ini, matatizo ya kinga ya mwili na matatizo katika via vya uzazi.

Madhara ya rangi zenye madini ya risasi ni makubwa lakini siyo rahisi kuonekana kwa mtu. Picha| Nichollaw.
Nini kifanyike?
Ili kudhibiti madhara hayo kwa wananchi wa Tanzania, wadau wa masuala ya mazingira wanashauri Serikali kuendelea kutoa elimu na kudhibiti uagizaji na matumizi ya rangi zenye madini ya risasi yenye kiwango kisichoruhusiwa.
Katibu Mtendaji wa AGENDA, Haji Rehani amesema uelewa wa jamii ni jambo la msingi ili kuhakikisha kuwa walaji wanaepuka kununua na kutumia rangi ambazo hazijakidhi kiwango cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
“Serikali na wadau wengine zikiwemo taasisi mbalimbali kama vile Ofisi ya Makamu wa Rais – Kitengo cha Mazingira zikishirikiana kupaza sauti na kuchukua hatua za kuacha kununua na kutumia rangi zenye madini ya risasi itasasidia Tanzania kuondokana na rangi zenye madini ya risasi,” amesema Rehani.
TBS ilishaweka kiwango cha madini ya risasi katika rangi tangu mwaka 2017 ambacho ni sehemu 90 kwa milioni (90 ppm) kinachotumika pia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hii ina maana kiasi cha madini ya risasi katika rangi zinazoingizwa, zinazozalishwa, zinazosambazwa, zinazouzwa na zinazotumika hapa Tanzania hakitakiwi kuzidi kiwango hicho.
Pia kuna haja ya kuhakikisha rangi zenye madini ya risasi zinaondolewa kabisa hapa Tanzania kwa kusimamia utekelezaji madhubuti wa hicho kiwango.
Tanzania ni kati ya asilimia 43 ya nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zenye udhibiti wa kisheria wa matumizi ya rangi zenye madini ya risasi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Walaji Tanzania (TCAS), Bernard Kihiyo amewataka Watanzania kukuza ushirikiano katika kuondoa rangi zenye madini ya risasi hapa nchini kwa kuacha kabisa kununua rangi ambazo hazijathibitishwa na TBS.
Wakati wa kununua rangi dukani, angalia kama kopo au ndoo ya rangi ina chapa ya TBS kuthibitisha kama imekidhi viwango vya ubora.

Rangi chakavu na zilizoanza kumenyeka ambazo zina madini ya risasi zinaweza kuababisha madhara hasa kwa watoto. Picha| Jowarsk Painting.
Madini ya risasi yanaingiaje mwilini?
Hufanyika kupitia rangi zilizoanza kumenyeka, kuchakaa na kuharibika hasa zilizopakwa kwenye kuta au vifaa ambapo huachia na kudondoka katika sakafu, vumbi au udongo.
Rangi yenye madini ya risasi huchanganyika na vumbi na hatimaye kusambaa kwenye mazingira husika.
Kwa mujibu wa WHO, watoto wapo katika hatari ya kuingiwa na madini ya risasi kutokana mazingira yanayowazunguka mfano ukuta au kifaa kilichopakwa rangi.
Iwapo vumbi au udongo umechafuliwa na madini ya risasi iliyomenyeka, watoto, humeza madini hayo kutokana na tabia ya watoto ya kuweka mikono kinywani.
Kwa wakubwa, rangi inaingia kwenye miili yao wakati wa kupiga msasa sehemu inayotakiwa kupakwa rangi, kula vyakula vilivyoingiwa (contaminated) na madini ya risasi.
Latest