Mtaalam: Punguzeni msongo wa mawazo kukishinda kisukari

November 14, 2022 10:46 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mmoja wa mwananchi akipata kipimo kutoka kwa mtoa huduma ya afya  katika maadhimisho ya siku ya ugonjwa wa kisukari duniani ambayo uadhimishwa kila mwaka ifikapo Novemba 14, ambapo  kitaifa yameadhimishwa mkoani Mwanza. Picha | Mariam John.


  • Watalaam wasema unachangia mtu kupata kisukari.
  • Pia kula mlo kamili, kuacha sigara na kufanya mazoezi kunaweza kusaidia. 

Mwanza. Watanzania wameshauriwa kuishi maisha kulingana na uwezo wao ili kuepuka msongo wa mawazo ambao unaweza kuchangia kupata ugonjwa wa kisukari. 

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa Kisukari duniani leo Novemba 14, 2022 jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Chama cha ugonjwa Kisukari Tanzania, Profesa Andrew Swai amesema uchunguzi wa awali wa umebaini kuwa chanzo cha ugonjwa wa kisukari huchangiwa na msongo wa mawazo.

Amewataka wananchi kuishi kulingana na vipato vyao na kuzingatia muda wa kupumzika kwa kuhakikisha wanapata usingizi wa kutosha ili mwili uweze kusawazisha palipoharibika.

“Pamoja na kuzingatia muda mwingi wa kupumzika lakini pia jamii iache matumizi ya kiwango cha juu cha sukari na chumvi na inashauriwa kwa siku mtu anapaswa kutumia vijiko vitano vya sukari na kijiko kimoja cha chumvi, ” amesema Profesa Swai. 

Mtaalam huyo wa masuala ya afya amesema jitihada zinahitajika kuzuia ugonjwa huo kwa mtu mmoja na taasisi. 

“Tunahitaji  kuzuia magonjwa haya kwani tiba yake  ni gharama kubwa lakini  tunaweza kuzuia kwa kufuata mtindo bora wa maisha, kula mlo kamili na kutoongeza sukari kwenye chakula na vinywaji,” amesema Profesa Swai.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni 19 katika bara la Afrika wana kisukari na idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni 47 mwaka 2025. 

WHO inashauri watu kuwa na uzito wa wastani, kufanya mazoezi, kuepuka uvutaji wa sigara na kula mlo kamili.

Kaimu Mkurugenzi wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, Valeria Millinga, amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari huchangia asilimia 33 ya vifo nchini hapa.

“Asilimia 9.1 ya Watanzania wana ugonjwa wa kisukari na katika nchi 10 barani Afrika kwa magonjwa ya kisukari Tanzania inashika nafasi ya 8 hivyo utaona kwa kiasi gani nchi yetu ilivyoathirika na ugonjwa huu,” amesema Millinga.

Katika maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo mwaka huu kitaifa yamefanyika mkoani Mwanza, wananchi 3,000 wameweza kupata huduma na kati yao 34 wamegundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa wa kisukari.

Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Bakari Salum, amesema wataendelea kusimamia halmashauri kwa kuhakikisha vituo vya afya vinatoa huduma ya upimaji wa ugonjwa wa kisukari kwa mujibu wa wananchi wananvyokuwa wanahitaji huduma ya afya.

“Hivi karibuni tutakuwa na mafunzo Mkoa wa Mwanza na Misungwi ikiwemo kwa watumishi wa afya ili baada ya mafunzo hayo kila kituo cha afya kitakachopata mafunzo haya kitatakiwa kianzishe kliniki ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na sisi kama Tamisemi tutalisimamia hilo,” ameeleza Dk Salum.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW