Taka za kielektroniki zinavyotafuna mazingira ya Tanzania
- Matumizi ya vifaa vya kielektroniki yachangia ongezeko ya taka hizo.
- Zachangia katika uharibifu wa mazingira na afya ya binadamu.
- Mifumo ya kisasa ya udhibiti wa taka hizo na sheria itasaidia kuokoa mazingira.
Dar es Salaam. Ni asubuhi ya saa nne na nusu, baada ya kufungua duka lake lililopo Mtaa wa Donga, Kijitonyama, Dar es Salaam, fundi wa vifaa vya kielektroniki anatengeneza kiraka cha plastiki kwa ajili ya kukiweka kwenye runinga aliyoitengeneza.
Kwa kutumia kisu, anapunguza sehemu ya kiraka hicho alichokata kutoka kwenye runinga iliyoharibika na kisha kupima kama kinatosha kuwekwa katika runinga anayoitengeneza.
Mbali na runinga, katika duka lake vipo vifaa vya umeme yakiwemo majagi ya kuchemshia maji, redio na feni.
“Kwa vitu ambavyo siwezi kuvitumia kabisa, navikusanya na kuviweka kwenye kiroba na gari la taka huvipitia. Kwa mwezi nalipia Sh5,000 huduma hiyo,” anaeleza fundi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Fundi huyo ni miongoni mwa Watanzania wengi ambao wanahifadhi na kutupa vifaa vya kielektroniki vilivyoisha matumizi na hivyo kuchangia uharibifu wa mazingira na afya ya binadamu bila wao kujua.
Fundi huyo anasema hakuna mifumo mizuri ya kutupa taka za kielektroniki nchini Tanzania kama ilivyo kwenye nchi zilizoendelea hivyo suluhu kubwa iliyopo ni kuzitupa kama taka nyingine.
Taka za elektroniki (E-Waste) ni jina la bidhaa za kielektroniki ambazo zimefikia mwisho wa matumizi. Hii inajumuisha kompyuta, vidhibiti, runinga, stereo, vinakili, vichapishaji, mashine za faksi, simu za rununu, kicheza dvd, kamera, betri, blenda na vifaa vingi vinavyotumia nishati ya umeme.
Vifaa vya kielektroniki vilivyotumika vinaweza kutumika tena, kuuzwa tena, kuokolewa, kuchakatwa tena au kutupwa.
Taka za kielektroniki na mabaki ya vitu vyote ambavyo hutumia umeme kujiendesha. Ni pamoja na simu, kompyuta majokofu na feni. Picha| Rodgers George.
Ripoti ya Taifa ya masuala taka za kielektroniki Tanzania Bara ya mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa, mwaka 2007, Tanzania ilizalisha jumla ya taka za kielektroniki tani 12,500.
Miaka 10 baadaye taka hizo ziliongezeka mara mbili zaidi ya zilizokuwepo mwaka 2007.
Ripoti hiyo inaeleza hadi kufikia 2017, uzalishaji wa taka hizo uliongezeka kwa asilimia 65 na kufikia tani 35,800.
Kwa mujibu wa ripoti ya taarifa kwa umma kuhusu kanuni za udhibiti na usimamizi wa taka hatarishi za mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ongezeko la taka za kielektroniki linachochewa na kuongezeko kwa matumizi ya bidhaa za kielektroniki hasa simu, kompyuta, runinga na redio.
Tatizo la taka za kielektroniki siyo la Tanzania peke yake, pia linaisumbua dunia kwa sasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikichochea athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP), kila mwaka tani milioni 50 za taka za kielektroniki huzalishwa duniani zikiwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 62 sawa na Sh142.4 trilioni.
Hata hivyo, ni asilimia 20 tu ya taka hizo za kielektroniki ndiyo hurejelezwa (recycling) katika mazingira rasmi ili kupata bidhaa mpya.
Soma zaidi:
- Teknolojia inavyotumika kuokoa mazingira
- Teknolojia ya kutengeneza matofali kwa taka za plastiki yaingia sokoni
- Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi – 3
Athari kwa mazingira na binadamu
Uzalishaji wa taka za kielektroniki zimekuwa na athari kubwa za kimazingira hasa katika maeneo ambayo hayana teknolojia ya urejelezaji.
Athari zake hujitokeza zaidi kwenye udongo kwa sababu hutoa kemikali ya metali nzito yenye sumu. Kemikali hizo hujumuisha madini kama risasi ambapo zinapoingia kwenye udongo, huathiri ukuaji mimea.
Hali hiyo inaweza kupunguza uzalishaji wa mazao ya wakulima ambao wamewekeza nguvu zao kwenye kilimo.
Taka za kielektroniki haziishii tu kwenye kuchafua mazingira. Pia zinaathiri afya za watu ambao wanafikiwa nazo.
Daktari kutoka Zahanati ya Sarib iliyopo Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Dk Ambilikile Malango anasema athari za taka za kielektroniki ikiwemo mabaki ya televisheni na kompyuta huambatana na madini ya shaba, zebaki na risasi, malighafi ambayo ni sumu yakikutana na mwanadamu.
Mtaalamu huyo wa masuala ya afya anasema, madini hayo yanapotupwa bila mpangilio mzuri yana madhara kwenye mapafu, figo, ini na hata mifupa.
“Kuna baadhi ya vifaa ikiwemo skrini za televisheni, kama hazitotupwa vizuri zinachangia uharibifu wa mifumo ya neva. Unakuta sehemu zenye kemikali za kadiamu au zebaki zimetupwa vibaya, mtoto akilamba zile lazima apate shida,” anasema Dk Malango.
Mtaalamu huyo wa afya anasema kutokuzitupa taka hizo vizuri kunasababisha sumu hizo ziingie kwenye mifumo ya maji hasa wakati wa mvua na hivyo kusababisha madhara kwa afya ya binadamu.
Ongezeko la taka za kielektroniki Tanzania linac hochewa na matumizi ya bidhaa za kielektroniki ambazo ni “mtumba”. Picha| ScrapWare.
Mambo yanayochangia ongezeko la taka za kielektroniki
Wadau mazingira wanasema ongezeko la taka hizo kwenye mazingira ni ni matokeo ya kuongezeka kwa matumizi ya vifaa vya kielektroniki hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Mdau wa mazingira na mshauri wa masuala ya maendeleo, Mbazi Marisa ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, nchi zilizoendelea tayari zina mifumo ya kupambana na taka za kielektroniki ikiwemo kuuza bidhaa zilizotumika katika nchi zinazoendelea.
“Bidhaa zilizotumika huletwa Afrika kwenye majiji makubwa kama Dar es Salaam, Accra, Lagos kwani kuna mzunguko mkubwa wa pesa. Watu hununua bidhaa hizo huku zikiwa ni fursa pia kwa vijana wafanyabiashara,” anasema Marisa.
Mdau huyo wa mazingira anasema jambo hilo linasababisha huchangia uchafuzi wa mazingira kwa sababu hakuna udhibiti wa kutosha wa uagizaji wa bidhaa za kielektroniki kutoka nje ya nchi.
Licha ya Tanzania kupiga hatua katika masuala ya urejerezaji wa taka ikiwemo za karatasi na plastiki, haina sheria mahususi ya kusimamia taka za kielektroni zaidi ya kuwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004,ambayo inasimamia na kuratibu masuala yote yanayohusu mazingira ikiwemo udhibiti wa taka za kielektroniki.
Mshauri wa masuala ya mazingira, Caroline Manyama ameiambia Nukta Habari kuwa, nchi zilizoendelea zina mifumo mizuri ya kurejeleza taka za kielektroniki ikiwemo kuzirejesha kiwandani bidhaa ya zilizotumika.
Licha ya baadhi ya mifumo hiyo kutumika Tanzania bado haijafikia bidhaa zote kwani inayojulikana zaidi ni kurejesha baadhi ya simu tu hasa za iPhone na Samsung.
“Kwa wenzetu simu mpya ikitoka, unarudisha ya zamani kiwandani, unaongezea fedha kidogo unapatiwa mpya, huku kwetu bado,” anasema Manyama.
Mdau huyo amesema hilo linasababisha bidhaa nyingi kuendelea kurundikana kwani hakuna mifumo ya kuzirudisha kwenye matumizi mengine ikiwemo kutengeneza bidhaa mpya.
Ukosefu wa elimu udhibiti wa taka, ni sababu nyingine inayochangia watupa taka hovyo katika mazingira yanayowazunguka.

Mambo ya kuzingatia
Ili kuondokana na adha za taka za kielektroniki kiafya na kimazingira, hatua za pamoja zinahitajika kati ya Serikali, wadau wa mazingira na jamii.
Kwa mujibu wa fundi Raphael, anasema elimu itolewe zaidi sambamba na kubuni mifumo ya kisasa ya urejelezaji wa taka za elektroniki katika maeneo yote yenye matumizi ya vifaa vya kielektroniki.
“Kuna baadhi ya vitu kama plastiki ngumu zenye rangi ambazo haziwezi kurejelewa nchini. Mifumo mizuri ya kuzirudisha viwandani huenda ikasaidia kupunguza taka hizo,” anasema Raphael.
Ripoti ya Ufuatiliaji wa taka za kielektroniki Duniani ya mwaka 2020 iliyotolewa na Programu ya Umoja wa Taifa ya Mazingira (UNEP) inaeleza kuwa ikiwa kutakuwa na mifumo mizuri ya ukusanyaji na urejelezaji wa taka za kielektroniki siyo tu tutaokoa mazingira lakini itakuwa ni chanzo cha ajira kwa vijana wengi duniani.
Wadau wa mazingira wameshauri Serikali kuharakisha mchakato wa kutunga sheria mahususi inayosimamia taka za kielektroniki ili kuongeza uwajibikaji katika eneo hilo.
Hata hivyo, Seriali imeendelea na mchakato wa kuandaa kanuni za udhibiti wa kata za kielektroniki ili kupunguza ongezeko la taka hizo nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo katika Hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2021/22 ilisema Serikali imetenga Sh200 milioni kwa ajili ya kupambana na changamoto za mazingira ikiwemo taka za kielektroniki.
Pia wizara hiyo imekamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira (1997) na kuandaa Rasimu ya Sera mpya ya Mazingira (2020).
“Lengo ni kuhuisha sera na kujumuisha maeneo mapya ya kimazingira kama vile kuongezeka kwa viumbe vamizi, taka za kielektroniki, matumizi ya kemikali na bioteknolojia ya kisasa yasiyo salama…” alisema Waziri Jafo.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.