Uwekezaji: Kilimo kivyoweza kuwatoa kimaisha vijana vijijini

January 19, 2023 7:18 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali zashauriwa kuwekeza katika sekta ya kilimo ili kuwawezesha kujiajiri.
  • Wadau wasema hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza njaa duniani.
  • Tanzania nayo yajitosa kuwainua vijana kwenye kilimo. 

Dar es Salaam. Mabalozi wawili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Kilimo Duniani (IFAD), Sabrina Dhowre Elba na mumewe Idris Elba wamezitaka serikali duniani kuwekeza kwa vijana waliopo vijijini ili kuinua sekta ya kilimo. 

Hotuba ya Sabrina katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos, Uswisi amesisitiza umuhimu wa sekta binafsi katika kuwekeza vijijini kwa kuwa, “jamii za vijijini zimesheheni vijana wenye vipaji, masoko na uwezo. 

“Tumejionea wenyewe. Si kwamba wanaweza tu kujilisha wenyewe, bali wanaweza na wasaidiwe ili walishe dunia,” amesema Sabrina jana Januari 18, 2023.

Takribani watu bilioni 3 wanaishi maeneo ya vijijini katika nchi zinazoendelea na kwa kiasi kikubwa tegemeo lao ni ukulimamdogo kwa ajili ya chakula na kujipatia kipato.

Akizungumzia kile alichoshudia wakati wa ziara zake akisema, “mara nyingi kwa wakulima wadogo, janga moja, au msimu mmoja wa mafuriko au ukame au kutokuvuna msimu mmoja kunawalazimu kuuza rasilimali zao ili waweze kujilisha.”

Taarifa ya IFAD iliyotolewa Roma, Italia inasema mathalani barani Afrika ambako matukio ya hali mbaya za hewa na mizozo vimeathiri zaidi uwezo wa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa familia zao, jamii na nchi, Idris na Sabrina wamekuwa wakitembelea na kuchagiza uwekezaji zaidi kwenye kilimo na maendeleo vijijini.

Mabalozi wema wa IFAD, Idris Elba (kushoto) na mkewe Sabrina Dhwore-Elba wakiwa na Mkurugenzi Mkuu wa IFAD Alvaro Lario baada ya kupokea tuzo ya mwaka 2023 ya Crystal huko Davos, Uswisi kunakofanyika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani, WEF. Picha | IFAD.

Licha ya jukumu hilo muhimu la wakulima wadogo katika kuhakikisha kuna uhakika wa chakula duniani, asilimia 75 ya watu wenye njaa na maskini zaidi duniani wanaishi vijijini katika nchi zinazoendelea.

Pamoja na mikutano na viongozi na taasisi mbalimbali, wawili hao wametembelea miradi kadhaa inayofadhiliwa na IFAD, mathalani huko Sierra Leone, Zambia na Kenya na kushuhudia changamoto za wakulima na kile wanachohitaji.

“Masikini wa dunia hii hawatafuti misaada bali wanataka uwekezaji. Uwekezaji kwa watu, mazingira, ugunduzi na ubia. Tukiweza kupata fedha zaidi, masoko, rasilimali, teknolojia, ufahamu na watu, tunaweza kuwa na mustakabali tofauti,” amesema Idris.

Kauli ya muigizaji huyo nguli imeungwa mkono na Rais wa IFAD, Alvaro Lario, ambaye amesema wito wake kwa viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi wanaoshiriki WEF ni kuongeza zaidi uwekezaji wa muda mrefu katika sekta ya kilimo kinachotekelezwa na wakulima wadogo.

“Ni kwa kuwekeza katika jinsi tunavyopanda, tunavyosindika, na kusambaza chakula chetu, ndipo mifumo yetu ya chakula iaweza kukidhi mahitaji ya dunia ya watu wenye afya na yenye afya sasa na siku zijazo,” amesema Lario.

Amekumbusha kuwa kutowekeza kwa kiasi kikubwa kutasababisha ongezeko la njaa, umaskini ambavyo baadaye vitachochea vurugu kwenye jamii, mizozo na uhamiaji.


Zinazohusiana: 


Tanzania yachukua hatua

Rais Samia Suluhu Hassan amesema sekta ya kilimo nchini inatarajiwa kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 ukilinganisha na ukuaji wa sasa wa takriban 3.6%.

Amesema Tanzania imetengeneza fursa za kitaifa kwa ajili ya mabadiliko ya mfumo wa chakula unaotarajia kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha maisha ya watu na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akichangia kwenye mada inayohusu masuala ya chakula ‘Food Action Partnership: Investing in Greater Resilience’, ikiwa mkutano mwingine wakati wa Jukwaa la Uchumi Duniani, Uswizi Rais Samia alizungumzia dira ya mabadiliko ya kilimo Tanzania.

Katika kudhibiti mfumo endelevu wa chakula nchini, Rais Samia amesema jitihada kadhaa zimefanyika, ikiwemo kuanzisha mradi kwa ajili ya vijana huku wakiendelea kuimarisha ukuaji wa shoroba za kilimo.

Jitihada nyingine zilizofanyika kuanzia mwaka huu wa fedha ni pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo mara 4 ukilinganisha na ile iliyopita. Aidha, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika Septemba 2023 kudhihirisha maendeleo hayo.

Mdahalo huo ulihudhuriwa na zaidi ya Viongozi 50 kutoka Afrika, Asia, Ulaya na Marekani kwa nia ya kuongeza kasi ya ushirikiano na uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya kila nchi.

Wachangiaji wakuu katika mdahalo huo mbali na Rais Samia walikuwa Rais Gustavo Petro wa Colombia, Tran Hong Ha, Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam na Bw Alvaro Lario, Rais wa Wakfu wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Roma.


Tangazo:


Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Nukta TV

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

Nukta TV