Shule 10 bora matokeo ya kidato cha nne 2022 hizi hapa

February 1, 2023 2:59 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni ni Kemebos, Feza Boys, na Graiyaki.
  • Shule kutoka Kanda ya Ziwa zang’ara zaidi.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali ya Tanzania kuondoa utaratibu wa kutangaza shule 10 bora ambazo zimefanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kitaifa, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imefanya uchambuzi na kubaini shule hizo zikiongozwa na Kemebos ya mkoani Kagera. 

Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) lilitangaza kuondoa utaratibu huo kwa kile kilichoitwa hauna tija kwani unawalinganisha watu ambao wamefanya mtihani mmoja lakini hawakusoma katika mazingira yanayofanana.

Hata hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda alipokuwa akitolea ufafanuzi suala hilo Bungeni jijini Dodoma leo Februali mosi amesema Serikali haijazuia watu wengine kusema shule bora ni zipi ila Necta ndiyo wamejiondoa katika utaratibu huo.

Nukta imetumia kigezo cha wastani wa ufaulu (GPA)  kati ya shule moja hadi nyingine kupata idadi ya shule 10 bora ambazo zilizofanya vizuri katika matokeo hayo yaliyotangazwa Januari 29 mwaka huu.

Orodha kamili hii hapa:

10. Marian Boys

Namba 10 ni shule ya wavulana ya Marian Boys iliyopo Mkoani Pwani ambapo katika watahiniwa 182 waliofanya mtihani wote wamepata daraja la kwanza na kuifanya shule hiyo kuwa na wastani wa ufaulu wa 1.2376.

Marian Boys inarejea katika nafasi 10 za juu mara baada ya kutokuweppo katika orodha hiyo mwaka 2021.

Katika matokeo hayo watahiniwa 78 wamepata daraja la kwanza pointi saba, 26 daraja la kwanza la pointi nane, 29 la pointi tisa, 20 la pointi 10 huku 13 daraja la kwanza la pointi 11, watano la pointi 12, watano la pointi 13, watatu la pointi 14,  watatu la pointi 16, na mmoja la pointi 17.


9. Bright Future Girls

Namba tisa imeshikwa na shule ya wasichana ya Bright Future iliyopo Jijini Dar es Salaam ambapo wanafunzi 113 waliofanya mitihani huo, wote wamepata daraja la kwanza.

Shule hii ina wastani wa ufaulu wa  daraja  A ambao ni 1.2287. Wanafunzi wake 39 wamepata daraja la kwanza la pointi saba, huku 16 la pointi nane. 15 wamepata daraja la kwanza la pointi tisa, 26 la pointi 10, sita la pointi 11, saba la point 12, wawili la point 13, na wawili ya point 14.

Tunaweza kusema shule hii imeporomoka kwani mwaka 2021 ilishika namba nne katika orodha ya shule bora ikiwa na wastani wa 1.2287.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Athumani Amasi. Picha | Esau Ng’umbi/Nukta.

8. Ahmes

Namba nane imeangukia kwa Shule ya Sekondari ya Ahmes kutoka mkoani Pwani ambayo watahiniwa wote 70, waliofanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne wamepata daraja la kwanza.

Ahmes nayo imerejea katika msimamo wa shule 10 bora nchini ikiwa na wastani wa ufaulu wa  1.2229 baada ya kutokuwepo katika orodha hii mwaka 2021. Imechukua nafasi ya Feza Girls ambayo ilishika nafasi hiyo mwaka 2021. 

Kati ya wanafunzi 70 hao waliofaulu kwa daraja la kwanza, 32 wako la daraja la kwanza la pointi saba, ikiwa ndiyo kiwango cha juu kabisa cha ufaulu. Nane wamepata daraja la kwanza la pointi nane.


7. Twiboki 

Kutokea Mkoani Mara, shule ya Twiboki imeingia kwenye orodha ya shule 10 bora zilizofanya vizuri kwenye mtihani wa kidato cha nne mara baada ya kupata wastani wa ufaulu wa 1.2222.

Shule imeingia katika orodha hiyo ya dhahabu baada ya kuing’oa Feza Boys katika nafasi hiyo. Hata hivyo, Feza Boys haikukubali kutoka katika orodha hiyo badala yake imepanda hadi nafsi ya nne. 

Tofauti na shule nyingine zilizopo katika orodha ya 10 bora, katika shule ya Twiboki, mwanafunzi mmoja tu mwenye matokeo ambaye amepata daraja la kwanza la pointi nane huku wenzake 66 matokeo yao yakizuiliwa.


6. Canossa

Namba sita imeturudisha jijini Dar es Salaam kwa shule ya Sekondari Canossa ambayo ina wastani wa ufaulu wa 1.2028 ambapo watahiniwa 120 waliofanya mtihani katika shule hiyo wote  wamepata daraja la kwanza.

Shule hii imeingia tena 10 bora baada ya kutokuwepo katika orodha hiyo mwaka 2021. 

Kati ya watahiniwa 120 waliopata daraja la kwanza, 72 wamepata daraja la kwanza la pointi saba, nane wamepata pointi tisa, 12 wamepata la pointi tisa, 13 wamepata pointi 10, watatu la pointi 11, sita la pointi 12.  Watatu daraja la kwanza la pointi 13, mmoja na 14, na mmoja aliyepata daraja la kwanza pointi 15.


Zinazohusiana: 


5.Waja Boys

Moja kwa moja mpaka Kanda ya Ziwa, ambako shule ya pili kutoka ukanda huo ya Waja Boys nayo imeingia 10 bora zilizofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022 ikishika nafasi ya tano.

Licha ya wanafunzi wote 44 waliofanya mtihani Waja Boys kufaulu kwa daraja la kwanza  shule hiyo  imeporomoka kwa nafasi mbili, kwani mwaka 2021 ilikuwa nafasi ya tatu kitaifa.

Ikiwa na wastani wa ufaulu wa 1.1742, wanafunzi  25 wamepata daraja la kwanza pointi 7, wanne daraja la kwanza pointi nane, tisa la pointi tisa, wawili la pointi 10, wawili pointi 11, na wawili pointi 12.


4.Feza Boys 

Kwa mara nyingine tena shule za Dar es Salaam zimeendelea kuonesha ubabe wao kwenye matokeo haya, Feza Boys ikiwa ni shule ya tatu kutokea jiji hilo linalokua kwa kasi Afrika Mashariki kuingia 10 bora. 

Feza ina wastani wa ufaulu wa 1.1506 ambapo wanafunzi wote 69 waliofanya mtihani wa kidato cha nne kwenye shule hiyo wamepata daraja la kwanza tu.

Feza imepanda kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya saba mwaka 2021, nafasi ambayo waliishikilia toka mwaka 2020.

Katika watahiniwa hao 69, watahiniwa 44 wamepata daraja la kwanza pointi saba, saba wamepata daraja la kwanza pointi nane na waliobaki wamegawana pointi zilizobaki.

3. St. Francis Girls

Moja kwa moja mpaka Mkoani Mbeya, ambako Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis imeshika nafasi ya tatu katika shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa kwenye mtihani wa kidato cha nne 2022.

St. Francis imeporomoka kwa nafasi moja kwani mwaka 2021 ilishika nafasi ya pili kitaifa ikiwa nyuma ya Kemebos. 

Mwaka 2022 watahiniwa 91, walifanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne kwenye shule hiyo ambapo wote wamepata daraja la kwanza, na hiyo kuifanya shule hiyo kuwa na wastani wa ufaulu wa 1.1449.

Wanafunzi 69 wamepata daraja la kwanza la pointi saba, huku 10 wakipata daraja la kwanza pointi nane, sita wamepata la pointi tisa, watatu la pointi 10 na watatu la pointi 11.


2. Graiyaki 

Kwa mara ya tatu tunarudi Kanda ya Ziwa na kwa mara ya pili tunarejea mkoani Mara, ambako Shule ya Graiyaki imekamata nafasi ya pili katika orodha ya shule 10 bora kitaifa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022.

Shule hii haikuwepo 10 bora ya 2021, ambapo watahiniwa wote 42 waliofanya mtihani kwenye shule hiyo wamepata daraja la kwanza na shule kuwa na wastani wa ufaulu wa 1.1164.

Kwenye matokeo yao, wanafunzi 34 wamepata daraja la kwanza la pointi saba, wawili wamepata daraja la kwanza la pointi nane, wawili la pointi tisa, watatu la poiti 10, na mmoja daraja la kwanza la pointi 11.


1. Kemebos 

Hatimaye kwa mara nyingine tena kutokea Kanda ya Ziwa, mkoani Kagera, shule ya Kemebos ndiyo imeibuka kinara, kwa kuongoza kwenye shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne.

Kemebos imeitunza nafasi hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo, ambapo walifanya hivyo mwaka 2020, 2021, na sasa 2022 wameshika tena nafasi hiyo mara baada ya wanafunzi 68 kupata ufaulu wa daraja la kwanza pekee.

Kati wanafunzi hao 68 waliopata daraja la kwanza, wanafunzi 65 wamepata daraja la kwanza la pointi 7, wawili daraja la kwanza pointi nane na mmoja daraja la kwanza pointi tisa.

Orodha hii ya shule ni kwa kuzingatia wastani wa ufaulu wa shule husika (GPA) ambao Serikali imesema utaratubu huo sio mbinu sahihi ya kupanga shule bora kwani hauzitendei haki baadhi ya shule.

Enable Notifications OK No thanks