Mambo ya kuzingatia unapoanza ‘freelancing’
- Ni pamoja kuwa na ufahamu wa uchumi wa kidijitali na ujuzi kutumia mitandao ya kijamii.
- Ni njia rahisi kwa vijana kuingiza kipato na kuboresha maisha yao.
Dar es Salaam. Dunia inakwenda kasi kwa sababu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia, mabadiliko hayo pia yameathiri jinsi watu wanavyofanya kazi, kwa sasa, siyo lazima mtu aajiriwe na kufanya kazi saa 5 hadi 9.
Unaweza kufanya kazi sehemu yoyote na muda wowote ukiwa katika mtandao wa intaneti. Kwa lugha ya Kiingereza inaitwa “Freelancing”.
Freelancing au ajira huru au kujitegemea ni aina ya kujiajiri ambapo watu wanafanya kazi kwa ajili yao wenyewe, badala ya kufanya kazi kwa kampuni.
Wafanyakazi huru kwa kawaida hutoa huduma zao kwa wateja wengi kwa msingi wa mkataba au mradi. Wanawajibika kwa kuweka viwango vyao wenyewe, kusimamia muda wao, na kutangaza huduma zao.
Asilimia kubwa ya watu waliopo katika aina hii ya ajira wana ujuzi ambao unahitajika sokoni ili kuboresha maisha ya watu.
Mitandao kama Fiverr, Freelancer.com, Upwork ni majukwaa yanayotumika kutangaza kazi na huduma ili kutoa fursa kwa watu kufanya kazi wakiwa kokote duniani.
Soma zaidi
-
Matumizi huduma za kibenki mtandaoni yapaa Tanzania, thamani yafikia Sh123 trilioni
-
Kitendawili: Kwa nini ‘ngada’ inalimwa zaidi Tanzania licha ya operesheni kali za dawa za kulevya?
Kazi nyingi za ‘freelancing’ zinapatikana katika taaluma za muziki, uandishi, uigizaji, usanidi programu (software development), kuunda wavuti (web designing), ubunifu michoro (graphics designing), ukalimani, marekebisho ya kiufundi, na utengenezaji wa filamu na video.
Kevin Metili, mwandishi wa makala aliyejiajiri ameiambia Nukta Habari kuwa ili kufanya kazi kama freelancer, vijana wanatakiwa kutengeneza mtandao wa watu ambao watafanya nao kazi.
“Kazi nyingi nimepata kwa kujichanganya na watu na kuweza kuwauzia huduma yangu kwa mazungumzo, sikumbuki kutumia mitandao ya kijamii, kazi nzuri inauza yenyewe, wateja wananifikia kwa kuambiwa na wateja wenzao,” anasema Metili ambaye amekua freelancer kwa miaka mitatu.
Metili ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya nguvukazi, ajira za kujitegemea ni njia rahisi kwa vijana kuingiza kipato na kuboresha maisha yao.
Mambo ya kuzingatia
JoanLisa Runyoro, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayowaunganisha vijana wenye ujuzi wa ufundi stadi na wateja ya Toolboksi, ameiambia Nukta Habari kuwa, jambo muhimu kabla ya kufanya freelancing ni kuwa na ujuzi wa kutosha wa kazi husika.
“Sio rahisi kutoboa bila ya kuwa na ujuzi na ufahamu wa uchumi wa kidijitali na kuweza kutumia mtandao, fursa nyingi zimejikita katika ubunifu tofauti na kazi za kiuhandisi,” amesema Runyoro.
Runyoro amesisitiza kuwa freelancing si rahisi kama wengi wanavyotafsiri kwani inahitaji kuwa na nidhamu na uwezo wa kujisimamia vitu ambavyo vijana wengi hawana.
Kwa nini uwe freelancer?
Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zaidi ya vijana milioni 10 hadi 12 wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka ambapo ni vijana milioni tatu pekee hufanikiwa kupata ajira.
kwa kuwa si wote wanaweza kuajiriwa katika mfumo rasmi unaweza kujiongeza kwa kujiajiri kupitia freelancing.
Mkurugenzi wa Sahara Venture, kampuni inayojihusisha na ushauri wa biashara, mitaji wezeshi kwa kampuni zinazochipukia, Jumanne Mtambalike ameandika katika ukurasa wake wa medium kuwa kutegemea kuajiriwa pekee sio suluhu ya changamoto ya ukosefu wa ajira unaozikumba nchi nyingi duniani.
“Freelancers’wamekua chachu ya maendeleo ya biashara, wanaongeza wigo mpana wa maamuzi ya waajiri pamoja na kupunguza gharama za rasilimali watu, kuchochea ubora wa huduma na mahitaji ya muhimu kama afya, kunaweza kushughulikiwa kwa kujiajiri,” amebainisha Mtambalike.

Kazi za freelacing mara nyingi huhitaji kuwa na kompyuta/ kompyuta mpakato au simu janja ili kzikamilisha. PichalUnsplash.com
Changamoto ya ‘Freelancing’
Kwa mujibu wa chapisho la ABC Attorneys, ajira za kujitegemea bado zina changamoto nchini Tanzania. Mazingira ya kazi si salama, kazi sio za uhakika, hakuna fidia kama bima au huduma za afya, na malipo mengine.
Kevin Metili, anasema changamoto alizokutana nazo kama freelancer ni pamoja na usimamizi wa muda kutokana na lundo la kazi alizopata.
“Pia nilikuwa na changamoto ya kujiamini haswa kwenye suala la pesa, hali iliyosababisha kushindwa kutoza wateja gharama iliyoendana na thamani ninayoongeza kwao, wateja wengine wana ugumu kulipa ukiwaambia gharama husika, watailinganisha na bei ya soko bila kuangalia thamani ninayowaongezea, ikawa inaleta mvutano,” anasema Metili.
Ni muhimu kabla ya kufanya kwanza utafiti ili kubaini aina ya kazi unazoweza kufanya kulingana na ujuzi wako, soko lake pamoja na kiwango cha malipo kinachotozwa kwa huduma husika.
Hii itakusaidia kuokoa muda wa kutafuta wateja pamoja na kutoza gharama kulingana na thamani ya kazi uliyoifanya, je wewe freelancer? una ujuzi wowote ungependa kushare nasi, unaweza kututumia andiko lako kupitia barua pepe info@nukta.co.tz au nambari ya simu 0677088088.
Latest