Serikali ya Tanzania yafungia gazeti la Raia Mwema kwa siku 30
- Gazeti hilo linakuwa la pili kufungiwa ndani ya kipindi cha mwezi mmoja baada ya gazeti la Uhuru.
- Raia Mwema wana nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 30 iwapo hawajaridhika na uamuzi wa Serikali.
Dar es Salaam. Serikali imelifungia gazeti la Raia Mwema kwa siku 30 kwa madai ya kuchapisha habari za uongo ikiwa ni gazeti la pili kufungiwa ndani ya mwezi mmoja.
Mkurugenzi wa Huduma za Habari Gerson Msigwa ameeleza kwenye taarifa yake kwa umma Jumapili (Septemba 5, 2021) kuwa uamuzi wa kusitisha leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo umekuja “kutokana na mwenendo na mtindo wa uandishi wa habari na makala ambao unakiuka misingi ya taaluma ya habari kwa kufanya upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa na uchochezi wa bayana.”
“Kwa kufanya hivyo, gazeti hili limekiuka masharti ya leseni lililopewa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuleta chuki miongoni mwa jamii na vile vile kuwafanya wananchi waichukie Serikali na viongozi wake,” amesema Msigwa.
Msigwa, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, ametoa mifano ya habari tatu za hivi karibuni zikiwemo zenye vichwa vya habari “Hamza wa CCM ni hatari” na “Maumivu mapya 17”.
Katika habari yenye kichwa cha habari “Maumivu mapya 17”, Msigwa amesema kuwa gazeti hilo limekiuka kwa kuchapisha na kusambaza habari zinazoleta taharuki miongoni mwa jamii na wananchi kwa kuonyesha kuwa Serikali inawaletea maumivu kwa kuwaletea tozo 17 za kazi mbalimbali za wasanii.
Leseni ya Gazeti la Raia Mwema yasitishwa kwa siku 30. pic.twitter.com/IUWiJnwbfp
— Gerson Msigwa (@MsigwaGerson) September 5, 2021
Habari hiyo na nyingine, Msigwa amesema zinakiuka Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016.
Msigwa amesema kuwa gazeti hilo, linalosifika kwa habari na makala za uchambuzi, lina haki ya kukata rufaa kwa waziri wa habari iwapo hawajaridhika na uamuzi huo ndani ya siku 30.
Katika adhabu hiyo inayoanza Septemba 6, Msigwa amesema, wanaamini kuwa itawapa nafasi ya kuboresha masuala yanayohusu weledi wa uandishi wa habari na utekelezaji wa masuala yote yanayohusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
Raia Mwema linakuwa gazeti la pili kufungiwa kwa muda ndani ya mwezi mmoja baada ya Serikali kusitisha kwa wiki mbili leseni ya uchapaji na usambazaji ya gazeti la Uhuru linalomilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Gazeti la Uhuru ambalo limesharejea sokoni baada ya kumaliza adhabu yake, lilifungiwa Agosti 11 baada ya kuchapisha habari iliyodai kuwa Rais Samia Suluhu Hassan hana nia ya kuwania kinyang’anyiro cha urais mwaka 2025.
Uongozi wa Raia Mwema haukupatikana mara moja kuelezea hatua hiyo ya Serikali kulifungia gazeti lao.
Latest