Miaka miwili: Airtel yaipatia Serikali ya Tanzania Sh122 bilioni

January 26, 2022 7:33 am · Wilson
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha hizo ni za gawio, kodi, malipo ya kila mwezi na uendeshaji wa minara ya simu.
  • Fedha hizo zimesaidia katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya kijamii.

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Airtel imetoa Sh122 bilioni katika kipindi cha miaka miwili ikiwemo gawio pamoja na kodi nyingine kwa Serikali ya Tanzania ambazo zimetumika kugharamia miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania aliyemaliza muda wake, George Mathen amesema katika kipindi chake cha miaka miwili na nusu cha kuongoza kampuni hiyo amefanikisha kutoa gawio na malipo mengine kwa Serikali yenye thamani ya Sh122 bilioni.

“Kati ya fedha hizo, Sh42 bilioni ni gawio kutokana na Serikali kumiliki hisa kwenye kampuni, Sh44 bilioni ni malipo baada ya kuhamisha umiliki wa minara yake kwenda kampuni ya minara pamoja na kiasi kingine cha Sh34 bilioni  zinazotokana na malipo ya kila mwezi ya Sh1 bilioni kwa kampuni hiyo ya minara tangu ilipoingia nayo makubaliano ya kuendesha minara ya mawasiliano kuanzia Mwezi Aprili 2019,” amesema Mathen.

Fedha hizo zilizotolewa Airtel Tanzania ambayo inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na kampuni ya Bharti Airtel ya nchini India zitasaidia katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na maji.


Soma zaidi:


Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ameipongeza kampuni hiyo kwa mafanikio makubwa na kueleza kuwa fedha hizo zimeiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kijamii ambayo ni chachu ya maendeleo.

“Fedha hizo zimeiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kijamii ambayo imekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi na kubadilisha maisha yao,” amesema Dk Nchemba.

Bharti Airtel waliingia katika mgogoro na Serikali baada ya kubainika kuwa mchakato wa ubinafsishaji wa Airtel Tanzania hapo awali uligubikwa na udanganyifu jambo lililomfanya Rais Magufuli kutangaza mwaka 2017 kuwa kampuni ilikuwa ni mali halali ya TTCL.

Hata hivyo, baada ya majadiliano ya awamu tano kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Profesa Palamagamba Kabudi, Serikali ilifikia makubaliano na kampuni ya Bharti Airtel yakiwemo kutoa malipo maalum ya Sh1 bilioni kila mwezi kwa miaka mitano, kubadili muundo wa bodi na menejimenti na kuongeza umiliki wa Serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 bila malipo yeyote.

Baada ya makubaliano hayo, kwa sasa Serikali inamiliki hisa za asilimia 49 katika kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano ya simu nchini Tanzania. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW